YESU ANAKWENDA KUIBADILISHA OFISI YAKE.

YESU ANAKWENDA KUIBADILISHA OFISI YAKE.

Mungu anayo agenda, na usipojua agenda ya Mungu katika siku hizi za mwisho ni ngumu sana kuiona ile ng’ambo, Leo hii tunaishi maisha ya juu juu tu kwasababu hatujamjua YESU ni nani na tabia zake ni zipi kulingana na majira ya wakati.

Tunapenda kumjua tu katika ule upande wake mmoja, wa upole na unyenyekevu (Mathayo 11:29)..Lakini hatujui ule upande mwingine ambao anasema yeye ni MKEMEAJI, na MKANAJI, na MFUKUZAJI na MUUAJI WA WAOVU. Ikiwa leo hii hatutamwamini, halafu tukafa, au siku ile ya mwisho ikatukuta tupo katika njia zetu wenyewe, tujue kuwa tabia tutakazoziona kwake kipindi hicho zitatustaajabisha sana, tena sana.

Kanisa hili la mwisho tunaloishi linaloitwa Laodikia, ndio kanisa pekee kati ya yale saba, ambalo Bwana amelikemea vikali, kwa tabia zake, za kuwa vuguvugu.. Hii ikiwa na maana kuwa mimi na wewe kama tupo katika uvuguvugu huu uliopo sasa hivi duniani tujue kuwa tupo katika Hasira ya Kristo, ya kwenda kutapikwa.

Uvuguvugu wa kusema mimi nimeokoka, lakini maisha yako hayauhakisi wokovu ule wa kimaandiko, ndio tabia ya kanisa hili la mwisho ilivyo, mamilioni ya wakristo ndio hivyo walivyo leo hii. Jambo ambalo halikuwepo miaka ya zamani, ambayo watu hawakumchanganya Mungu na uovu, waliookoka walijulikana, waliokuwa waovu walijulikana. Hakukuwa na mtu aliyeshiriki meza ya Bwana na wakati huo huo ni mzinzi au mlevi, mtu anakwenda ibadani, halafu kesho pia anakwenda disco, hayakuwepo hayo. Waovu walijitenga, na watakatifu waliookolewa walijitenga, Lakini leo hii ni kawaida sana, kusikia hata mmiliki bar anasema ameokoka.

Ufunuo 3:15 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

3.16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi NAWAKEMEA, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami”.

Lakini pia hakemei tu peke yake, kuna siku atasimama KUWAKANA na kuwaonea aibu watu wengi sana, mbele ya Baba yake, na mbele ya  maelfu ya malaika zake huko mbinguni. Ikiwa leo hii unamwonea Kristo aibu unaogopa kuitwa mlokole, unaogopa kuvaa vizuri mavazi ya kujisitiri kisa utaitwa mshamba, unaona aibu kumtumikia Mungu wako, siku ile utakuonea aibu na wewe kweli kweli, hata hatapeleka jicho lake kukangalia.. wakati wengine akiwapongeza na kuwasifia.wewe utakuwa kama mtu baki tu.

Marko 8:38 “Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”.

Halikadhalika na kumkana vivyo hivyo, naye pia atakukana siku ile.

Kama hilo halitoshi Bwana Yesu pia anasema, atawafukuza watu wengi sana, siku ile, sio wachache, bali wengi sana. Na watakaofukuzwa sio watu wasiomjua Kristo bali, ni sisi sisi tuliopo kanisani, tunaolitumia jina lake kutenda miujiza lakini hatutaki kuishi maisha yampendezayo yeye. Tunapenda maisha ya uvuguvugu.

Mathayo 7:22 “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.

Biblia bado inatuonyesha siku ile atakapotokea mawinguni atawaua wanadamu wengi sana watakaokuwa wameipokea ile chapa ya mnyama na kufanya vita naye..

Ufunuo 19:13 “Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.

14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.

15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.

16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA Bwana WA MABwana”.

Unaweza kuona jinsi mwonekano wa Bwana utakavyokuwa wa tofauti sana wakati ule?. Ndio hapo utakapojua ni kwanini biblia inasema mataifa watamwombolezea, kwasababu hatakuja tena na sura ya upole kama wengi wetu tunavyodhani, bali atakuja na jina jipya la kifalme, la kuteka na kutawala, la kutiisha lenye nguvu nyingi. Sio tena la kuokoa mtu.

Lakini kwa upande wa pili, kwa wale waliomtii, waliokubali kutembea katika njia zake, anasema atawakiri, na kuona fahari kwa ajili yao mbele za Mungu na za malaika wake, vilevile atawapa mamlaka ya kutawala pamoja naye kama wafalme, Na atawafuta machozi watakatifu wake wote.

Hivyo ndugu, leo hii Kristo bado kaketi kama mwana-kondoo, aliyechinjwa, mpole, mnyenyekevu, aokoaye, anakuvuta kwa upole mwingi kwake, ili usiopote katika aungamivu wa ulimwengu. Angalia wakati huu umebakia mchache sana, kabla ya yeye kwenda kubadilisha ofisi yake. Kwanini usitubu umrudie muumba wako?

 Damu yake bado ipo kukuokoa, na kukusamehe kabisa, mkaribishe leo kwenye moyo wako, akupe uwezo mpya wa kuushindwa huu ulimwengu. Pengine ulishamwamini au kumpokea lakini umekuwa mkristo vuguvugu mkristo jin, jambo ambalo ndio halitaki kabisa, amelikemea, hivyo toka kwenye huo uvuguvugu wako, toka katika udhehebu, mfuate Yesu kweli kweli, ondoa vizuizi vyote vinavyokufanya usiwe safi mbele za Mungu.  Na yeye mwenyewe atakutengeneza na kukufanya uwe tayari kwa ajili ya kwenda kwenye unyakuo ambao upo karibuni kutokea.

Natumai sote tutaanzana kuuonyesha mabadiliko mapya. Kabla ya mabadiliko yake hayajajidhihirisha kwetu.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

UFUNUO: Mlango wa 2 part 3

UFUNUO: Mlango wa 14

ESTA: Mlango wa 8, 9 & 10. (SIKU KUU YA PURIMU)

UFUNUO: Mlango wa 19

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Nahitaji kupata masomo haya yote kwa whatsap maana kwa kweli yamenibariki haswa