JIEPUSHE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

JIEPUSHE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

Jina la Bwana libarikiwe. Karibu tujifunze Biblia..

Hatari kubwa iliyopo katika siku hizi za mwisho ni Kunyanyuka kwa jopo kubwa la Manabii wa Uongo…Sasa biblia inapotaja uwepo wa manabii wa uongo, haimaanishi tu manabii bali hata waalimu, wainjilisti, mitume, wachungaji, maaskofu, mashemasi(2Petro 2:1) n.k…Yaani kwa ufupi kila karama ina waongo wake…Sasa watumishi wote hao wa uongo biblia imewapa jina moja la ujumla ambalo ndio hilo MANABII WA UONGO.

Kwahiyo akitokea mwalimu anafundisha uongo huyo ni Nabii wa Uongo wa siku za mwisho, kadhalika akitokea mchungaji anafundisha uongo huyo pia ni Nabii wa uongo kulingana na Biblia.

Sasa katika siku hizi za mwisho wameongezeka sana…Ni sababu gani imewafanya waongezeke kwa kasi kiasi hicho?? NI KWASABABU HIZI NI SIKU ZA MWISHO! HILO TU!..Hawajataka wenyewe kunyanyuka kwa nguvu zao hapana! bali kuna nguvu ya siku hizi za mwisho ndio zinazowanyanyua.

Umewahi kujiuliza kwanini karibia na mstari wa mwisho wa riadha, ndio watu wanongeza spidi? Na kelele za mashabiki ndio zinaongezeka?.. umewahi kujiuliza kwanini karibia na goli ndio nguvu za wachezaji zinajiongeza mara mbili?, na kelele zinakuwa nyingi uwanjani?..tofauti na mpira ukiwa katikati ya uwanja?…..ni kwasababu mpira unakaribia mwisho wa uwanja ambapo ni golini.…. karibia na mwisho kuna kitu kinawasukuma wamalizie kwa nguvu ili wafunge goli, na pia kama ukichunguza dakika 5 kabla mpira au mchezo wowote kuisha ndio kelele zinaongezeka uwanjani na wachezaji wanacheza kwa nguvu zaidi? Ni kwasababu mwisho umekaribia….kadhalika mstari wa siku za mwisho tunaoukaribia ndio unaoharakisha mambo kama tunavyoona….kama sio huo mstari wa siku za mwisho tunaoukaribia kuwa karibu na sisi, nguvu hii ya kuwasukuma watu kuzimu isingekuwa kubwa kiasi hiki…Kwasababu muda ungekuwa bado sana

Ndugu ipo nguvu kubwa ya upotevu katika hizi siku za mwisho, imeachiwa, ili imalizie kwa nguvu kuwapeleka watu upotevuni…Na pia kuna nguvu ya Mungu imeachiliwa kwa watu wa Mungu itakayowapeleka kwa nguvu uzimani. Hizo nguvu mbili ndio zinazotenda kazi sasa.

Wale wasiompenda Mungu, hii nguvu ya upotevu inawavaa…Sasa inawavaa vipi?

Mtu alikuwa anapenda ulevi, na haipendi injili inayomwambia aache pombe na hataki kutubu…Mungu anamletewa mhubiri wa uongo atakayemuhakikishia kwa maandiko kitu anachokifanya ni sawa mbele za Mungu..atahubiriwa pombe ni sawa kulingana na maandiko, na atatoka amesafishika akiamini anachokifanya ni sahihi, kumbe kasafishiwa Zaidi njia yake ya kwenda upotevuni…

Na ndio hivyo hivyo siku za mwisho Mungu atawaruhusu manabii wengi wa uongo, watimize kusudi lake, ingawa manabii hao watakuwa wametumwa na shetani.

2Timotheo 3:13 “Lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika”.

2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11 Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;

12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.

1 Wathesalonike 5: 3 “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Unaambiwa leo, uvaaji mbaya ni dhambi, uvaaji wa mawigi, vimini, na suruali kwa wanawake ni dhambi lakini hutaki kusikia..Utaletewa mhubiri, aliyesomea chuo cha Biblia kabisa, atakuhakikishia kwa maandiko kwamba vimini, mawingi, suruali, uwanja, lipstiki, sio dhambi…atakupa na vifungu vya biblia na atakuombea kabisa na utapokea hata uponyaji…

Na wewe utatoka umeamini kuwa upo sawa, kumbe tayari umepokea nguvu itakayokufanya kuendelea kufanya dhambi pasipo kuwa na mashaka yoyote..kwasababu mashaka ndio yanayomfanya mtu awe hapo katikati… na mtu aliye katikati anaonekana bado hajakomaa vizuri, hivyo ni ngumu kujua kama ni ngano au gugu…ili kujua ni ngano au gugu ndio inaachiliwa nguvu hiyo juu yake..ikishaachiliwa hiyo nguvu ndio inamfanya achague upande mmoja pasipo kuwa na mashaka…Hivyo ndivyo magugu na ngano vinavyotengwa.

Kadhalika Leo hii unaambiwa Ulimwengu na fahari zake unapita, na usijiwekee hazina duniani mahali ambapo nondo na kutu vinaharibu, unaambiwa usiupende ulimwengu, kwasababu kuwa Rafiki wa ulimwengu ni kuwa adui wa Mungu (Yakobo 4:4) na tena hivi karibuni dunia itafikia mwisho, kila kitu kitaharibiwa na waovu wote wataondolewa na hivyo kila kitu kitakuwa ni kazi bure.…lakini wewe hutaki kusikia hilo, unataka kulazimisha kuwa mambo ya ulimwengu huu yamekubaliwa na Mungu, na kwamba dunia haitaharibiwa kutaendelea kuwa na amani hivi hivi siku zote…. hata wakati mwingine unakejeli na kudharau wanaoukataa ulimwengu na kumtafuta Mungu…

Nataka nikuambie ukweli, ukweli kabisa wa dhati!! nguvu ya upotevu itaachiliwa juu yako…au pengine imeshaanza kuachiliwa ni hujui tu…Mungu atakuletea mhubiri, tena inawezekana akawa ni mhubiri maarufu sana, huyo atakuambia kwa kutumia maandiko matakatifu kuwa bado sana dunia iishe! Atakupa na historia ndefu yenye kutumia akili nyingi, atakuaminisha kuwa bado kuna miaka mingi ya hii dunia kuendelea kuwepo, hakutatokea vita wala matetemeko…hivyo usiogope! Endelea na shughuli zako, Mungu atafuata baadaye.

Ndugu yangu! Hao ni manabii wa Uongo, walioruhusiwa watokee siku hizi za mwisho..wanafanya kazi yao ya kupotosha ulimwengu mzima na wakishamaliza wataenda kuhukumiwa..

Tubu leo, ipende kweli na Itii Injili pasipo kuipunguza, Epuka kusikiliza injili hizi za manabii wa uongo, wanaokufariji katika dhambi, lakini hawakuambii ukweli kuwa, ukiendelea na Maisha ya dhambi unayoishi utakwenda kuzimu. Manabii hao ni asili yao ni kuzimu, na siku ile watu wengi sana watashangaa kuwaona Jehanamu.

Bwana anasema..

Yeremia 23: 15 “Basi Bwana wa majeshi asema hivi, katika habari ya manabii, Tazama, nitawalisha pakanga, nitawanywesha maji ya uchungu; kwa kuwa kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru kumeingia katika nchi yote.

16 Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana.

17 Daima huwaambia wao wanaonidharau, Bwana amesema, MTAKUWA NA AMANI; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.

18 Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia?

19 Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea; ni dhoruba ya kisulisuli; itapasuka, na kuwaangukia waovu vichwani.

20 Hasira ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtalifahamu neno hili kabisa.

21 Mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri”.

Kama hujayakabidhi Maisha yako kwa Kristo, unangoja nini?..Kama hujabatizwa ubatizo sahihi wa kuzama mwili wote na kwa Jina la Yesu ni nini unasubiri?..Mlango wa Neema upo wazi sasa, ila hautakuwa hivyo siku zote.

Bwana akubariki.


Mada Nyinginezo:

TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.

MPINGA-KRISTO NI NANI?

JE! MUNGU ATAIANGAMIZA DUNIA TENA BAADA YA GHARIKA YA NUHU?

MANENO HAYA YANA MAANA GANI? “..KWA SABABU HAMTOI ROHO KWA KIPIMO. (YOHANA3:34)”


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments