LIONDOE JIWE.

LIONDOE JIWE.

Ulishawahi kujiuliza ni kwanini siku ile Bwana Yesu alipofufuka kutoka katika wafu, hakupotea na kutokea nje ya kaburi kisha kuendelea na safari yake ya kuwatokea mitume, na watu wengine lakini kinyume chake ilimpasa kwanza jiwe la kaburini liondolewe, ndipo atoke?

Kimsingi Bwana Yesu alipofufuka alikuwa na uwezo huo wa kupotea na kutokea, utakumbuka alifanya hivyo kwa watu zaidi ya 500, Tukiachia mbali siku ile mitume walipokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya wayahudi, Yesu aliwatokea na kuanza kuzungumza nao, wala hakuhitaji kuingia kwa kupitia mlangoni.

Lakini tukirudi kwenye kaburi, ilikuwa ni lazima apitie kwenye malango yake, na kama ni hivyo basi ni sharti pia jiwe liviringishwe ili atoke, na ndio maana malaika walitokea juu na kuifanya kazi hiyo (Mathayo 28:2).

Lakini sio wakati huo tu, utakumbuka pia kifo cha Lazaro, Bwana Yesu hakumfufua Lazaro hivi hivi tu, bali aliwaambia kwanza wale watu waliokuwa  pale waliondoe jiwe kwanza ndipo shughuli za kufufua ziendelee. Hii ni kanuni ya kiroho ya Mungu, hakifufuliwi chochote bila kwanza kuondoa jiwe.

Yohana 11:39  “Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne….

43  Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. 44  Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”

Na sisi pia, ili tumwone Yesu aliyefufuka na nguvu zake, ni lazima tuyaondoe mawe mioyoni mwetu. Tusitazamie Yesu atafanya lolote, au atatenda muujiza Fulani, hiyo haipo, atafufuka kweli lakini hatoweza kutoka mpaka tutakapoyaondoa mawe hayo makubwa mioyoni mwetu.

Mawe hayo ni yapi?

Ni ule ugumu wa mioyo yetu.

Kama tunavyofahamu sikuzote jiwe ni gumu, tofauti na nyama..si rahisi kuathiriwa na chochote, ukilipitisha kwenye moto litakuwa vilevile, ukilipitisha kwenye upepo haliwezi kukakamaa, ukilipitisha kwenye maji haliwezi kulowa, ukilipiga upanga, ndio kwanza upanga unaumia.

Wapo watu ambao wanasema wamemwamini Kristo, lakini hawapo tayari Kristo ayatengeneze maisha yao, bado mawe yamefunika mioyo yao, wanataka maisha yao ya sasa, na yale ya kale yasiwe na utofauti, lakini wakati huo huo wanasema wameokoka. Hawajui kuwa ukristo ni badiliko la maisha moja kwa moja.

Wakiambiwa, wasivae mavazi yampasayo mwanamume, wanaona ni unyanyasaji wa kijinsia, wakiambiwa, biblia inasema tusiipende dunia, kwasababu tukiipenda dunia, tunafanyika maadui wa Mungu( 1Yohana 2:15)…watakuambia hizo ni zama za kale, wakiambiwa kubeti ni dhambi, wanajifanya kama hawaoni, wao kila jambo linalogusa maisha yao ya dhambi, hupinga tu..

Hata waonyweje, hawataki kubadilika, Sasa, haya ndio mawe yanayomzonga Yesu asifufuke katika maisha ya watu wengi wanaosema wamempokea Yesu. Kamwe hawawezi kuona nguvu ya kufufuka kwa Yesu katika maisha yao, Watausikia tu upendo wa Yesu, lakini moyoni mwao kutakuwa kukame daima, wataisikia amani ya Kristo, lakini kiuhalisia wao hawajawahi kuionja mioyoni mwao. Yesu atabakia kuwa kama mtu Fulani mashuhuri aliyewahi kutokea zamani, kama tu wengine, lakini sio mwokozi, anayebadilisha maisha ya watu.

Ndugu yangu, jiachie kwa Bwana akuongoze kwa  jinsi apendavyo yeye na sio kama upendavyo wewe, ndivyo utakavyouona wema wake, na nguvu zake maisha mwako. Ondoa jiwe hilo, mbele yako, liviringishe mbali, moyo wako uwe wazi ili Yesu atoke afanye kazi yake, na Bwana atayamalizia yaliyosalia sawasawa na ahadi yake katika;

Ezekieli 36:26 “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama”

Dunia ya sasa ni kujihadhari nayo sana, kwasababu, hata mpagani asiyemjua Mungu kabisa, ukimuuliza Je! Umempa Yesu maisha yako? Atasema ndio. Wokovu umepunguzwa na kufanywa kama staili tu, lakini sio geuko la maisha, Na ndicho shetani anachotaka kitokee kwako pia, ili kwamba usikae  uone nguvu za Yesu aliyefufuka katika maisha yako.

Hivyo ikiwa wewe ni mkristo vuguvugu, embu kuanzia sasa, amua kujitwika msalaba wako na kumfuata Yesu, usiogope kuonekana mshamba, usiogope kuonekana umerukwa na akili, hata Bwana mwenyewe, alionekana hivyo, sasa kwanini wewe uogope, usiogope kutengwa na ndugu kisa umeamua kubadili mfumo wa maisha.. Ondoa jiwe hilo linalouzinga moyo wako.

Bwana akutie nguvu.

Ikiwa hujaokoka na upo tayari kuanza maisha mapya ndani ya Kristo kwa kumaanisha kabisa, kuukataa ulimwengu na mambo yake yote, Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithibitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.

Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ikiwa utahitaji msaada wa hayo yote, basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

JIWE LILILO HAI.

Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika.

Biblia inapotumia neno “Bila kazi ya mikono”, ina maana gani?

CHAGUA NI JIWE LIPI LITAKALO KUFAA KWA UJENZI.

YESU MPONYAJI.

Ni kwa namna gani, upendo husitiri wingi wa dhambi? (1Petro 4:8).

URIMU NA THUMIMU NI NINI KATIKA BIBLIA?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Issaya Zakayo
Issaya Zakayo
1 year ago

Haleluya, Kwa nini wayahudi walipokuwa wanazika walikuwa wanaweka jiwe juu ya kaburi???

Anonymous
Anonymous
1 year ago
Reply to  Issaya Zakayo

Haleluya, Kwa nini wayahudi walipokuwa wanazika walikuwa wanaweka jiwe juu ya kaburi