Kula uzao wa tumbo lako maana yake nini? (Kumbukumbu 28:53)

Kula uzao wa tumbo lako maana yake nini? (Kumbukumbu 28:53)

Swali: Katika Kumbukumbu 28:53, tunaona Mungu anasema watu watakula nyama za wana wao, na uzao wa tumbo lao, je alikuwa anamaanisha nini kusema hivyo?.

Jibu: Tusome,

Kumbukumbu 28:53 “Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa BWANA, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako”.

Ukisoma kuanzia juu mstari wa kwanza wa sura hiyo ya 28, utaona baraka ambazo Mungu aliwaahidia wana wa Israeli endapo wataenda katika sheria zake na amri zake..kwamba watabarikiwa mjini na vijijini, hali kadhalika watabarikiwa waingiapo na watokapo..na zaidi sana uzao wa matumbo yao utabarikiwa.

Kumbukumbu 28:1 “Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;

2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.

3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.

4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako”.

Lakini ukizidi kusogea mbele katika mstari wa 15, Utaona Mungu anatoa tahadhari na ole kwa hao hao Israeli kama endapo watamwacha na kwenda kuabudu miungu mingine, na kuzivunja amri zake, basi watakumbana na laana nzito.

Na mojawapo ya laana hizo waliambiwa kuwa watakula nyama za watoto wao kutokana na njaa Bwana atakayowapiga nayo.

Kumbukumbu 28:15 “Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.

16 Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani………….

49 BWANA atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake;

50 taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana;

51 naye atakula uzao wa ng’ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng’ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza.

52 Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa BWANA, Mungu wako.

53 NAWE UTAKULA UZAO WA TUMBO LAKO MWENYEWE, NYAMA YA WANA WAKO NA BINTI ZAKO aliokupa BWANA, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako”.

Sasa unaweza kuuliza jambo hilo lilitimia lini?..kwamba wana wa Israeli walifikia hatua ya kula nyama za watoto wao.

Kama wewe ni msomaji wa biblia, utakumbuka kuna wakati Israeli ilimwacha Mungu, na matokeo ya kumwacha Mungu..Bwana akaruhusu jeshi la Shamu liwazunguke…na kwa hofu ya jeshi hilo kubwa, wana wa Israeli walijifungia ndani ya mji..(kumbuka miji ya zamani ilikuwa inazungushiwa ukuta pande zote). Hivyo mlango wa mji ukifungwa hakuna mtu anayeweza kuingia wala kutoka.

Kwahiyo Israeli walijifungia mjini kwa kipindi kirefu kwa hofu ya jeshi la washami lililopo nje.

Na matokeo ya kujifungia ndani kwa muda mrefu ni chakula kuisha ndani, na kuanza kufikiria kula mavi ya njiwa na kula wanyama wasiolika, ilifikia hatua kichwa cha punda kinaauzwa kwa fedha nyingi sana.

Na njaa ilipozidi watu wakaanza kula watoto wao, mpaka taarifa zikamfikia mfalme za wanawake wawili waliokuwa wanagombania kula nyama za watoto wao.

Tusome,

2 Wafalme 6:24 “Ikawa baada ya hayo, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru Samaria.

25 Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha.

26 Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme.

27 Akasema, BWANA asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni?

28 Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, MTOE MTOTO WAKO, TUMLE LEO, NA MTOTO WANGU TUTAMLA KESHO.

29 Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake.

30 Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake”.

Umeona?..Mungu kamwe hasemi uongo!..alisema siku watakayomwacha watakula watoto wao, na kweli ikatokea hivyo hivyo kama alivyosema siku walipomwacha na kuzivunja amri zake…walikula nyama za watoto wao waliowazaa wenyewe. (Unaweza kusoma pia Yeremia 19:9, Maombolezo 4:10, na Ezekieli 5:10).. utaona jambo hilo hilo.

Hiyo inatufundisha nini?

Inatufundisha kuwa maneno ya Mungu kamwe hayapiti..aliposema watu watakula nyama za watoto wao ni kweli ilitokea…hali kadhalika anaposema kuwa wazinzi na waasherati na waabudu sanamu hawataurithi uzima wa milele kwasababu wamemkataa yeye…basi neno hilo litatimia kama lilivyo na wala hasemi uongo..

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.

Na sio tu hasara ya kuukosa ufalme wa mbinguni, bali hata maisha ya mtu aliyemkataa Mungu akiwa hapa duniani, yatakuwa ni ya tabu tu siku zote, hatakuwa na furaha wala amani, hatafanikiwa wala kuwa na tumaini, na atakufa na kumbukumbu lake litasahauliwa.

Je umempokea Yesu?.

Kama bado ni nini unachosubiri? Kumbuka unyakuo wa kanisa upo karibu wakati wowote parapanda ya mwisho inalia na watakatifu watanyakuliwa, wewe ambaye hujaokoka.lwo hii utakuwa wapi siku hiyo??..au wewe uliye vuguvugu leo, siku ile utakuwa mgeni wa nani?.

Bwana akubariki.

Maran atha!.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

WEKA KUMBUKUMBU YA MAMBO BWANA ANAYOKUFANYIA KWASABABU YATAKUFAA MBELENI.

USIRUDI NYUMA KWA KUITUMAINIA HAKI YAKO.

EE MUNGU, MUNGU WANGU, NITAKUTAFUTA MAPEMA:

Je! Mtume Paulo alikuwa ni Mrumi, Myahudi au raia wa Tarso?

Zile Rangi saba za Upinde wa Mvua zinawakilisha nini?

Kisiwa cha Patmo kipo nchi gani?.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mercy
Mercy
2 years ago

Asante ..ubarikiwe