USITUMAINISHWE NA MANENO YA UONGO.

USITUMAINISHWE NA MANENO YA UONGO.

Kwanini usitumainishwe na maneno ya uongo?

Kipindi kifupi sana kabla ya Hukumu ya Mungu kuja juu ya mtu, au juu ya nchi , au juu ya ulimwengu. Shetani huwa ananyanyua wimbi kubwa la manabii wa uongo, ambao kazi yao inakuwa ni kupunguza makali ya hukumu inayokuja. Shetani anajua kabisa watu wakiitafakari sana hukumu ijayo watatubu na hivyo atawapoteza na yeye hataki hata mmoja akose kwenda jehanamu pamoja na yeye, ndio lengo lake kubwa.

Tuutazama mfano mmoja katika biblia ambao utatupa mwanga kamili juu ya jambo hili. Mfano huu tunaoutoa kwenye Biblia kwasababu kila neno ili liwe kweli ni lazima lilinganishwe na biblia. Neno lolote linalotoka au kuhubiriwa kama halilingani au halipo kwenye biblia basi Neno hilo ni uongo. Hivyo tutamua biblia kuthibitisha mambo yote.

Tukisoma kitabu cha Wafalme wa pili, tunaona kuna wakati Maovu ya Wana wa Israeli yalifikia kiwango kikubwa sana mpaka Mungu akawatabiria kwamba watachukuliwa tena utumwani kama walivyochukuliwa wakati wa Farao wa Misri. Hivyo aliwaonya kwa kutumia watumishi wake wengi(manabii) watubu lakini hawakutaka (Soma 2Nyakati 36:15-17). Na hivyo kufikia kiwango ghadhabu ya Mungu kuachiliwa juu yao, kwa kuchukuliwa kwenda utumwani Babeli, na wengi wao kuuawa.

Lakini ni kwanini hawakutubu na kuishia kuangamizwa?

Ni kwasababu waliwasikiliza manabii wa Uongo badala ya kuwasikiliza manabii wa kweli wa Mungu. Kipindi hicho kulikuwa na manabii wa kweli wa Mungu kama vile Nabii Isaya ambaye alikuwa anawaonya juu ya maangamizi yanayokuja mbele yao, na kwamba wasipotubu watachukuliwa utumwani, lakini walimdharau. Bwana akamtuma na Nabii Yeremia ambaye aliwaonya na kuwaambia katika hali waliyofikia, kwenda utumwani watakwenda tu.

Hivyo wasitafute hata kupigana bali wajinyenyekeze kwa Nebukadneza, lakini badala yake wakamfunga na kumwona kama mtu asiye na Uzalendo na nchi yake na ni nabii wa uongo na kibaraka wa Nebkadneza. Hivyo wakawasikiliza manabii wengine ambao waliwatabiria mema. Kwamba hawatakufa, hawatapatikana na madhara, watastawi katika nchi ya Ahadi waliyopewa. Waliowatabiria kwamba watajenga na kupanda na kustawi. Manabii hao hawakugusia habari za maasi yao na kwamba wasipotubu watauawa, wao wakawahubiria habari za raha tu na amani..

Tunamsoma Nabii mmoja wa uongo anayeitwa HANANIA. Huyu ni mmoja wa walioibuka kipindi hicho cha Nabii Yeremia ambaye alikuwa anawatabiria watu amani kwamba kutakuwa shwari. Watu wasiogope Mungu bado yupo na wao, hajawaacha. Kamwe Nabii huyu hakuwahi kuwagusia habari za dhambi zao wanazozitenda zinazowafanya Mungu akae mbali nao, yeye aliwahubiria tu amani na mafanikio.

Tusome.

Yeremia 28:1 “Ikawa, katika mwaka ule ule, mwanzo wa kutawala kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, mwaka wa nne, mwezi wa tano, HANANIA, mwana wa Azuri, nabii, wa Gibeoni, akasema nami ndani ya nyumba ya Bwana, mbele ya makuhani na watu wote, akisema,

2 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimeivunja nira ya mfalme wa Babeli.

3 Kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, nitavirudisha mahali hapa vyombo vyote vya nyumba ya Bwana, ambavyo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, aliviondoa katika mahali hapa, akavichukua mpaka Babeli.

4 Nami nitamrudisha hapa Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, pamoja na mateka wote wa Yuda, waliokwenda Babeli, asema Bwana; maana nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.

5 Ndipo nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, mbele ya makuhani, na mbele ya watu wote waliosimama ndani ya nyumba ya Bwana,

6 naam, nabii Yeremia akasema, Amina, Bwana na atende hivi; Bwana ayatimize maneno yako uliyotabiri, kuvirudisha hapa vyombo vya nyumba ya Bwana na watu wote waliofungwa, toka Babeli, hata mahali hapa.

7 Lakini lisikilize sasa neno hili nilisemalo, masikioni mwako, na masikioni mwa watu wote, 8 Manabii waliokuwako kabla ya zamani zangu, na zamani zako, walitabiri juu ya nchi nyingi, na juu ya falme kubwa, habari ya vita, na ya mabaya, na ya tauni.

9 Nabii atabiriye habari za amani, neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa Bwana amemtuma kweli kweli.

10 Ndipo nabii Hanania akaitwaa hiyo nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, akaivunja.

11 Naye Hanania akanena mbele ya watu wote, akisema, Bwana asema hivi, Hivyo ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, na kuiondoa shingoni mwa mataifa yote. Basi nabii Yeremia akaenda zake”.

Upotoshaji wa nabii Hanania.

Huyu (HANANIA), Nabii wa uongo… Kawadanganywa wana wa Israeli kwasababu wanapenda faraja, hawapendi kushutumiwa, hawakupenda kukemewa maisha yao ya dhambi, ya uasherati wanaoufanya, ya ulevi, ya anasa, ya wizi na ushoga na chuki, na uabuduji sanamu..moja kwa moja wakamwamini Hanania na hivyo wakapumbazika, kuamini kwamba katumwa na Mungu. Sasa sikia Bwana kipindi kifupi tu baadaye Bwana alichomwambia Nabii Yeremia.

Yeremia 28: 15 “Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini UNAWATUMAINISHA WATU HAWA MANENO YA UONGO.

16 Basi Bwana asema hivi, Tazama, nakutuma uende zako toka juu ya uso wa nchi; mwaka huu utakufa, kwa sababu umenena maneno ya uasi juu ya Bwana.

17 Basi nabii Hanania akafa, mwaka uo huo, mwezi wa saba”.

Kujirudia kwa yale yale duniani leo.

Umeona hapo?. Mambo yaliyotokea kipindi hicho ndiyo yanayotokea sasa kipindi hichi tunachoishi sasa. Shetani ameshajua tumeukaribia mwisho sana hivyo watu wote wanaanza kufikiri juu ya hukumu ijayo, ya moto wa umilele.

Na hataki mtu hata mmoja akose kuingia jehanamu, kwahiyo ili kuwapumbaza watu ananyanyua JOPO KUBWA LA MANABII WA UONGO!, Ambao kazi yao kubwa ni KUWATUMAINISHA WATU KWA MANENO YA UONGO..Kwamba hakuna hukumu!..Kwamba Dunia bado sana iishe, kwamba Mungu hawezi kuwatesa watu kwenye moto, kwamba usifikirie sana kuhusu mambo yajayo baada ya maisha haya…Watakazana kufundisha na kuhubiri namna ya kupata pesa!. Namna yakufunguliwa kiuchumi, namna ya kutoka kimaisha..Lakini kamwe hawatafundisha namna ya kutoka kwenye dhambi!!. Wana macho ya kuona kesho utaolewa, lakini hawana macho ya kuona kesho utakwenda jehanamu kama usipotubu. Wanaona maono ya wewe Kesho yako itakuwa ni ya kicheko, lakini hawaona maono kuwa Kesho yako itakuwa ni kilio na kusaga meno kama utaendelea kuishi na huyo mke ambaye si wa kwako, na huyo mume ambaye si wa kwako, na huo ulevi ambao unaufanya sasa, na hizo biashara haramu ambazo unazifanya sasa.

Ni wangapi leo hii wana maswali mengi yahusuyo maisha baada ya kifo na hawapati msaada wowote. Zaidi sana kila wanapokwenda wanaambiwa habari za kutabiriwa ndoa zao na biashara zao?. Huyo mtu akiwa tajiri namba moja duniani na akifa katika ulevi wake, au uasherati wake, au kutokusamehe kwake? au visasi vyake alivyonavyo moyoni. Huo utajiri vitakwenda kumsaidia nini huko?.

Tumeonywa tujihadhari.

Biblia inasema katika 1 Wathesalonike 5:3 “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Kama hujasamehewa dhambi zako fahamu kuwa ni maelfu wamesamehewa dhambi zilizo nyingi kuliko za kwako bure na Bwana Yesu na anaendelea kutusamehe kila siku. Hivyo nafasi hiyo ya kipekee isikupite, kabla mlango wa Rehema kufungwa. Wakati ambao watu watatubu lakini hatawasikia. Hivyo unachopaswa kufanya ni kujitenga mahali ulipo kwa dakika chache. Na kutubu kwa kukiri makosa yako yote na kuahidi kutokutenda tena, na unaacha kwa vitendo. Hiyo ni hatua ya kwanza. Hatua ya pili kama hujabatizwa katafute ubatizo sahihi kwa maji mengi (Yohana 3:23) na kwa jina la Yesu kwaajili ya ondoleo la dhambi zako kulingana na (Matendo 2:38). Na baada ya hapo Roho Mtakatifu atakusaidia kufanya yaliyosalia ikiwemo kukupa uwezo wa ajabu kushinda dhambi, na kukupa uwezo mkubwa wa kuyaelewa maandiko.

Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Nitamjuaje nabii wa Uongo?

JIEPUSHE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

EPUKA MUHURI WA SHETANI

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

 

JINSI WATU WANAVYOZAMA KATIKA USHIRIKINA NA UCHAWI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments