MAJARIBU 10 WANA WA ISRAELI WALIYOMJARIBU MUNGU.

MAJARIBU 10 WANA WA ISRAELI WALIYOMJARIBU MUNGU.

Hesabu 14:22 “kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya WAMENIJARIBU MARA HIZI KUMI, wala hawakuisikiza sauti yangu; 

23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;

24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki”

Maandiko yanaonyesha kuwa wana wa Israeli walimjaribu Mungu MARA KUMI, je ni wapi katika maandiko panaonyesha hayo?

1. JARIBU LA KWANZA: (Mkabala na bahari ya Shamu)

Kutoka 14:9 “Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. 

10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana. 

11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?

12 Neno hili silo tulilokuambia huko Misri”

Hili ndio jaribu la Kwanza wana wa Israeli walilomjaribu nalo Mungu, ijapokuwa walishaona matendo yake makuu kwa Farao na Misri yote kwa ujumla jinsi alivyoipiga Misri na kuiharibu kwa ishara kubwa na maajabu mengi, lakini hapa wanamjaribu Mungu kuangalia kama atawapigania tena kinyume na Farao au la!.. jambo ambalo ni dhambi kwao kwani tayari wanaujua uweza wa Mungu na hivyo hakuna haja ya kumjaribu ili kuona atakachokifanya.

2. JARIBU LA PILI: (Maji ya Mara)

Kutoka 15:22 “Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

 23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. 

24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko”

Hili ni jaribu la pili, baada ya kuona uweza wa Mungu wa kupasua bahari, lakini bado wakamjaribu Mungu kuangalia kama atawafanyia muujiza wa Maji au la.. Na Bwana akawapa maji kama walivyotaka lakini bado hawakuridhika…

3. JARIBU LA TATU: (Katika bara ya Sini, kutaka Nyama)

Kutoka 16:1 “Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri

2 Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; 

3 wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.”

Hili ni jaribu la tatu baada ya kumjaribu Bwana kwa maji ya Mara na sasa wanataka kumwangalia Bwana kama anaweza kuwafanyia muujiza wa Nyama katikati ya jangwa, na Bwana akawapa nyama, kama walivyotaka lakini bado hawakuchoka kumjaribu..

4. JARIBU LA NNE: (Kusaza kwa Mana).

Kutoka 16:19 “Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.

 20 Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana”

Walipewa maagizo wasikisaze (yaani wasibakishe chochote mpaka asubuhi) lakini wao wakafanya kinyume chake kwa kusudi la kuchunguza ni nini kitatokea.

5. JARIBU LA TANO: (Ukusanyaji wa Mana siku ya Sabato)

Kutoka 16:26 “Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana. 

27 Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione. 

28 Bwana akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini? “

Mungu aliwaambia wasitoke kwenda kuokota Mana siku ya Sabato, bali wapumzike, kwasababu hiyo mana haitapatikana siku hiyo, lakini wenyewe wakatoka kwenda kuhakiki kama kweli haitapatikana?.. hivyo ikawa ni dhambi kwao.

6. JARIBU LA SITA: (Maji ya Refidimu).

Kutoka 17:1 “Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama Bwana alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe.

2 Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu Bwana?

3 Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?”

Baada ya kumjaribu Bwana kule Mara, kwa kutaka maji, sasa wanarudia tena yale yale makosa.. ya kutaka watokezewe maji ya kimiujiza..Kulikuwa hakuna haja ya kumjaribu Mungu mara ya pili, kwani tayari walishaona uweza wake mara ya kwanza, lakini wao walitaka kuona tena na tena..

7. JARIBU LA SABA: (Sanamu ya Ndama).

Kutoka 32:7 “Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao,

8 wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri”

Wametoka kunywa maji kimiujiza katika Mwamba, na kuhakiki kwamba Bwana yupo katikati yao, lakini hapa wanafanya makusudi kutengeneza sanamu ya Ndama, kama ishara ya kumsusia Mungu, ambaye wanajua kabisa yupo..

8. JARIBU LA NANE: (Moto wa Tabera)

Hesabu 11:1 “Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. 

2 Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma.

3 Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao’

Manung’uniko haya ni yale ya kutafuta kuona kitu cha kimwujiza kutoka kwa Mungu, kwasababu walikuwa wameshajua kuwa Mungu anaweza kufanya lolote..

9. JARIBU LA TISA: (Tamaa ya Nyama)

 Hesabu 11:4 “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?

 5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;

 6 lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu”

Wana wa Israeli wanataka nyama, si kwasababu walikuwa na njaa sana, bali kwasababu walikuwa wanataka kuona jambo jipya kutoka kwa Bwana..

10. JARIBU LA KUMI: (Wapelelezi wa Kaanani)

Hesabu 14:1 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.

 2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. 

3 Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?

4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri”.

Hili ndilo jaribu la mwisho, wana wa Israeli walilomjaribu nalo Mungu, nalo ndilo likawa Muhuri wa wao kuipoteza ahadi ya kuiona ile nchi, isipokuwa watu wa wawili tu, ambao ni Yoshua na Kalebu.

Nasi pia tunachoweza kujifunza katika habari hiyo kuwa “KUMJARIBU MUNGU NI DHAMBI KUBWA SANA”.

Kama tumeshaujua uweza wake kwanini tumjaribu?.. kama tumeshajua kuwa Mungu anaweza kutuokoa na hatari kwanini tujiweke katika hatari??.. Kama tumeshajua kuwa Mungu anaweza kutuokoa na yule mwovu kwanini basi tujisogeze karibu na yule Mwovu??.. Kama tumeshajua kuwa “tutakapokula vitu vya kufisha, havitatudhuru, kwanini basi tuvile makusudi”, kama umeshajua kuwa Mungu ni mponyaji kwanini basi tunywe sumu makusudi?..

Kama umeshajua kuwa Bwana anakupenda kwanini ujiuze kwenye dhambi ili uujaribu upendo wake???.. unadhani utabaki salama?

Ndicho wana wa Israeli walichokuwa wanakifanya, pasipo kujua kuwa wanafanya dhambi kubwa sana, ambayo itawagharimu kukosa kuingia Kaanani.

Kumbuka Hili ndilo jaribu ambalo shetani anawaangusha nalo watu wengi hata siku hizi za mwisho, na ndilo hata alilolichagua kama moja kati ya majaribu yake matatu yenye nguvu kubwa, ili aweze kumwangusha Bwana Yesu lakini alishindwa!,

Mathayo 4:5 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,

6  akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe

7  Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.”

Na wewe usimjaribu Bwana, usiujaribu Msalaba.

Bwana akubariki.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.

JIHADHARI NA MKUTANO WA WATU WALIOCHANGANYIKANA.

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.

Je Ni kweli haturuhusiwi kula nyama kulingana na Isaya 66:3?

UPEPO WA KUSI HULETA MVUA;

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments