NIKUPE WEWE URITHI WA BABA ZANGU?

NIKUPE WEWE URITHI WA BABA ZANGU?

1Wafalme 21:1 “Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria.

2 Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake.

3 Nabothi akamwambia Ahabu, BWANA APISHE MBALI NIKUPE WEWE URITHI WA BABA ZANGU.

4 Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula”.

Katika agano la kale ilikuwa ni sheria hakuna mtu yeyote kuuza shamba la familia au ukoo, vitu vingine vyote viliweza kuuzwa lakini linapokuja suala la shamba la urithi ni utaratibu uliokuwepo hakuna mtu yeyote kuuza shamba hilo haijalishi kafilisika au halitumii, hata sasa kwenye jamii zetu nyingi mambo kama hayo tunayaona, mtu ukiuza shamba la ukoo, anaweza akatengwa kama sio kufukuzwa kabisa na ndivyo ilivyokuwa hata katika desturi za wayahudi..

Hapa tunaona mtu mmoja wa kawaida tu aliyeitwa Nabothi alikuwa na shamba lake lililokuwa karibu sana na hekalu la Raisi wake, Ahabu..Hiyo inatupa picha kamili kuwa shamba hilo lilikuwa ni lenye thamani nyingi sana, kama angekuwa ni mtu mwenye tamaa basi angeliuza kwa gharama kubwa sana, kiasi kwamba angepata pesa ya kununua mashamba mengine kama yale hata zaidi ya 10 mahali pengine na bado angebakiwa na pesa na kujenga na kula katika maisha yake yote na familia yake…

Shamba hilo ni wazi kuwa lilikuwa zuri sana, kiasi cha kwamba lilimfanya hata mfalme Ahabu akose usingizi kwa kunyimwa kuuziwa shamba lile na mmiliki mwenyewe Nabothi, Sio kwamba Nabothi alipenda kumdharau mfalme, au hakuwa na shida na mali hapana, lakini alijua kuwa shamba la urithi haliuuzwi, haijalishi ni nani amesimama mbele yake, ni mkuu,au sio mkuu, ni tajiri au sio tajiri, kanuni ni ile ile shamba la urithi haliuzwi… Nabothi alikuwa tayari kufa lakini sio kuachia shamba lile liende nje ya ukoo wake. Ukiendelea kusoma pale utaona mpaka Yezebeli anamuundia visa auawe ili alichukue shamba lile.

Biblia inatuambia mambo hayo yaliandikwa kwa mifano ili kutufundisha sisi, ambao sisi tutakuja kuishi katika agano lililo bora zaidi (1Wakorintho 10:11).. Na sisi pia tunao urithi tulioachiwa na mababa zetu wa Imani (Mitume), na urithi huo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO,

1Petro 1:3 “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;

4 TUPATE NA URITHI USIOHARIBIKA, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.

5 Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho”.

Unaona mtu yeyote aliyempokea Kristo moja kwa moja tayari, ameupokea Urithi usioharibika ambao ulianza tangu enzi na enzi za mitume Baba zetu ambao hao walikuwa watangulizi wetu waliokuwa tayari hata kufa lakini wasiuuze urithi waliopewa na Mungu mbinguni yaani Kristo maishani mwao, na walipoondoka wakaturithisha na sisi urithi huo huo ambao ni YESU KRISTO Bwana wetu, ili na sisi pia wakati ukifika tuwarithishe Watoto wetu, sasa cha kushangaza leo hii utaona watu wengi wanasema wao ni wakristo, wameokoka, lakini wapo tayari kuuza urithi huu kirahisi rahisi tu, mtu yupo tayari kumwacha Kristo kwa ajili ya mali, yupo tayari kumwacha Kristo kwa ajili ya wazazi, au ndugu, yupo tayari kumwacha Kristo kwa ajili ya mwanamke au mwanaume…Yupo tayari kurudi nyuma ki-wokovu kwa ajili ya rafiki zake, kwa ajili ya wafanyakazi wenzake, kwa ajili ya boss wake, kwaajili ya ujana wake, kwaajili ya umaarufu wake…Kirahisi rahisi tu, jambo lolote likijitokeza ambalo anaona kabisa ni kinyume na imani yake yupo tayari kuacha mara moja, akidhani kuwa Imani hiyo akishaichia ipo siku ataipata tena,,Ndugu yangu usidanganyike biblia inatumbia IMANI hii tuliyonayo tunakabidhiwa mara moja tu, hakuna cha mara mbili wala mara tatu..soma…

Yuda 1:3 “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu”.

Na hiyo ndio inatufanya tuwe makini sana kuilinda kwasababu tukishaipoteza kuipata tena ni ngumu..

Ni sawa na mtu anayeliuza shamba, akishaliuza mara moja, basi hatakaa alipate tena milele, linakuwa ni milki halali ya mtu mwingine..Vivyo hivyo na leo hii wewe unayeuuza wokovu wako kirahisi rahisi tu, unarudi nyuma kirahisi rahisi tu, siku Roho Mtakatifu akiondoka kwako basi ndio moja kwa moja hivyo , hakuna toba hapo.. Umesikia injili mara ngapi lakini bado wiki hii unaompango wa kwenda kuzini, unamfanyia jeuri Roho wa Mungu, unadhani kuna siku itafika utubu…tambua hakuna jambo kama hilo saa ya wokovu ni sasa, jitwike msalaba wako mfuate YESU.

Marko 8:35 “Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.

36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?

37 Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?

38 Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”.

Ifikie wakati uwe na ujasiri wa kumwambia ibilisi ki-vitendo “Nikupe wewe urithi wa Baba zangu?”..weka mbali mambo ya ulimwengu huu uanze kuulinda urithi wako.

Bwana akubariki sana.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

USIONDOE ALAMA YA MPAKA ILIYOWEKWA NA MABABA.

KAMA MWIZI USIKU WA MANANE:

CHUKIZO LA UHARIBIFU.

EDENI YA SHETANI:

CHUKIZO LA UHARIBIFU

YEZEBELI ALIKUWA NANI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments