MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze tena maandiko siku ya leo. Kwasababu Neno la Mungu ndio mwanga wa njia zetu na taa iongozayo miguu yetu. Maana yake tukiwa na Neno la Mungu vya kutosha ndani yetu basi njia ya maisha yetu itakuwa wazi, tutakuwa tunajua tulikotoka, tulipo sasa na tunapokokwenda…kwasababu ile Nuru inamulika nyuma yetu, mahali tulipo na mahali tunapoelekea.

Kama wengi wetu tunavyojua kuwa muunganiko wa madhehebu na dini ni mpango wa Yule Adui. Lakini unaweza kujiuliza ni kwanini uwe ni mpango wa Adui na ilihali tunajua kuungana ni jambo jema na zaidi ya yote Biblia imehimiza tuwe na umoja.(Yohana 17:11, Yohana 17:21, Waefeso 4:3 na Waefeso 4:13)..Mistari yote hiyo inazungumzia suala la umoja. Lakini kwanini huu muunganiko wa madhehebu na dini usiwe ni mpango wa Mungu?. Kama kweli ni mtu wa kutafakari hili swali ni lazima utajiuliza..Na kama hutachunguza kwa makini unaweza ukajikuta unakubaliana nalo na kusema hakuna ubaya wowote kuwepo umoja huo au unaweza kujikuta unakuwa tu mshabiki wa kuupinga lakini usijue ni kwanini unaupinga..

Hivyo leo kwa neema za Bwana tutaangalia kasoro moja iliyopo katika muungano huo kwa kutumia Biblia na mifano dhahiri katika maisha …ambayo hiyo ndio itakayotufanya tuhukumu wenyewe kama kweli ni mpango wa Mungu au sio mpango wa Mungu..

Kabla ya kwenda kwenye biblia hebu tafakari mfano huu kisha tutakwenda kwenye maandiko..

Wanandoa wawili ambao wamefunga ndoa halali mbele ya madhabahu ya Mungu…wamegombana na kuachana na kila mmoja akaenda kuoa na kuolewa na mwingine…na huko walikokwenda kila mmoja akapata watoto..na wakawa wamekaa katika hali hiyo muda mrefu sana miaka mingi sana ikapita pasipo kuonana wala kuwasiliana kwa ufupi kila mmoja akawa ameanza maisha yake mengine na ana mipango yake…

Siku moja katika shughuli zao wakakutana mahali pamoja pa kazi kila mmoja akiwa na mpenzi wake mpya na watoto wake…

Sasa kwasababu tayari kila mmoja ana mpenzi wake mpya na familia mpya, na walishaachana kitambo na wameshakuwa watu wazima sana hata ule upendo haupo tena…. ikabidi watambulishane tu kwamba huyu alikuwa ni mpenzi wangu wa zamani lakini tulishaachana kitambo sana..kila mmoja akamtambulisha mwenziwe na sasa hatuna mahusiano yoyote…lakini kwasababu wote tumekutana na shughuli yetu ni moja basi hebu tushirikiane tufanye kazi pamoja tujiendeleze kiuchumi na kutunza familia zetu..

Hivyo familia hizo mbili zikaungana kufanya kazi pamoja…kwahiyo kukawa na kaumoja Fulani lakini si cha mahusiano bali cha maslahi fulani. Familia hizo zikawa zinakutana kuuziana bidhaa na kushirikishana fursa mpya za kazi, na kutekeleza mipango mengine ya kimaisha n.k..

Sasa hebu jiulize?..Huo muungano ni muungano wa ki-Mungu?…Ni kweli wameungana, wanasadiana kiuchumi, kimawazo na hata kifursa lakini mbele za Mungu wanaonekanaje?..Mbele za Mungu wanaonekana ni wazinzi na waliotengana…maandiko yanasema hivyo…

Luka 16:18 “Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini”.

Haijalishi watafanya vitu vingapi kwa umoja, mbele za Mungu wanaishi katika uzinzi, haijalishi wameachana kwa makubaliano mazuri kiasi gani, haijalishi watakwenda pamoja kusaidia mayatima na maskini kwenye makambi lakini mbele za Mungu bado ni wazinzi..Na hivyo huo umoja ni umoja wa shetani hata kama wanafanya mema elfu, wakifa wote wanakwenda motoni…Kwasababu Mungu hawezi kuunganisha wazinzi wawili wapatane..Badala yake Mungu angewarudisha kwanza warudiane ili wasiishi katika uzinzi..na ndipo hayo mambo mengine yafuate.

Ili uwe umoja wa KiMungu ilikuwa ni sharti kila mmoja amrudie mpenzi wake wa kwanza ambaye walifunga naye ndoa kanisani, na kuachana na huyu aliyenaye sasa….Endapo wangerudiana na kuungana kwa namna hiyo, hapo mbele za Mungu wangekuwa wameungana na hivyo ungekuwa tayari ni umoja upo katikati yao.

Ndicho kinachotokea kwenye madhehebu sasa…Shetani kawatenganisha wakristo na kuwaweka katika makundi makundi…dhehebu hili, na lile…kaondoa ule umoja wa Roho ambao ulianza pale Pentekoste ambapo hakukuwa na dhehebu lolote wote walikuwa wamoja…

Matendo 2: 44 “Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika”.

Mitume hawakuanzisha madhehebu…waamini wote walikuwa ni kitu kimoja…Sasa shetani kashatutenganisha..halafu anataka kutuunganisha katika hali ya matengano tuliyopo…tupo tumetengana na bado anataka tuungane tusaidiane kifursa, TAG na EAGT tuungane tusaidiane kutatua matatizo Fulani Fulani ya kijamii, Lutheran na katoliki tuungane, Anglikana na Morovian tuungane ili tushirikiane kutatua kwa pamoja matatizo Fulani Fulani. Wakati kila mmoja msingi wa Imani zetu zimepishana.

Je! unadhani huo ni mwunganiko wa kiMungu?…La! hata kidogo sio muunganiko wa kiMungu kabisa… Ili uwe muunganiko wa kiMungu ni sharti wakristo wote tungepaswa tuungane na kuwa kitu kimoja katiba yetu ikiwa biblia na si kuunganisha madhehebu…pasipowepo kusema mimi ni wa dhehebu hili au lile..wote jina letu linapaswa liwe moja (wakristo), huo ndio umoja wa Roho unaozungumziwa katika maandiko kwamba tunapaswa tuwe nao..

Ni sawa na kijana kapewa gunia la mchele la kila 50, na akaambiwa akifika nyumbani auchanganye vizuri na kuutoa uchafu na kisha ahamishie ule mchele kwenye gunia lingine lililosafi zaidi…na kijana alipofika nyumbani akalifungua akaanza kutenga ule mchele kuuweka kwenye vifungashio tofauti tofauti .. akatenga kilo 5 akazifungia kwenye mfuko, kilo nyingine kumi kwenye gazeti, kilo nyingine 2 kwenye kichupa kidogo, nyingine 4 kwenye kopo nyingine 8 kwenye kijimfuko cha rambo nyingine 10 kwenye kiroba na hicho kiroba akakipiga lebo..mpaka zilipotimia zote 50. Na akavichukua hivyo vifungashio vyote na viroba vyote akavitumbukiza kwenye gunia hilo jipya la kila 50.Na kusema tayari kauleta pamoja ule mchele…hapo kauleta mchele pamoja au viroba pamoja?..Atakuwa hajatumia akili kwasababu alipaswa aumimine mchele wote uliosafi kwenye lile gunia moja haikuhitajika tena kufungwa matita matita. Na madhehebu yote ni vifungashio…ndani ya Gunia kuu la ukristo.

Na vifungashio hivyo Mungu kavikataa..Ndio maana anasema katika Ufunuo 18: 4 “Tokeni kwake enyi watu wangu..msishiriki dhambi zake”..Maana yake tutoke kwenye kamba za udini na madhehebu…tuunganike wakristo na si madhehebu..

Ndio Mungu kaweka tofuati ya utendaji kazi katika kanisa, Lakini kumbuka ni utofauti wa utendaji kazi, na sio utofauti wa Imani,..Leo hii katika ukristo zipo Imani tofauti tofauti haiwezekani mmoja anaamini mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu ni mmoja tu Yesu Kristo, mwingine anasema pembeni ya Yesu kuna mwingine anayeitwa Mariamu n.k. Halafu hao wote bado wawe kitu kimoja. Na kibaya Zaidi umoja huu unalenga kufikia hadi kuunganika na dini nyingine zisizomtambua hata Kristo.

Sasa tukirudi katika maandiko madhara ya muunganiko huo ni nini?

Madhara ya muunganiko wa madhehebu ni kuitengenezea njia roho ya Mpinga kristo kufanya kazi…Kumbuka Mpinga-kristo atakuwa ni mtu wa kidini na atakuwa mshirika wa muungano huo..Roho ya kumpinga kristo haianzii freemason, kama wengi wanavyofikiri, wala kwa waislamu, wala kwa mabudha…roho ya mpingakristo inaanzia kwenye huu umoja wa dini na madhehebu…Waliompinga Kristo wa kwanza wakati akiwa hapa duniani hawakuwa wachawi, wala watu wa mataifa bali walikuwa ni mafarisayo na masadukayo (watu waliokuwa wameshika sana dini).

Sasa mafarisayo na masadukayo yalikuwa ni madhehebu ya kiyahudi…Kila moja lilikuwa linadai linamjua Mungu zaidi ya lingine…hivyo yakatengana kama madhebu yalivyotengana leo..na baada ya kutengana wakati Bwana Yesu anakuja na kuhubiri…yakainuka yote kumpinga Bwana Yesu na kufanya shauri pamoja ya kumuua…Na muunganiko wa madhehebu leo hii utakuja kusimama kuwapinga wakristo wakweli katika siku za mwisho, na kuwaletea dhiki.

Yohana 16:2 “Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada”.

Na yatamtengenezea njia pana Mpinga-Kristo ambaye atanyanyuka na kuutumia huo muungano  kuiunda ile CHAPA YA MNYAMA. Ambapo itafikia kipindi watu hawataweza kununu wala kuuza bila kuwa mshirika wa umoja wa muungano huo.

Mathayo 22: 34 “Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja”.

Je upo chini ya kifungashio gani? Cha Neno la Mungu au cha dhehebu lako?..Je unajisifia dhehebu au Imani?..Hebu jifikirie tangu upo katika dhehebu lako umejifunza kuhusu kumjua Yesu kiasi gani?..unamjua Mungu kiasi gani,Neno unalifahamu na umelishika kiasi gani?..je umekuwa mtakatifu kiasi gani?..una uhakika kwa kiasi gani kwenda mbinguni?..Je umeshawahi kutenga muda mwenyewe pasipo kuambiwa kusoma maandiko?, au kusali au kwenda kuwahubiria wengine habari njema…

Kama hujawahi kufanya hayo na zaidi ya hayo na bado unajiisifia dhehebu…tenga muda ujitafakari tena ndugu yangu…Usijisifie dhehebu, wala usiufurahie kila muungano unaosimama mbele yako…Rudi katika Neno la Mungu ambalo ndio katiba yetu. Unyakuo umekaribia sana, Kristo anakaribia kuja na Mpinga-Kristo kashatengeneza mazingira yake yote ya kufanya kazi zake.

Bwana akubariki.

Tafadhali share na kwa wengine na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo ya kujifunza kwa njia ya inbox au whatsapp basi utatutumia ujumbe kwa namba hii 0789001312

Mada Nyinginezo:

MPINGA-KRISTO

MUUNGANO WA DINI NA MADHEHEBU YOTE, UMEKARIBIA.

Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?

ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!

Sabato halisi ni lini, Je! ni Jumapili au Jumamosi?, Ni siku gani itupasayo kuabudu?

NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments