UFUNUO: Mlango wa 14

UFUNUO: Mlango wa 14

Kama tunavyofahamu baada ya wakati wa mataifa kuisha yaani unyakuo kupita itakuwa imebaki miaka 7 tu mpaka dunia kuisha, ndani ya hicho kipindi kifupi Mungu atakuwa anashughulika na Taifa la Israeli, na kuwatia muhuri wale wayahudi 144,000 kama tunavyosoma katika sura ya 7 ya kitabu cha Ufunuo, kwahiyo ile miaka mitatu na nusu ya kwanza itakuwa ni injili kwa wayahudi na ile miaka mitatu na nusu ya mwisho itakuwa ni wakati wa ile DHIKI KUU.

Tukiendelea na ufunuo sura ya 14 ambayo ni mwendelezo wa habari ya wale wayahudi 144000 waliotiwa muhuri na Mungu, kama haujapitia sura ya 7, unaweza ukaanzana nayo kwa kufuata link hii kisha ndio tuendelee na sura hii ya 14 >>> Ufunuo: Mlango wa 7

Ufunuo 14:1-5″ Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao.

2 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao;

3 na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne elfu, walionunuliwa katika nchi.

4 Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.

5 Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.

Hapa tunaona wale wayahudi 144000 wakionekana wakiwa na mwanakondoo juu ya mlima Sayuni ikifunua nafasi za hawa wateule wa Mungu mbele za YESU KRISTO,katika utawala unaokuja wa miaka 1000, watakapomiliki na kutawala na YESU katika mlima Sayuni (yaani Yerusalemu), pia hawa wanaonekana ni bikira ikiwa na maana kwamba hawajajitia unajisi wowote na mafundisho ya dini za uongo,

Na pia kama tunavyoona walijifunza wimbo mpya ambao ni wao tu waliouweza kuuimba, sasa huu wimbo unamaana kuwa ni “furaha ya Roho Mtakatifu”, kama vile sisi wakristo tunapompokea Kristo na Bwana anapotuokoa na kutupa pumziko pale tunapomfurahia na kumshukuru wimbo mpya wa Mungu unazalika ndani ya mioyo yetu ambao hakuna mwingine anayeweza kuuimba isipokuwa mwenye Roho wa Mungu kama sisi

..Daudi alisema katika Zaburi 40:1 “Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.

2 Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu.

3 AKATIA WIMBO MPYA KINYWANI MWANGU, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana “.

Kwahiyo hawa 144000 baada ya kutiwa muhuri wa Mungu kwa kupokea Roho Mtakatifu na kupata ufunuo kwamba mwokozi wao anaishi na ndiye atakayekuja kuwapigania wimbo mpya utazaliwa ndani ya mioyo yao ambao hakuna mwingine yoyote atakayeweza kujifunza isipokuwa wao,

Na pia kumbuka watu hawa hawakuwa mbinguni, bali ni hapa hapa duniani, ukisoma kwa makini utaona sio wale 144000 ndio waliokuwa mbinguni mbele ya kiti cha enzi wakiimba hapana bali ni sauti ilisikiwa mbinguni wakiimba na hawa si wengine zaidi ya malaika, na ndio wale 144000 walionekena wakijifunza wimbo ule. Hivyo hawa 144000 hawakunyakuliwa mbinguni, bali watakuwa hapa hapa duniani.

INJILI YA MILELE:

Tukiendelea..

Ufunuo 14:6-13″ 6 Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa,

7 akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.

8 Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.

9 Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake,

10 yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo.

11 Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake.

12 Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.

Katika mistari hii tunaona baada ya wale 144,000 kutiwa muhuri, na Bwana akiwaweka mbali na yule mnyama watafunguliwa pia na mlango wa kuhubiri INJILI YA MILELE. Na ndio wale malaika watatu tunaona wakiruka katikati ya mbingu wakihubiri injili ya milele juu yao wakaao juu ya nchi, kumbuka Mungu hajawahi kutumia malaika kuhubiri injili duniani, siku zote huwa anawatumia wanadamu, biblia inasema malaika ni roho zitumikazo kuwahudumia watakatifu(waebrania 1:14). Hivyo watakaozihubiri hizi jumbe za wa hawa malaika warukao ni wale wayahudi 144000.

Kumbuka Injili tuliyonayo sasa ni Matendo 2:38 “…Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu “. Injili hii ni ya kuwafanya watu kuwa wakristo lakini INJILI YA MILELE ni kwa watu wote na inayojulikana na watu wote, kwamfano inajulikana kuwa ushoga ni kosa,usagaji, kuua ni kosa, kuzini, kutukana,ufiraji, kuzini na wanyama,kufanya maasi ni kosa, dhamiri ya mtu ikimshuhudia kabisa kuwa anachokifanya sio sahihi bila hata kuhubiriwa n.k. ni injili ambayo kwa ufupi hahiitaji biblia kuijua, inajulikana na watu wote wenye dini na wasio na dini. Hiyo ni hofu ya Mungu ambayo ipo kwa kila mwanadamu.

Kwahiyo INJILI hii ya MILELE itahubiriwa tena kwa mara ya mwisho kwa wanadamu wote waliopo ulimwenguni wanaotenda maasi ili mtu asiwe na udhuru wa kusema sijasikia, kwa maana kwa wakati huo maasi yatakuwa ni mengi sana duniani kama tunavyoyaona leo…

Warumi 1:18 “Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.

19 Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana YAMEKUWA DHAHIRI NDANI YAO , kwa maana Mungu aliwadhihirishia.

20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, UWEZA WAKE WA MILELE NA UUNGU WAKE; hata wasiwe na udhuru; ……..

32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao. “

Hivyo injili hii ya MILELE itagusa makundi yote hata wasiokuwa na dini, kwasababu ni mambo yaliyodhahiri ambayo yanajulikana na kila mtu.

Malaika wa pili akafuAata akisema “8 Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.”

Hawa watu 144000 baada ya kupokea ufunuo wa Mungu kuwa anayetawala dunia nzima na dini zote ni mpinga-kristo (PAPA) na jinsi kanisa Katoliki lilivyohusika kuwaua watakatifu wengi na litakapokwenda kuishia, kwamba Mungu ameshalihukumu hivyo watahubiri ujumbe wao katika dunia nzima, hukumu ya Babeli mkuu.

Tukiendelea mstari wa 9-11 tunasoma..

“9 Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake,

10 yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo.”

Sasa hili ni onyo la mwisho litakalohubiriwa kwa watu wote, kwamba mtu yoyote atakayemsujudia yule mnyama na sanamu yake (yaani Kushirikiana na Kanisa Katoliki na mafundisho yake au kuwa mshirika wa umoja wa madhehebu) au kuipokea chapa katika mkono wake au katika kipaji cha uso wake, atashiriki mapigo yote ya Mungu yanatakayofuata huko mbeleni.

Kumbuka hapo kanisa litakuwa limeshaondoka, watanyakuliwa watu wachache sana wakati huo ulimwengu hautajua chochote, dhiki zote zitawakuta wale waliobaki duniani, je umeokolewa?. kama biblia inavyoendelea kusema.. “13 Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao. “

SHINIKIZO LA GHADHABU YA MUNGU:

14 Kisha nikaona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali.

15 Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa.

16 Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa.

17 Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali.

18 Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana.

19 Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu.

20 Shinikizo lile likakanyagwa nje ya mji, damu ikatoka katika shinikizo mpaka kwenye hatamu za farasi, kama mwendo wa maili mia mbili. “

Mistari wa 14-20 unaelezea maandalizi juu ya ile vita ya Harmagedoni, vitakavyopigwa Israeli, Hapa tunaona malaika akiwa ameshika mundu mkali na kuvuna mzabibu wa nchi kuashiria maovu ya wanadamu yamefikia kilele, kikombe cha ghadhabu ya Mungu kimejaa wakati wa rehema hakuna tena, kinachofuata ni hasira ya Mungu kumwagwa juu ya nchi, na ndio maana unaona zile zabibu zikatupwa katika lile shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu na damu ikatoka pale mpaka kwenye hatamu za farasi kwa mwendo wa maili 200, kumbuka farasi anawakilisha vifaa vya kijeshi, hii ni picha halisi inayoonyesha jinsi hiyo vita itakavyokuwa ya kumwagika damu nyingi hayo yatatimia katika kumiminwa kile kitasa cha sita kati ya vile saba vya ghadhabu ya Mungu..

Ufunuo 16:12-16″

12 Na huyo wa sita akakimimina kitasa chake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua.

13 Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.

14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.

15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)

16 Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni.

Pia Ufunuo 19:11-16 Inasema…”11 Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.

12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.

13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.

14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.

15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, NAYE ANAKANYAGA SHINIKIZO LA MVINYO LA GHADHABU YA HASIRA YA MUNGU MWENYEZI .

16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA.”

Hii itakuwa ni vita ya mwisho mabilioni ya watu watakufa, na baada ya kumiminwa kile kitasa cha mwisho cha saba mwisho wa dunia utakuwa umefika. 

Hivyo ndugu kumbuka shetani hapendi ukifahamu kitabu cha UFUNUO kwasababu anajua siku ukiyajua mambo ya kutisha yanayokuja huko mbeleni utatubu na kuishi maisha ya uangalifu hapa duniani, yeye anachotaka ujue ni kuwa dunia itadumu milele na ni raha tu siku zote lakini biblia usisahau inasema 1wathesalonike 5:3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.”

Huu ni wakati wa jioni sana BWANA YESU yupo mlangoni kurudi kulinyakua kanisa lake je! na wewe utakuwa miongoni mwa wale watakaokwenda naye? Ni mara ngapi umesikia injili ubadilike lakini bado unaabudu sanamu, unapenda mambo ya ulimwengu huu zaidi ya Mungu , unavaa vimini, unapaka lipstick, unazini, mlevi, msengenyaji, mtukanaji,? Injili hiyo halitadumu milele, upo wakati mlango wa neema utafungwa hapo ndipo Bwana Yesu anasema kutakuwa na kilio na kusaga meno.

Mpe Bwana maisha yako leo uokolewe.

Mungu akubariki.

Kwa Mwendelezo >> UFUNUO: Mlango wa 15

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada zinazoendana..


INJILI YA MILELE.

ALAMA KATIKA VIPAJI VYA NYUSO.

JE! KUBET NI DHAMBI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments