HAPAKUWA NA NAFASI YA KUPITA KWA YULE MNYAMA ALIYEKUWA CHINI YANGU.

HAPAKUWA NA NAFASI YA KUPITA KWA YULE MNYAMA ALIYEKUWA CHINI YANGU.

Nakusalimu katika jina kuu la mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Nehemia ni mtu  aliyekusudia kutoka katika moyo wake, kwenda kuukarabati ukuta wa Yerusalemu uliokuwa umebomoka, mtu huyu hakuwa nabii, wala kuhani, wala hakujulikana popote, lakini kwa kuguswa kwake moyoni kwa habari alizozisikia kuhusiana na uharibifu ule, aliumia sana, ndipo akajitia nguvu, kumwomba Mungu kibali na baadaye akapewa, na kuweza kwenda Yerusalemu kwa ajili ya kazi hiyo ya kuukarabati. Sasa hatuna muda wa kueleza historia yote, kwa muda wako waweza kusoma habari yake tangu mwanzo hadi mwisho katika kitabu hicho.

Hivyo naamini kwa kuyatazama mapito yake, utapata funzo, hata na wewe ambaye, anataka kuingia katika kazi ya kusimama “mahali palipobomoka” ili upakarabati.

Sasa wakati Nehemia anafika Yerusalemu, ili kuanza operasheni yake ya kuujenga tena ukuta ule, ilimbidi kwanza, atembee, katika malango yote, na sehemu zote za ukuta huo ili atathimini, uharibifu uliotokea, pamoja na nguvu na gharama zitakazotumika kuukarabati tena..

Biblia inatuambia, aliondoka, usiku wakati ambapo watu wamelala, akaanza kuuzunguka ukuta ule wa mji ambao ulikuwa ni mrefu sana, Kuonyesha kuwa mpango bora wa kukarabati kusudi la Mungu, huwa hashirikishwi  kila mtu, bali watu wachache sana tena, waaminifu, ambao wanaweza kuchukua mzigo wako..Tusome

Nehemia 2:11 “Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu.

12 Kisha nikaondoka usiku, mimi na watu wachache pamoja nami; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe”.

Anaendelea kusema…

13 Nikatoka nje usiku, kwa njia ya lango la bondeni, nikashika njia iendayo kisima cha joka, na lango la jaa; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto. 14 Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; LAKINI HAPAKUWA NA NAFASI YA KUPITA KWA YULE MNYAMA ALIYEKUWA CHINI YANGU.

15 Kisha nikapanda usiku kando ya kijito, nikautazama ukuta; kisha nikarudi nyuma, nikaingia kwa lango la bondeni, nikarejea hivyo.

16 Wala mashehe hawakujua nilikokwenda, wala nilivyotenda; wala sijawaambia Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala mashehe, wala watu wengine waliokuwa wakiifanya kazi hiyo. 17 Kisha nikawaambia, Mnaona hali hii dhaifu tuliyo nayo, jinsi Yerusalemu ulivyo hali ya ukiwa, na malango yake yalivyoteketezwa kwa moto; haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu, ili tusiwe shutumu tena.

Hapo mwanzo alipoanza safari,alikuwa na mnyama wake, Ambaye ni farasi/punda.. Mnyama Yule alimsaidia sehemu baadhi tu kufika,na kuona uharibifu uliotokea katika kuta, lakini alifika mahali, ambapo mnyama asingeweza kupita katika penyo zile, bali ni mtu tu! Hapo ndipo ikabidi amwache mnyama Yule, atembee yeye kama yeye, mguu kwa mguu, kutazama sehemu za ukuta, ndogo ndogo, za mafichoni, zilizokuwa zimeharibiwa vibaya sana na maadui zao. Asingefanya hivyo, ukarabati wake ungeishia pale pale punda alipoishia, asingekarabati kote.

Ndipo alipomaliza ziara hiyo, akarejea mjini, na kuwaambia makuhani na wahusika wote, hali ilivyokuwa.

Sasa ni nini Bwana anatufundisha katika habari hii?

Bwana anasema..

Ezekieli 22:30 “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu”.

Sikuzote kusimama mahali palipomoboka si rahisi, Mungu anatafuta watu hao mfano wa Nehemia hawaoni,,ni lazima tufahamu kuwa zipo gharama kubwa sana, za kukarabati, waweza kudhani, utakwenda na taasisi, au utakwenda na ushirika, au utakwenda na kiwango Fulani cha pesa kwenye akaunti yako.. Hapana vyote hivyo vinaweza kukusaidia kwa muda tu, bali utafika wakati hivyo vyote havitakusaidia, bali itakubidi usimame wewe kama wewe, kama ni kuomba, kama ni kuhubiri, kama ni kukemea dhambi, kama ni kuanzisha jambo..

Mnyama aliye chini yako, hataweza kuvuka nawe, ndugu zako hawataweza kutembea na wewe,katika maono hayo Mungu aliyokupa juu ya kusudi lake, .. Bali ni wewe kama wewe.

Ilimpasa Nehemia afanye hivi, japokuwa alipitia changamoto nyingi, mpaka mbeleni wakawa wanamdhihaki na kumwambia, ukuta unaoujenga jinsi ulivyo dhaifu, hata mbweha wakipita juu yake utaanguka.(Nehemia 4:3), Lakini hakuvunjika moyo, yeye aliendelea  kusimama mpaka mwisho ..

Walipokuwa wanaujenga, mkono mmoja ulishika silaha, na mwingine tofali, waliujenga katika hofu, usiku kucha, Lakini mwishoni ulikamilika, katika utukufu mwingi. Na faida yake ni kwamba hadi sasa tunaisoma habari ya Mtu huyu Nehemia, na kumbukumbu lake lipo hadi leo.(Nehemia 4: 17-23)

Ndugu zipo kuta nyingi sana zilizobomolewa na ibilisi, hadi sasa Bwana anatafuta watu watakaosimama, makanisani kujenga nyumba yake, watakaosimama kwa vijana, kuwaweka kwenye misingi ya imani, watakaosimama kwa familia na watoto kuwafundisha kumcha Bwana. Watakaosimama katika Neno la Mungu, kufundisha injili ya kweli isiyoghoshiwa, na kukemea mafundisho potofu..

Swali ni Je! Sisi tutaweza kusimama na kujenga upya?

Kama ni hivyo basi tuwe tayari hata wakati mwingine kusimama peke yetu, kama Nehemia, pale ambapo hatuona sapoti, uwe ndio wakati wa kusonga mbele, na kuitenda kazi ya Mungu, pale ambapo tunaona vita, na dhihaka, tusife moyo bali uwe ndio tuifanye kazi, usivunjike moyo wala usikate tamaa..Kwasababu Kujenga kuna gharama. Lakini faida zake ni kubwa sana mwishoni.

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kisima cha joka na lango la jaa ni nini?(Nehemia 2:13)

Wana wa Asafu ni akina nani katika biblia?

Mlango uitwao “Mzuri” Unaozungumziwa katika Matendo 3:2 ndio upi?

TIMAZI NI NINI

UFUNUO: Mlango wa 17

Pango la Makpela ni lipi, je lina umuhimu wowote kwetu?

Neno Buruji lina maana gani katika biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments