KISIMA CHA MAJI YA UZIMA NI KILE KILE CHA ZAMANI.

KISIMA CHA MAJI YA UZIMA NI KILE KILE CHA ZAMANI.

 kisima cha maji ya uzima ni kile kile cha zamani. Hakitachimbwa kingine.

Shalom, Jina la Bwana wetu YESU KRISTO libarikiwe daima. Leo tutajifunza tena habari ya Isaka,.. kisha tuone ni nini Bwana anataka tujifunze kwa Mababa zetu hawa wa Imani,.. Mungu kujiita, yeye ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, halafu akagotea hapo hakuendelea mbele, alikuwa anayo maana kubwa, Hivyo tunapaswa tujifunze sana juu ya watu hao watatu kwasababu zipo siri nyingi za ufalme zimelala hapo…

Kuhama kwa Isaka:

Tukisoma Mwanzo 26 tunaona kuna wakati njaa kali ilipita katika nchi yake,..Hivyo Isaka akalazimika kuhamisha makao yake kwa muda na kwenda kukaa kwa wafilisti,. lakini huko alipofika Mungu akamfanikisha kupita kiasi akawa Tajiri kiasi cha kuogopesha mpaka wenyeji kumwonea wivu na kumfukuza mpikani mwao,.. lakini alipokuwa huko ilimpasa pia awe na visima vya maji vya kulisha mifugo yake pamoja na watumwa wake, na watu wa nyumbani mwake wote..Lakini tunasoma Isaka hakuchimba kisima chochote kipya katika nchi ile bali alivifukua vile vile vilivyokuwa vimechimbwa na baba yake Ibrahimu tangu zamani sana ambavyo wafilisti walikuwa wamevifukia, na hapo ndipo somo letu la leo lilipo…

Embu Tusome wote sasa:

Mwanzo 26:15 “Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi.

16 Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.

17 Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko.

18 Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye.

19 Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika.

20 Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.

21 Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.

22 Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.

23 Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba”.

Isaka japokuwa alikuwa ni Tajiri, mwenye uwezo wa kuchimba visima vingine vingi vipya,.. lakini yeye hakufanya hivyo bali alivifukua visima vilevile vilivyochimbwa na Baba yake zamani…japo vilikuwa vimeshafukiwa na wafilisti havifai tena, lakini yeye alivifukua hivyo hivyo..kwasababu alijua anachokitafuta

Alitambua kuwa si kila Kisima kilicho mbele yake ni cha kunywa maji yake..

TUNAJIFUNZA NINI SISI WATU WA AGANO JIPYA?

Hata leo hii vipo visima vingi, vinavyodai kutoa maji, wengine kwao elimu ndio Kisima pekee,.. wengine biashara, wengine uongozi, wengine kipaji..wengine umaarufu n.k…lakini kipo Kisima kimoja tu chenye uwezo wa kutoa maji yaliyo hai yenye uzima, ambacho mtu akinywa kwa kupitia hicho, hataona kiu milele..

Watu wengi wamejaribu kukifukia Kisima hiki tangu siku ile ya Pentekoste,..na kikaonekana kweli kama kimeshafukiwa na kupotea kabisa,.. wakati ule kanisa lilipopitia kipindi kirefu cha giza, kwa miaka Zaidi ya elfu moja..lakini kuanzia karne ya 15 kilianza kuchimbuliwa tena na wajenzi ambao Mungu alishaweka tayari kwa kazi kama hiyo, kama vile Calvin,Martin Luther, John Wesley, na wengineo, na mpaka kufikia karne ya 20 yaani kuanzia mwaka 1906 na kuendelea kikaonekana kikitoa maji tena, yale yale yaliyokuwa yanabubuja wakati wa Pentekoste ya kwanza ya mitume…yaani Mambo yale yale yaliyokuwa yanafanyika katika kanisa la Kwanza, yalianza kuonekana tena yakifanyika katika kanisa hili la mwisho…Ndiyo tuliyaona yakianza na wakina William Seymour, William Branham na wengineo…Na hata sasa yule yule anaendelea kufanya kazi…HALELUYA!!

Roho yule yule aliyeachiliwa kipindi cha Pentekoste ambaye Kristo alisema kuwa yeye ndiye atakayeleta chemi chemi ya maji uzima, ndiye aliyemwagwa tena katika kanisa letu hili la mwisho la Laodikia..

Yohana 7:37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.

38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.

39 Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea.”

Kamwe usikoje maji haya ya uzima.

Lakini cha kusikitisha ni kuwa bado watu wanatafuta maji katika visima vingine,.. japokuwa hichi tayari kinaonekana kutoa maji mengi ya uzima tena bure, sio kwa kulipiwa kama vingine..Kaka/Dada ikiwa bado unaichezea hii neema, ipo siku utaitamani, na kuililia lakini utaikosa…Upo wakati utayatamani haya maji hata tone moja tu yakupe uzima lakini utayakosa…

Yule Tajiri aliyekuwa kule kuzimu aliye mwomba Lazaro achovye ncha ya kidole chake katika maji amnyweshe alikuwa hazungumzii maji ya bombani..hapana bali maji ya uzima, walau kidogo tu,.. yaani arudishwe duniani kuhubiriwa injili kwa dakika moja tu atubu aokoke kisha afe tena..Lakini ilishindikana na ndio maana akaomba basi ndugu zake wahubiriwe injili ili wasifike pale alipo..hakuomba ndugu zake wapewe maji mengi sana na washibe vizuri, ili wakifa wasisikie kiu huko aliko, au hakuomba wabebe maji ya kunywa kusudi huko wanakokwenda wawe naye mengi.. hapana aliomba wahubiriwe injili…kwasababu alijua hayo ndio maji ya uzima..

Leo hii itakufaidia nini upate, utajiri wote, upate elimu yote, upate umaarufu wote,.. na ujuzi wote, halafu unakufa ghafla, au kwa uzee mwema na kujikuta upo kuzimu.?..Ni kwanini leo hii usitafute jambo ambalo litakulinda sio tu ukiwa hapa duniani, bali pia hata huko unapokwenda….

Usipuuzie maji ya uzima, maji yaleyale yaliyochimbwa na mababa zetu mitume…Hayo ndio tunayoyaamini, na kumethibitishwa maji mengine, ni batili.

Bwana Yesu alimalizia na kwa kusema..

Ufunuo 21:6 “Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure” Amen.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.

KAZI YA UZURURAJI WA SHETANI.

SEHEMU ISIYO NA MAJI.

INGIENI KWA KUPITIA MLANGO ULIO MWEMBAMBA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments