NDUGU,TUOMBEENI.

NDUGU,TUOMBEENI.

Ukiangalia ujenzi wa kwanza wa hekalu na ule wa pili utaona kuna utofauti fulani, Kwanza ule wa kwanza uliojengwa na mfalme Sulemani, ulikuwa ni wa utajiri mwingi, ambao ulikuwa tayari umeshakusanywa na Daudi baba yake Sulemani huko nyuma, pili ulikuwa ni wa amani, na utulivu, kiasi kwamba hata siku ile unapokamilika hakukusikika kelele wala sauti ya nyundo (1Wafalme 6:7).. Lakini ujenzi wa hekalu la pili ambalo lilibomolewa na mfalme Nebukadneza, ulikuwa ni wa shida sana, ulikuwa ni wenye vikwanzo vingi sana, vilevile uliozungukwa na maadui wengi, ili kukwamishwa tu Hekalu lile lisijengwe.

Ni kawaida ya shetani huwa akishajua jambo fulani au ujenzi fulani unafanyika, ambao utaleta madhara makubwa katika ufalme wake huko mbeleni, au utakuwa na utukufu mkubwa Zaidi wa Mungu ni lazima alete vipingamizi vingi..Na ndivyo ilivyokuwa katika ujenzi huu, Mungu aliwaambia wayahudi kuwa utukufu wa nyumba hiyo ya pili utakuwa ni mkuu kuliko ule wa nyumba ya kwanza (Hagai 2:9). Hivyo shetani kulijua hilo akanyanyua vipingamizi vingi sana.

Na miaka kadhaa tu kabla ujenzi huo haujaanza Mungu alishamwonyesha Danieli jinsi utakavyokuwa wa shida na mgumu.

Danieli 9:25 ‘Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, KATIKA NYAKATI ZA TAABU’.

Hivyo Zeruababeli na Yoshua walipooanza kuijenga nyumba, mwanzoni tu wakakumbana na mikono ya maadui zao, wakawatisha wasiijenge, mpaka wakaenda kuomba kibali kutoka kwa mfalme, kazi hiyo isiendelee, mpaka baada ya miaka mingi kupita Mungu anawanyanyua tena mioyo yao na kuwaambia waanze kazi wasiogope.,Ndipo Mungu akawa pamoja nao na kuimaliza.

Lakini baada tena muda mrefu kupita hapo tayari hekalu limeshakamilika, shetani hakupumzika alilivamia tena hekalu, na kuharibu kuta zake, hapo ndipo tunaona Mungu akimnyanyua mtu mwingine aliyeitwa Nehemia, ili kuzisimamisha tena kuta za mji na kulikarabati hekalu, lakini mambo hayakuwa maraisi kama ilivyokuwa.

Maadui waliwalemea wakina Nehemia, ukipata nafasi pitia mwenyewe kitabu cha Nehemia usome jinsi walivyopata tabu..Mpaka ikafikia wakati sasa, kila mjenzi anabidi ajifunze na ujuzi mwingine wa ziada..Kwamba sio tu kujenga, bali pia kulinda..Kila mjenzi alilazimika kubeba silaha zake mgongoni, na wakati huo huo alikuwa anajenga..ili kwamba ikitokea tu maadui zao wamewavamia wakati wowote, basi wawezi kupambana nao. Na wengine walikuwa wakipokezana..wakati wanajenga wengine wanalinda.

Nehemia 4:16 “Ikawa tokea wakati huo, nusu ya watumishi wangu walitumika katika kazi hiyo, na nusu yao wakaishika mikuki, na ngao, na pinde, na darii; na maakida walikuwa nyuma ya nyumba yote ya Yuda.

17 Watu wale walioujenga ukuta, na wale waliochukua mizigo, walijitweka wenyewe, kila mtu alifanya kazi kwa mkono mmoja, na kwa mkono wake wa pili alishika silaha yake;

18 nao wajenzi, kila mtu alikuwa na upanga wake, umefungwa ubavuni mwake, ndivyo alivyojenga. Na yeye aliyepiga baragumu alikuwa karibu na mimi.

19 Nikawaambia wakuu, na mashehe na watu wengine; Kazi hii ni nyingi, tena kubwa, nasi tumetawanyika juu ya ukuta, kila mtu mbali na mwenzake;

20 basi mahali po pote mtakaposikia sauti ya baragumu, enendeni huko, mkatujie; Mungu wetu atatupigania.

21 Hivyo tukajitia kAtika kazi hiyo; na nusu yao waliishika mikuki, tangu alfajiri hata nyota zikatokea.

22 Kadhalika, wakati ule ule, nikawaambia watu, Kila mtu na akae ndani ya Yerusalemu pamoja na mtumishi wake, wapate kuwa walinzi wetu wakati wa usiku, na kufanya kazi wakati wa mchana.

23 Basi mimi, na ndugu zangu, na watumishi wangu, na watu wa ulinzi walionifuata, hatukuvua nguo zetu hata mmoja; kila mtu alikwenda kuteka maji akichukua silaha yake.

VIPI KUHUSU HEKALU LA SASA?

Sasa hilo lilikuwa ni hekalu la kimwili linapitia changamoto hizo, vipi kuhusu hekalu la Mungu la rohoni..ambalo ni kanisa lake? (2Wakorintho 6:16)..Tukisema kanisa hatumaanishi jengo hapana bali tunamaanisha waliomwamini Kristo..maana hiyo ndiyo tafsiri yake.. Shetani ataleta mapambano na Zaidi ya mapambano.. Kanisa la Mungu halisimami kirahisi rahisi kama wengi wanavyodhani, shetani hawezi kutulia kuangalia tu watu wanaokoka wanamfuata Kristo, wanapata uzima wa milele na asilete vipingamizi vingi..

Na hapo ndipo tunapolazimika kuvaa silaha zote za Injili kama tunavyozisoma katika Waefeso 6 ili tuweze kumpinga adui..Na silaha mojawapo ni MAOMBI.

Waefeso 6:18 ‘kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

19 pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;

20 ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena’.

Unaona, mstari wa 19 na 20 Mtume Paulo hakuona aibu kuomba aombewe..Vivyo hivyo na watumishi wote wa Mungu hata sasa tunahitaji maombi yako ili kazi ya Mungu isikwamishwe na hila zote za shetani. Hata sisi tunaoandika masomo haya mitandaoni tunaomba maombi yenu sana..kwasababu ni vipingamizi vingi sana tunakumbana navyo..wakati mwingine shetani anaharibu vifaa tunavyotumia kuandika masomo haya, inatugharimu tutumie hivyo hivyo tu kwa shida…Wakati mwingine unapomaliza tu kuandaa na kutaka ku-post ibilisi anaharibu network nzima lakini kwa upande wa masomo tu, inaweza kukuchua hata masaa 2 au zaidi ku-post somo moja tu, lakini cha ajabu wakati huo huo network iko vizuri unapofungua kurasa nyingine, wakati mwingine unapanga ufanye hichi au kile cha kiMungu lakini kinanyanyuka hiki au kile kukukwamisha..Na changamoto nyingine nyingi tu ambazo huwezi kutaja moja moja hapa..Hivyo kwa nje mambo yanaweza kuonekana yapo vizuri lakini nyuma kuna vita vingi sana vinaendelea..

Hivyo maombi yako, yana mchango mkubwa sana kwetu na kwa wengine, na kwa ajili ya injili ya Mungu isonge mbele..Sisi wenyewe hatuwezi, hivyo tuombeane sote..Adui yetu shetani anapoona watu wengi wanamgeukia Mungu hawezi kutulia.

Hakuna silaha nyingine tutakayoweza kumshinda shetani Zaidi ya maombi.

1Wathesalonike 5:25 “Ndugu, tuombeeni”

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

KAMA MHUBIRI NI WOKOVU UPI UNAUPELEKA KWA WATU?

UFUNUO: Mlango wa 11

DANIELI: Mlango wa 9

WALE WAZEE ISHIRINI NA WANNE (24), WANA KAZI GANI?

Nifanye nini ili niondokane na Hofu maishani mwangu?

HATA NA BARNABA PIA AKACHUKULIWA NA UNAFIKI WAO!!

JE KUJIUA NI DHAMBI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Atlas
Atlas
2 years ago

Amen