Nifanye nini ili niondokane na Hofu maishani mwangu?

Nifanye nini ili niondokane na Hofu maishani mwangu?

Neno Hofu linatokana na  kuogopa. mfano ukishaogopa kitu Fulani tu basi hapo hapo hofu inaingia na mashaka pia.. tuchukulie mfano umekutana na nyoka njiani, usipomuogopa ni wazi kuwa hofu haiwezi kukuingia bali utaweza aidha kumpisha apite, au kukabiliana naye. Lakini ukishaogopa tu, basi hapo hapo hofu nayo inapata nafasi, na vilevile wasiwasi au  mashaka yatakujia ambayo yatakufanya udumu katika hofu ya muda mrefu kiasi kwamba hata siku ukipita karibu na majani na ukahisi  kitu kidogo tu kinakugusa mguuni bado utadhani ni nyoka anakutembelea kwasababu mashaka tayari yalishakuingia..

Hivyo chanzo cha Hofu ni kuogopa. Lakini tukirudi katika biblia zipo hofu za aina mbili, ya kwanza ni hofu ya Mungu..Ambayo hii Mungu amekusudia tuwe nayo lakini si kwa lengo la kututisha sisi , hapana bali kwa kutufanya tumche yeye na kuzithamini amri zake.

1Petro 1:17 Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.

Luka 12:4 “Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi.

5 Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo”.

Unaona? Mtu mwenye hofu ya Mungu, ni wazi kuwa atamuheshimu Mungu, na vilevile ataziogopa hukumu zake, Hivyo itamfanya aishi katika maisha ya uangalifu zaidi na ya kumpendeza yeye.

Lakini zipo hofu nyingine zinazoasisiwa na shetani mwenyewe, mfano wa hizi ni kama.

Hofu ya magonjwa, hofu ya kuhisi hutosamehewa na Mungu (umemkufuru Roho Mtakatifu), hofu ya maadui, hofu za kukataliwa, hofu ya uzee, hofu ya kutokufanikiwa, hofu ya kushindwa, hofu ya kesho itakuwaje, hofu iliyopitiliza ya kifo,  hofu ya wachawi na mapepo kama ile waliyokuwa nayo mitume walipokuwa baharini usiku na kuona kivuli tu cha Bwana kinakuja na kuhisi kama ni mzimu umewafuata kuwaua..Hizi zote ni hofu ambazo zina asisiwa na shetani mwenyewe.  N.k

Na lengo la shetani kumletea mtu  hofu hizi zote ni kwa lengo la kumfanya akate tamaa, au arudi nyuma au akufuru au hata ikiwezekana afikie hatua ya kuutoa uhai wake au asione thamani kabisa ya maisha yake hapa duniani..

Nataka nikuambie…

Hakuna njia au suluhisho lolote la kuimaliza hofu ndani ya maisha yako, mbali na Mungu, hata uwe umefanikiwa kiasi gani, hata uwe na fedha nyingi kiasi gani, hata uwe na afya njema na elimu nzuri kiasi gani, kama Mungu hayupo ndani yako basi kipengele kimojawapo cha hofu hizi kitakuvaa tu.. Na bado utakuwa unaishi katika mateso na nafsi..

Biblia inatuambia..

1Yohana 4:16 Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.

17 Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.

18 KATIKA PENDO HAMNA HOFU; LAKINI PENDO LILILO KAMILI HUITUPA NJE HOFU, KWA MAANA HOFU INA ADHABU; NA MWENYE HOFU HAKUKAMILISHWA KATIKA PENDO.

Unaona hapo? Ukilipata hili pendo la Mungu..Basi uhakika wa kuishinda hofu ya namna yoyote ile upo ndani yako, kwasababu hilo Pendo ndilo litakaloitupa nje hofu ya namna yoyote ile. Kwasababu pale unapoamua tu kumpa Kristo maisha yako, wakati huo huo   Amani yake anaanza kuachilia juu yako ili kuiua hofu yote iliyokuwa imeufunika moyo wako kwa muda mrefu.

Sikiliza maneno ya YESU..

Yohana 14:27 “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga”.

Yesu anatoa amani ambayo huwezi kuipata kwa mtu yeyote, wala kutoka katika dini yeyote wala katika chuo chochote  kile, yeye hakufariji katika hofu yako kwa wanadamu wafanyavyo bali anakupa Amani inayoondoa hofu yote.

Anasema tena..

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Mimi kabla sijaokoka nilikuwa ni mtu mwenyewe hofu ya hukumu, na ya maisha isiyokuwa ya kawaida, mpaka ilifikia wakati ikanifanya nijione kama maisha yangu hayana thamani yoyote na kujisemea moyoni kwanini Mungu aliniumba mimi si ni heri angeniumba mjusi au ndege ningekuwa sina hatia yoyote ile..lakini ashukuruwe Mungu ulipofika wakati wa YESU kunifungua kutoka katika minyororo hiyo ya shetani..Na kunipa wokovu..Tangu huo wakati hadi sasa nimekuwa nikiisha maisha ya amani nyingi sana..Sina hofu yoyote haijalishi nipo katika hali gani ile amani yake ya tumaini la uzima wa milele linabubujika ndani yangu kila siku.

Sina hofu ya wachawi, wala hukumu, wala ya kushindwa, wala ya chochote kwasababu, Pendo lake kalimwaga ndani yangu..

Vivyo hivyo na wewe leo hii, ukiwa tayari kumruhusu Bwana Yesu ayabadilishe maisha yako, atakupa AMANI hii ambayo anaitoa bure..Unachopaswa kufanya ni kufungua tu moyo wako leo..

Kama upo tayari kufanya hivyo leo basi nataka nikuambie uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao utaufurahia maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwangu mimi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.

Na ile amani ya Mungu utaanza kuiona inaumbwa upya ndani yako.

Vile vile baada ya kutubu kwako bila kukawia kawia, unahitaji kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Luka 12:32 “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme”

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

IFANYE KAZI YA MUNGU PASIPO HOFU!

TOA SADAKA ISIYO NA KASORO KWA BWANA.

Nifanye nini ili niwe na uhakika nikifa naenda mbinguni?

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

KWANINI NAYAWEZA MAMBO YOTE KATIKA YEYE ANITIAYE NGUVU?

NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

UNAMALIZAJE MWAKA WAKO, JE NA MUNGU AU SHETANI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments