USIRUDI NYUMA KWA KUITUMAINIA HAKI YAKO.

USIRUDI NYUMA KWA KUITUMAINIA HAKI YAKO.

Adui yetu shetani, ni kama simba angurumaye akitafuta mtu wa kummeza (1Petro 5:8), hivyo usiku na mchana anatupigana vita ili mradi, atuangushe au atwae vile tulivyo navyo.

Leo tutaingalia njia moja anayoitumia kutunyang’anya baraka zetu.

Shetani akishajua kuna Baraka Fulani umeahidiwa na Mungu, moja kwa moja anaanza kutafuta njia ya kukupokonya hiyo, sasa tofauti na wengi wanavyodhania kuwa adui yetu shetani anatunyang’anya baraka zetu kwa kutuloga, au kututumia wachawi!.. La! Hakuna uchawi wowote unaweza kubatilisha Baraka za Mungu alizotuahidia kwa kinywa chake.

Wengi wanapoteza nguvu nyingi na muda mwingi kushughulika na wachawi na washirikina wakidhani wao ndio wanaozuia Baraka Mungu alizowaahidia juu ya maisha yao kumbe sio!. Shetani anajua kabisa hawezi kamwe kutupokonya kile Mungu alichotuahidia, hizo nguvu hana!. Mungu akisema nitakupa hiki au kile, shetani hawezi kubatilisha hilo jambo..hivyo hatumii uchawi, wala uganga!.. Anachotumia ni kutafuta tu njia ya kumkosesha mtu na Mungu wake ili Mungu aibatilishe ile ahadi aliyomuahidia… Huo ndio uchawi mkubwa wa shetani, wala si mwingine!.

Kwamfano umekwenda katika njia za haki, umekuwa mnyenyekevu mbele za Mungu, umemtumikia na Mungu akapendezwa na wewe sana, hata akakupa ahadi kama alivyompa Ibrahimu, pengine  labda ya kuishi miaka mingi, au hata ya kupata mtoto au jambo lingine lolote zuri..na pengine akakuonyesha kabisa hata katika maono, au hata akamtuma malaika wake kukupa huo ujumbe.

Anachofanya shetani baada ya kujua kuwa umepewa ahadi kabambe kama hiyo, si kukutumia wachawi wakuloge au wachukue nyota yako.. la! Hawezi kufanya hivyo kwasababu anajua atakuwa anapoteza muda..atakachokifanya ni kuhakikisha wewe unaitumainia ile haki yako ya kwanza, na kuanza kukufanya upoe kuendelea kutenda haki.. ili Mungu achukizwe na wewe, na aiondoe ile ahadi aliyokuahidia…

Utauliza je! Mungu huwa anabatilishaga ahadi zake? Jibu ni ndio!.. Endapo mtu akiacha njia yake ya haki na kurudia uchafu, Mungu huwa anazighairi zile ahadi zote alizomwahidia mtu, haijalishi alimtuma malaika wake kumpelekea ujumbe, au alimtokea yeye mwenyewe, lakini mwisho ataibatilisha tu… Utauliza ni wapi katika maandiko tunasoma hilo…

Ezekieli 33:13 “Nimwambiapo mwenye haki, ya kwamba hakika ataishi; KAMA AKIITUMAINIA HAKI YAKE, AKATENDA UOVU, basi katika matendo yake ya haki, hata mojawapo halitakumbukwa; bali katika uovu wake alioutenda, atakufa katika uovu huo”.

Bwana akikupa ahadi ya kuishi miaka mingi, ukikengeuka na kuacha haki yako, utakufa kabla ya kutimiza miaka yako, japokuwa alishakuonyesha kuwa utaishi miaka mingi.

Dada, unayemcha Mungu sasa, Bwana akikuonyesha kuwa umebeba mtoto siku za mbeleni, au atakutumia kwa viwango vikubwa mbeleni na wewe ukakengeuka, na kuanza kufanya uasherati, ukaanza kuvaa kama wanawake wa kidunia wanavyovaa, ukaanza kuwa msengenyaji n.k, hiyo ahadi utaisahau.. Utabaki kujiuliza kama kweli ni Mungu alizungumza na wewe siku ile au la!.. Utatanga tanga huku na kule.. Na jambo hilo halitatimia kwako, na mwisho utakata tamaa na kusema Mungu ni mwongo!. Si mwongo, tayari shetani kashaitwaa Baraka yako siku nyingi sana, na wala hajaitwaa kwa uchawi!.. Ameitwaa kwa kukufarakanisha wewe na Mungu wako.

Kumbuka siku zote kuwa, Bwana akikupa ahadi ya jambo Fulani haimaanishi kuwa hilo jambo ndio tayari umeshalipata!. (Hilo usilitoe katika akili yako)

Inawezekana na wewe leo hii shetani kashakunyang’anya taji yako, au ahadi yako nzuri ambayo Mungu alishakupa…shetani ameshakurudisha kwenye ulimwengu, ndio maana huoni tena dalili ya ile ahadi  Mungu aliyokupa kutimia, alikuonyesha maono ya kwamba utakuja kumtumikia, na tena kwa viwango vikubwa.. lakini mpaka sasa huoni chochote unajiuliza ni Mungu kweli alikuonyesha yale maono au ni kitu gani!..

Ndio ni Mungu mwenyewe ndiye aliyekuonyesha, na wala hakukudanganya, isipokuwa ni  wewe ndio umemruhusu shetani kuitwaa taji yako…. Ulisahau kuwa ahadi za Mungu zinatimia juu yetu, endapo tu tukidumu katika mapenzi yake, tunapotoka katika mapenzi yake hakuna ahadi yoyote ya Mungu itakayotimia juu yetu.

 Lakini habari nzuri ni kwamba tumaini bado lipo, hata kama shetani kakuibia Baraka yako, upo uwezekano wa wewe kuirudisha tena, na zile Baraka zote zilizofutwa juu yako zikakurudia…

Ezekieli 33:15 “kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang’anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa.

16 Katika dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake; ametenda yaliyo halali na haki; hakika ataishi.”

Unachopaswa kufanya sasa, ni kutubu!..na kumrudia Bwana kwa moyo wako wote!.. sio umrudie kwasababu tu unataka Baraka!. Bali urudi kwasababu kweli umejua wewe ni mkosaji, njia zako ni mbovu, kama ulikuwa unaiba unaacha wizi, na unarudisha vile ulivyoiba kama bado vipo katika uwezo wa mikono yako, kama ulikuwa ni mzinzi unaacha uzinzi, kama ulikuwa ni mlevi unaacha ulevi kwa vitendo, kama ulikuwa unavaa vibaya, (Ni mwanamke lakini unavaa suruali, vimini, wigi, hereni, unapaka lipstick n.k) yote hayo unaacha, mwanaume kama ulikuwa unanyoa mitindo ya kidunia, na ulikuwa unavaa nguo za kidunia unaacha..na mambo mengine yote yasiyofaa.. Na baada ya kuacha yote hayo, na kutubu hatua inayofuata ni ubatizo, kumbuka ubatizo ndio unaokamilisha wokovu kwa mtu (Marko 16:16). Na ubatizo sahihi ni wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo.

Na baada ya hapo Roho Mtakatifu aliyeingia ndani yako, atakuongoza na kukutia katika kweli yote. Na yeye mwenyewe atazirejeza zile Baraka zote na ahadi zote zilizokuwa zimefutwa juu yako. Utaziona zinatimia mbele ya macho yako.

Hiyo ndiyo njia rahisi ya kurejesha Baraka zako na Ahadi zako, wala huhitaji kuombewa na mtu.. Na wewe tu kurejesha mahusiano yako na Mungu, ambayo yalikuwa yamevurugwa..na Baraka zako zote utaziona..

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Ni vitu vipi hivyo viwili visivyoweza kubadilika? (Ebr 6:18)

UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?

Kama tunaokolewa kwa neema kwanini wokovu tuupate kwa nguvu?

Ni vitu vipi hivyo viwili visivyoweza kubadilika? (Ebr 6:18)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments