Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia, maneno ya Mungu wetu aliye juu..kwasababu maneno yake ndio Mwanga wa njia yetu ya kuelekea mbinguni, na Taa iongozayo miguu yetu.(Zab.119:105)
Je umewahi kujiuliza kwanini bendera nyingi zinakuwa ni kitambaa chenye rangi mbali mbali, na kila rangi inakuwa na maana fulani?. Utaona mataifa mengi bendera zao zinakuwa ni mistari tu ya rangi tatu au nne au tano. Na kama ukifuatilia utagundua zile rangi si urembo, bali zimebeba maana fulani kwa hilo Taifa.
Kwamfano bendera ya Taifa la Tanzania ina rangi 4, Nyeusi, Njano, kijani na Bluu. Rangi nyeusi inawakilisha wenyeji wa Taifa hilo (ni watu wenye ngozi nyeusi), rangi ya njano inawakilisha maliasili zote zilizopo ndani ya Taifa hilo, rangi ya kijani inawakilisha mimea na uoto wa asili wote pamoja na mazao ya nchi.. na rangi ya bluu inawakilisha Maji yote ikiwemo bahari, mito na maziwa. Hivyo kama ukiweza kuzisoma rangi hizo tayari utakuwa umeshalielewa Taifa la Tanzania, ni taifa la namna gani hata kabla ya kufika.
Kadhalika na Bwana Mungu wetu anayo bendera yake ambayo inawakilisha tabia zake. Na bendera yake hiyo aliiwasilisha kwetu baada tu ya ile gharika ya wakati wa Nuhu. Na hiyo si nyingine zaidi ya Ule Upinde wa Mvua wenye rangi saba. Kikawaida Bendera zetu zinakuwa ni kitambaa tu kilichochorwa mistari ya rangi, na tunaipandisha inakuwa inapepea angani, lakini bendera ya Bwana haijachorwa katika kitambaa bali katika anga juu sana, na imechorwa kwa mistari ya rangi saba.
Bendera hiyo Ndiyo inayomwelezea Mungu ni nani kwetu..
Sasa kabla ya kuendelea mbele ni vizuri tukazijua tabia kuu mbili za Mungu, ambazo hizo ndio msingi wa somo letu.. Biblia inasema Mungu ni MWINGI WA HASIRA (Nahumu 1:2) na vile vile biblia inasema Mungu ni MWINGI WA HURUMA.(Kutoka 34:6, Zaburi 145:8, Yoeli 2:13, Yona 4:2). Hizo ndio tabia kuu mbili za Mungu wetu. Ana hasira nyingi sana, vile vile ana huruma nyingi sana. Lakini pamoja na kwamba ni mwingi wa hasira, biblia imesema si mwepesi wa hasira, maana yake si rahisi akasirike kwa haraka.
Hivyo tukirudi katika mifano ya maisha ya kawaida..Mtu anavyozidi kuwa na hasira ndivyo ndani mwake kunavyozidi kuwaka, maana yake ni kwamba ni kama kuna moto unachochowa ndani yake na anazidi kuwa mwekundu, ikiwemo unyama huko huko.. Ndio maana watu weupe wakikasirika ni rahisi kuona hata ngozi za nyuso zao zimebadilika na kuwa nyekundu.. Hivyo rangi nyekundu inawakilisha hasira au ghadhabu..
Lakini vile vile, mtu huyo huyo hasira yake inapoanza kupoa utaona ule wekundu unaondoka na anarudia rangi yake. Ule wekundu unaanza kufifia kidogo kidogo mpaka, unaisha kabisa…
Vile vile Katika mifano mingine ya maisha ya kawaida pia kitu cha moto sana kinawakilishwa na rangi nyekundu, lakini kitu cha baridi kinawakilishwa na rangi ya bluu.. maana yake rangi ya bluu ni rangi ya utulivu uliozidi sana, ni rangi ya upole, ni rangi ya kulipooza jambo la moto!, ni rangi ya kutuliza ghadhabu kwa ufupi ni rangi ya rehema…na ni kinyume kabisa cha rangi ya Nyekundu.
Kwa mifano hiyo tutakuwa tumeshaanza kuelewa kwanini uwepo upinde angani unaoanza na Rangi nyekundu, na kisha zifuate rangi nyingine mpaka itokee rangi ya mwisho ya bluu..Utaona kwa jinsi zile rangi zinavyozidi kusogea mbele ile nyekundu inafifia na kuwa rangi ya chungwa (Orange), na kisha njano na kisha kijani… Maana yake hapo, Hasira ya Mungu inapungua kutoka juu kushuka chini, mpaka kufikia kusamehe kabisa..na kutoa neema (Ndio rangi ya kijani iliyopo katikati)..
Na inavyozidi kuendelea utaona Neema ya Mungu inazidi kuwa nyingi na hata kuelekea kwenye rangi ile ya blue ambayo inawakilisha utulivu wa Mungu wa hali ya juu, na Neema isiyo na kikomo..kiasi kwamba Rehema zake ni nyingi mno na hata kuipooza na kuizima ghadhabu yote..Hivyo rangi ya inavyozidi kukolea kuwa bluu ndivyo ndivyo neema zake zinavyozidi kuwa nyingi….Ndio maana hata anga lina rangi ya bluu, kuonyesha wingi wa huruma zake kuliko hasira zake.
Hivyo zile rangi saba zinawakilisha ghadhabu ya Mungu jinsi inavyosogea na kubadilika kuwa Rehema zake…Ndio maana Baada ya Nuhu kutoka kwenye gharika, Mungu aliirehemu dunia ambayo alikuwa ameighadhibikia kwa ghadhabu kubwa, na kuahidi kutoiangamiza tena kwa maji. Hapo ni hasira zake zimesogea kutoka kwenye nyekundu kwenda kwenye blue.
Ni Mungu tu pekee ndio ana tabia hiyo, hakuna kiumbe kingine duniani, au mbinguni ambacho kina wingi wa hasira na hapo hapo kina wingi wa huruma.
Ndio maana alisema katika..
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; 30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”
Haijalishi Umemwudhi Bwana kiasi gani leo, kumbuka huruma ni nyingi, yupo tayari kukusamehe kabisa endapo utamgeukia yeye kwa moyo wako wote na kudhamiria kuacha dhambi. Unachopaswa kufanya ni kutubu mbele zake kwa moyo wa unyenyekevu kabisa na kisha kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu, na kupokea Roho Mtakatifu. Naye atafuta dhambi zako zote, na kukufanya kuwa mtakatifu kana kwamba hujawahi kumkosea kabisa katika maisha yako. Na wala ghadhabu yake haitakuwa juu yako hata kidogo.
Lakini ukipuuzia rehema zake hizo ambazo zinapatikana bure, na kuzidi kuisogelea ghadhabu yake, fahamu kuwa yeye bado hajabadilika, bado ni mwingi wa hasira… alisema…katika Nahumu 1: 2 “Bwana ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; Bwana hujilipiza kisasi, NAYE NI MWINGI WA HASIRA; Bwana hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira”
Ni jambo baya sana kuangukia kwenye hasira ya Mungu, ni heri ukatubu leo na kumwamini..
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali. Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
MUNGU HAONI SHIDA KUMUHAKIKISHIA MWOVU ULINZI.
Fadhili ni nini? Nini maana ya “fadhili zake ni za milele” kibiblia?
Je, kama hauna ubatizo sahihi hauwezi kuwa na Roho Mtakatifu?
TAFUTA KUWA NA AMANI NA WATU WOTE.
NIKUPE WEWE URITHI WA BABA ZANGU?
Rudi nyumbani
Print this post