UFUNUO: Mlango wa 2 part 3

UFUNUO: Mlango wa 2 part 3

Sehemu ya tatu.

BWANA wetu YESU KRISTO apewe sifa. Karibu katika kujifunza Neno la Mungu, leo tukiendelea na sehemu ya tatu, ya sura hii ya pili, ambapo tulishatangulia kuona lile Kanisa la Efeso na Smirna, pamoja na wajumbe na ujumbe wao kutoka kwa Bwana. Na hapa tutaona kwa ufupi kanisa lingine la tatu linaloitwa PERGAMO. Tunasoma

KANISA LA PERGAMO.

Ufunuo 2: 12 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili”.

Kama tulivyotangulia kujifunza tunaona hapa Bwana anaanza kwa kujitambulisha kama “yeye aliye na huo upanga mkali,wenye makali kuwili”. Tulishaona katika makanisa yaliyopita,kwamba ule utambulisho wa kwanza Bwana anaoanzana nao, una uhusiano mkubwa na ujumbe wa kanisa husika..Sasa hapa anaposema “yeye mwenye upanga mkali”, haimaanishi jambo jema sana kwa kanisa hilo, kama alivyojitambulisha katika kanisa la Smirna aliposema “yeye aliyekuwa amekufa kisha akawa hai” kuonyesha kwamba kuna tumaini baada ya kifo,.Lakini hapa ni tofauti, anaanza kwa kutamka upanga na upanga siku zote unaashiria vita, na tena anasema unatoka katika kinywa chake ikiwa na maana kuwa ataenda kufanya vita kwa kinywa chake, (Ambalo ndio Neno lake). Na pia kumbuka hapa hazungumzi na watu wa mataifa (yaani wasio wakristo na wasiomjua Mungu) hapana bali anazungumza na wakristo, na hao ndio atakaofanya nao vita kwa huo upanga utokao katika kinywa chake.. Lakini ni kwanini afanye nao vita?, tutakuja kuona hapo mbeleni sababu zenyewe:

Tukiendelea kusoma..:

” 13 Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani. “

Neno “Pergamo” tafsiri yake ni “NDOA”. Na Historia inaonyesha kanisa hili lilianzia mwaka 312WK na liliisha mwaka 606WK. Lakini hapa tunaona Bwana anawaambia watakatifu wa wakati huo kwamba anafahamu kuwa mahali walipokaa ndipo penye kiti cha Enzi cha shetani, (mahali penyewe tutapaona mbeleni) na pia ameona kuwa wamelishika sana jina lake wala hawakuikana imani, licha ya kwamba shetani alikuwa anawaua wakristo wengi, tangu kanisa lililotangulia nyuma hadi huo wakati waliokuwepo wakristo wengi waliuawa, hata katika siku za Antipa, ambaye alikuwa pia ni shahidi mwamifu wa Bwana aliyeishindania Imani mpaka kufa bila kuikana.Hawa wote hawakutikisika kwa lolote pamoja na dhiki hizo zote.

Lakini Bwana anaendelea kusema;

 ” 14 Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.

Baada ya shetani kuona kuwa watu bado wapo radhi kutoa hata maisha yao kwa ajili ya IMANI yao, akaona kwa njia ya vitisho na dhiki haina nguvu tena kuwatoa watu kwa Mungu, ndipo akabadilisha mbinu, na kuhamia kwenye njia ya udanganyifu, Na ndio maana hapo tunaona Bwana anasema ” unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu ” Swali ni je! haya mafundisho ya Balaamu ni yapi?.

Habari za Balaamu tunazipata katika agano la kale kitabu cha Hesabu 22. Tunasoma kuwa wakati wana wa Israeli wakiwa jangwani katika safari yao ya kuelekea nchi ya ahadi walikutana na wana wa Moabu njiani, na walipotaka kukatiza katika nchi yao mfalme wao aliyeitwa Balaki aliwazuia. Na zaidi ya yote akaenda kumwajiri Balaamu nabii wa uongo ili awalaani wana wa Israeli (Kuwaloga) wasifanikiwe katika safari yao. Hivyo Bwana alimzuia Balaamu mara tatu asiwalaani, na kinyume chake akawabariki. Lakini haikuishia hapo Balaamu yule nabii wa uongo kwa kupenda fedha ya udhalimu, kutoka kwa mfalme Balaki alitafuta njia mbadala ya kuwakosesha wana wa Israeli. Ndipo akamshauri Balaki afanye karamu na kuwaalika wanaume wa Israeli ili wafanye uzinzi na wanawake wa kimoabu na kutoa sadaka kwa miungu yao, ili iwe ukwazo kwao kwa Mungu wa Israeli na Mungu awaadhibu. Hivyo njama yake kweli ilifanikiwa, na hasira ya Mungu ikawaka juu ya Israeli, nao wakaadhibiwa kwa kosa lile. Hivyo tunaona hapo Balaamu ndiye aliyekuwa chanzo cha kuwakosesha Israeli.

Vivyo hivyo katika hili kanisa la Pergamo, Kumbuka kwa wakati ule Rumi ndiyo iliyokuwa inatawala dunia, na utawala ule ulikuwa ni utawala wa kipagani, Lakini ilifika wakati mtawala wa Rumi aliyeitwa KONSTANTINI alipokuwa anataka kwenda kupigana vitani dhidi ya maadui zake, aliota ndoto na akaona angani ya msalaba, Hivyo alipoenda vitani akaweka nembo ya msalaba katika mavazi yake ya kivita akiamini kuwa yale ni maono kutoka kwa Mungu, na aliposhinda ile vita akasema Mungu wa wakristo amemsaidia hivyo kuanzia huo wakati akataka kuifanya dini ya kikristo kuwa ya dini ya taifa, hivyo akaanza kufanya jitihada za kuunganisha pamoja warumi na wakristo hivyo akachukua desturi za dini za kipagani za Rumi(za kuabudu miungu mingi) na ukristo akavileta pamoja ili awapate wote. Kwa lugha nyepesi alichofanya Konstantini ni KUOANISHA ukristo na upagani..Na ndio maana tafsiri ya neno Pergamo ni NDOA.

Kwahiyo alichofanya mwaka 325WK ni kuitisha baraza kubwa la maaskofu, na viongozi wote wa Kikristo mahali panapoitwa NIKEA. Ambapo zaidi ya viongozi wa kidini 1,500 walihudhuria kuzungumzia suala hilo. Na ndipo wote wakafikia muafaka wa kuundwa Dini moja ya ulimwengu mzima (Kanisa Katoliki). Kumbuka tafsiri ya Neno Katoliki ni “ulimwengu wote” hivyo kanisa Katoliki maana yake ni “Kanisa la ulimwengu wote”.. Sasa kuanzia hapo ule ukristo ambao ulikuwa haujachanganyikana na mafundisho yoyote ya uongo, ukafa na kuzaliwa ukristo mpya bandia ambao umechukuliwa na desturi za kipagani za Rumi mfano wa kuabudu miungu mingi, na ndio hapo vitu kama ubatizo wa vichanga ukazaliwa, ubatizo wa kunyinyuziwa ukaundwa, ibada za sanamu,kusali rozari na za kuomba kwa watakatifu waliokufa zamani mambo ambayo huwezi kuyaona katika maandiko matakatifu au kufanywa na mitume wa zamani,pamoja na ibada za miungu mitatu, Ambazo utazikuta kwenye desturi za kirumi.

Sasa kumbuka huyu Konstantini ndio mfano wa Balaamu Bwana Yesu aliyemzungumzia kuwa anawakosesha watu wake (Kumbuka roho ile ile ya shetani iliyokuwa ndani ya Balaamu ndiyo hiyohiyo iliyokuwa ndani ya Konstantini). Kama vile Balaamu alivyotia ukwazo kwa wana wa Israeli wale vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu na kuzini vivyo hivyo Konstantini alianza kuwakosesha watu wa Mungu (wakristo) kwa kuwatoa katika mstari wa ukristo wa kweli wa mitume, na kuwaingiza katika dini ya kipagani aliyoianzisha yeye (Ukatoliki). Na kuwafanya wafanye uzinzi wa kiroho na kuamsha ghadhabu ya Mungu katikati yao.

Bwana Yesu aliendelea na kusema…

“15 Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile”

Kumbuka pia hawa wanikolai tuliwaona tokea Kanisa la kwanza la Efeso, isipokuwa kule walikuwa wanaonyesha matendo tu lakini hapa katika kanisa hili wamehama kutoka katika matendo na kuwa katika “Mafundisho” ikifunua kuwa ni kitu kilichotia mizizi sana, kimeundiwa kanuni na sheria za kufuatwa. Kumbuka tena tafsiri ya neno NIKOLAI ni “kuteka madhabahu”. Hivyo wanikolai ni watekaji madhabahu, watu wanaochukua nafasi ya madhabahuni ambayo ingepaswa iwe ya Roho Mtakatifu mwenyewe na kuifanya yao. Mfano vyeo vya upapa, ukadinali, upandre viongozi wakuu, n.k.kujengwa kwa madaraja yanayomtofautisha mkristo mmoja na mwingine mbele za Mungu. Kwamba ilikuwa huwezi kumfikia Mungu au kumwomba Mungu bila kupitia kwanza katika ngazi za juu yako.Ilikuwa ili kusamehewa dhambi ilimpasa mtu apitie kwa pandre wake amwombee, yeye mwenyewe hawezi kufanya hivyo. Hivyo uhusiano binafsi wa mtu na Mungu uliuliwa, ukaundwa uhusiano wa mtu na mtu kwa niaba ya Mungu..(Huo ndio unikolai), uongozi wa Karama za rohoni ukafa, ukanyanyuka uongozi wa kibinadamu kanisani… Na mafundisho haya yalipokomaa na kuhasiliwa na hiyo dini ya ulimwengu mzima (Kikatoliki) ndipo ukatokea UPAPA (ambao Unasimama kama mwakilishi wa Mwana wa Mungu duniani)..Hii ndiyo ngazi ya juu kabisa ya hii roho ya unikolai.

Lakini Bwana anamaliza na kusema…

” 16 Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.

17 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea. “

Unaona kama vile wana wa Israeli walivyouliwa kwa upanga siku ile watu elfu 24, kwa kosa tu la Balaamu.. Vivyo hivyo Bwana aliwaonya na hao wakristo wa hilo kanisa la Pergamo kwamba watubu na wajiupushe na mafundisho ya Konstantini yaliyofananishwa na Balaamu (yaani dini iliyoundwa ya kikatoliki), inayowapelekea kufanya uasherati wa kiroho, na ibada za sanamu. Lakini walikuwepo watu ambao hawakutubu kipindi hicho wakachukuliana na hiyo dini ya uongo ya Konstantini, Bwana aliwaua hao wote kwa upanga utokao katika kinywa chake, Hao wote walikufa kiroho, na kabla ya kuangamizwa nafsi zao Bwana aliwanyanyulia mjumbe kwanza na kuwahubiria mambo hayo na kuwarudisha katika njia ya kweli ya mitume kwa udhihirisho wa kipekee kutoka kwa Bwana, na mjumbe huyo ni MARTINI ndiye aliyekuwa (Malaika/Mjumbe) wa hilo kanisa.

Kwahiyo wale wote walioupokea ujumbe wake,na kujitenga na uasi huo Mungu aliwalinda mpaka mwisho kama tunavyosoma..’

“17 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea”.

Hivyo wote walioshinda, Bwana alizidi kuwaongozea ufunuo wa ziada wa kuzijua siri zake, na kumtambua shetani na hila zake (Ndiyo ile mana iliyofichwa). Kumbuka ni mana iliyofichwa ikimaanisha kuwa sio watu wote wataiona isipokuwa bibi-arusi tu aliyejitenga na mifumo yote ya yule kahaba mkuu (Katoliki). Huyo tu ndiye atakayepokea hicho chakula cha kipekee kitokacho mbinguni. Kadhalika alisema pia yeye ashindaye atapewa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea..Sasa thawabu hii watapewa katika ule ulimwengu unaokuja..

Ni mfano wa zawadi na ndio maana anasema juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea. Kuashiria kwamba siku atakapolipokea ndipo atakapojua thamani ya alichopewa na watu wengine wataiona baadaye.. Sasa kumbuka anaposema kupewa jina, haimanishi kubadilishiwa jina, au kupewa jina lenye mvuto mzuri hapana, tunaweza tukajifunza kwa maisha tu ya kawaida unaweza ukapita mahali fulani ukasikia mtu fulani ana jina mahali pale.. Haimaanishi kuwa jina lake ni zuri au ni la kipekee sana hapana moja kwa moja utajua huyo mtu anayo nguvu fulani labda ya kifedha au kimamlaka, au ki-sifa ndiyo iliyompa jina hilo..Na ndivyo itakavyokuwa huko katika utawala wa milele unaokuja.. Kuna watu watakuwa na majina mazito na makubwa kutokana na uaminifu wao waliokuwa nao hapa duniani, na kuna watu pia watakuwa na majina madogo. Biblia inatuambia hata Bwana mwenyewe atakuja na Jina jipya, siku hiyo ndiyo kila mtu atamfahamu kwa mapana yeye ni nani na biblia ilikuwa inamaanisha nini ilipokuwa inasema kuwa yeye ni BWANA WA MABWANA na MFALME WA WAFALME. HALELUYA!!.

Kwahiyo ndugu yangu hata sasa haya mafundisho ya Balaamu yapo ndani ya Kanisa na yapo katika kiwango cha juu sana kuliko hata kile cha kipindi kile, roho ya mafundisho ya kipagani imejichanganya katikati ya watu wa Mungu. Hivyo toka huko. Bwana leo hii anaachilia mana yake iliyositirika kwa wachache waliotayari kutii, lakini wakati utafikia tusipotubu na kuyaacha mafundisho ya uongo na kuyakimbia.. Bwana atakuja kufanya vita nasi kwa Neno lake kwa kupitia vivywa vya watumishi wake. Na ukishafikia hiyo hatua, kutakuwa hakuna nafasi ya pili, hapo ni kuingojea ile siku ya Bwana inayowaka kama moto na kutupwa katika lile ziwa la moto. Hivyo huu ni wakati wa kutengeneza mambo yako sawa ili hayo yote yasikupate kabla ya mlango wa neema kufungwa.

Ubarikiwe.

1.Ufunuo: Mlango wa 2 Part 4

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.

Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Kifaru Malale
Kifaru Malale
2 years ago

Tupo pamoja mtumishi, naelewa sana somo hili Kwa lugha rahis