SALA YA BWANA. (Namna ya kuiomba)

SALA YA BWANA. (Namna ya kuiomba)

Sala ya Bwana ni sala ambayo Bwana wetu Yesu Kristo aliwafundisha wanafunzi wake, kabla ya kuondoka kwake. Na kwa kupita sala ile, hakuwafundisha tu wanafunzi wake bali alitufundisha na sisi pia, maana yake ni kwamba, nasi pia tunapaswa tuombe kama vile Bwana alivyowaelekeza wanafunzi wake.

Lakini ni muhimu kuielewa sala hii kwa mapana, ili kusudi tuisikose shabaha tunapoomba.. Kwa maana tusipoielewa vizuri basi tutajikuta tunaifanya kama Mashairi (kwa kuirudia rudia kama watu wa mataifa, wanavyofanya wanapoiomba miungu yao).. Sisi biblia imetuambia tusifanane na hao.(Mathayo 6:7).

Sasa sala ya Bwana Imegawanyika katika vipengele vikuu nane (8).. Na vipengele hivyo sio sala yenyewe bali ni kama “maelekezo ya sala”. Sala yenyewe hatuwezi kuandikiwa, bali tunaomba kila mtu kulingana na anavyoongozwa au kujaliwa na Roho Mtakatifu.

Ni sawa mtu akupe vipengele saba vya kuombea, akakuambia ombea Familia, ombea Taifa, ombea Kanisa, ombea Marafiki.. Sasa kwa kukwambia hivyo huwezi kwenda kupiga magoti na kusema naombea Taifa, kanisa, ndugu na marafiki halafu basi uwe umemaliza!, Huwezi kufanya hivyo.. bali utakachofanya ni kuzama ndani kwa kila kipengele kukiombea..

Kwamfano Katika kipengele cha kuombea Taifa utaombea Viongozi wote na Hali, na hali ya Taifa, na  ya Imani kwa ujumla katika Taifa zima, jambo ambalo linaweza kuchukua dakika kadhaa au masaa kadhaa, vile vile katika Familia, na katika kanisa utafanya hivyo hivyo..zitahitajika dakika nyingi kwasababu  kuna watu wengi katika familia, na kuna matatizo mengi ambayo ukianza kuyataja mbele za Mungu, huenda yakachukua dakika nyingi au masaa mengi.. Hivyo kwa vipengele tu hivyo vichache unaweza kujikuta unasali hata masaa 6.

Vile vile katika sala ya Bwana, ni hivyo hivyo,  vile alivyoviorodhesha Bwana ni vipengele tu, na sio sala yenyewe, maana yake Mitume hawakuchukua hiyo sala na kuikariri kama shairi na kisha kuirudia rudia kila wakati kabla na baada ya kulala, kama inavyozoeleka leo kufanyika hivyo.

Sasa hebu tuisome sala yenyewe na kisha tutazame kipengele kimoja baada ya kingine.

Mathayo 6:7 “Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.

8 Basi msifanane na hao; maana BABA YENU ANAJUA MNAYOHITAJI KABLA NINYI HAMJAMWOMBA.

9 BASI NINYI SALINI HIVI; BABA YETU ULIYE MBINGUNI, JINA LAKO LITUKUZWE, UFALME WAKO UJE,

10 MAPENZI YAKO YATIMIZWE, HAPA DUNIANI KAMA HUKO MBINGUNI.

11 UTUPE LEO RIZIKI YETU.

12 UTUSAMEHE DENI ZETU, KAMA SISI NASI TUWASAMEHEVYO WADENI WETU.

13 NA USITUTIE MAJARIBUNI, LAKINI UTUOKOE NA YULE MWOVU. [KWA KUWA UFALME NI WAKO, NA NGUVU, NA UTUKUFU, HATA MILELE. AMINA.]”

1.BABA YETU ULIYE MBINGUNI

Hiki ni kipengele cha kwanza, ambacho Bwana anatuelekeza tuanze nacho katika sala zetu. Kwamba maombi yetu tuyaelekeze kwa Baba aliye mbinguni, kwamba tumwite Baba asikie maombi yetu na haja zetu, na yeye ni mwaminifu atatupa kama tutakavyomwomba, ikiwa tutaomba sawasawa na mapenzi yake.

Na jambo la kuzingatia hapo ni kwamba Bwana Yesu anatufundisha kuomba kwa “Baba” na sio  kwa “Mungu”. Sasa Baba ndio huyo huyo Mungu, lakini cheo cha ubaba kinahubiri mahusiano mazuri zaidi kwetu na aliyetuumba kuliko cheo cha UMUNGU.  Viumbe vyote vinamwona muumba kama Mungu, lakini kwetu sisi wanadamu tumepewa heshima ya kipekee kwamba tumwite Mungu, Baba yetu (1Yohana 3:1).

Kwahiyo tunapoingia kwenye sala/ maombi ni vizuri sana kuomba kwa kumwita muumba wako Baba kuliko Mungu, kwasababu wewe ni zaidi ya kiumbe chake bali ni mtoto wake.

Luka 11:11 “Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?

12 Au akimwomba yai, atampa nge?

13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”

2. JINA LAKO LITAKASWE/ LITUKUZWE

Baada ya kumwita Baba aliye mbinguni kwamba atege sikio lake na kusikia maombi yetu sisi watoto wake, Hoja ya kwanza tunayopaswa tumpelekee ni kwamba JINA LAKE LITAKASWE au LITUKUZWE. Wengi hawajui kuwa jina la Mungu linachafuliwa kila siku kutokana na maovu watu wa Mungu wanayoyafanya..

Warumi 2:22 “Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?

23 Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?

24 KWA MAANA JINA LA MUNGU LATUKANWA KATIKA MATAIFA KWA AJILI YENU, kama ilivyoandikwa”.

Madhara ya jina la Mungu kutukanwa katika mataifa, ni watu wengi kupotea na kuifanya thamani ya msalaba isionekane.. Hivyo basi mwenye uwezo wa kulitakasa jina lake ni Mungu tu, (yeye mwenye jina), hivyo tunapochukua nafasi hiyo ya kuomba kwamba Bwana alitakase jina lake, maana yake tunaomba Mungu alete utukufu katika Injili yake.. Kwamba Bwana ajalie watu kuliogopa jina lake, kwa kuonyesha matendo makuu na ya ajabu, na hivyo wengi kutubu na kumrudishia yeye utukufu.

Kwahiyo hii inapaswa iwe sehemu ya sala kwa kila mkristo kila mahali..

3. UFALME WAKO UJE.

Siku ambayo Ufalme wa Mungu utakuja duniani ni siku ambayo Mateso yatakuwa yameisha, tabu zitakuwa zimeisha, huzuni zitakuwa zimeisha, na maumivu yatakuwa yameisha.. (hakika huo ni wakati mzuri sana). Dunia ya sasa imejaa tabu na mahangaiko na majaribu mengi.. hivyo kila siku hatuna budi kuomba kwa Baba kwamba aharakishe kuileta ile siku ambayo tutapata pumziko la hakika, dhidi ya haya majaribu mengi ya ulimwengu.

Kwa mtu ambaye anatamani kuondokana na haya maisha na kutamani kukaa na Mungu milele, basi atatumia muda wa kutosha kumwomba Bwana aulete ufalme wake. Na kwa kuomba hivi maana yake, tunaomba pia watu wengi waokolewe, kwasababu ile siku haitakuja mpaka kondoo wa mwisho aliyekusudiwa uzima wa milele, aingie ndani ya zizi.. Hivyo basi kwa kuomba ufalme wake uje basi moja kwa moja pia tutakuwa tumeomba Bwana aharakishe kuwavuta watu wake ndani ya Neema.

4. MAPENZI YAKO YATIMIZWE.

Baada ya kuomba kwamba ufalme wake uje, basi hatua inayofuata ni kuomba kwamba Mapenzi yake yatimizwe.. Tunayo mapenzi yetu (yaani matakwa yetu), lakini pia yapo mapenzi ya Mungu ambayo huwenda sisi hatuyafahamu.. Bwana Yesu kabla ya kuteswa alimwomba Baba na kusema, “kikombe hiki kiniepuka lakini si kama nitakavyo mimi bali utakavyo wewe  soma Mathayo 6:39.

Na sisi hatuna budi kuomba kuwa mapenzi ya Mungu yatimizwe hapa duniani, katika shughuli zetu, katika utendaji kazi wetu, na katika mambo yote yanayoendelea, mapenzi yake yakatimizwe kama yanavyotimizwa huko mbinguni, mahali malaika walipo..

5. UTUPE LEO RIZIKI ZETU.

Baada ya kuomba mapenzi yake yatimizwe, sasa ni wakati wa sisi kupeleka haja zetu, kama chakula, mavazi, makazi, fedha, na mambo yote tunayoyahitaji katika mwili na katika roho, Baba akatupatie.. Na Mungu anayesikia maombi atatupa kama ni fedha, au chakula au makazi au malazi, vile vile katika kipengele hiki ndicho kipengele pia cha kuwaombea wengine Bwana awape pia riziki, hivyo kinaweza kuchukua muda mrefu, kulingana na haja mtu alizonazo.

6. UTUSAMEHE DENI ZETU.

Ipo tofauti ya Deni na dhambi,  Mtu anaweza kusamehewa dhambi lakini Deni la adhabu lipo palepale, Daudi alisamehewa dhambi yake ya kumtwaa mke wa Uria, lakini deni la kuadhibiwa yeye na mtoto wake halikuondoka, na hapa sala ya Bwana inatuelekeza kwamba tumwombe Bwana atusamehe Deni zetu, huenda tumemkosa Mungu na tukamwomba msamaha na yeye akatusamehe lakini adhabu bado hajaiondoa.. hivyo hatuna budi kumwomba Mungu kwa kuugua sana kwamba atuondolee dhambi zetu pamoja na madeni yetu,

Hapa mtu anaweza kutumia muda mrefu, kujiombea mwenyewe na kuwaombea wengine. Lakini tunapoomba tusamehewe madeni ni sharti kwamba na sisi tuwasamehe wadeni wetu, tusipowasamehe wadeni wetu na Baba yetu aliye mbinguni hatatusamehe sisi.

7. USITUTIE MAJARIBUNI, BALI UTUOKOE NA YULE MWOVU.

Shetani anatutafuta usiku na mchana ili atuingize katika kukosa, sasa hila zote za shetani ili kutuangusha sisi ndio “majaribu yanayozungumziwa hapo”

Bwana anatufundisha kumwomba Baba, atuepushe na mitego hiyo ya mwovu, ambayo kaiweka kila mahali ili kutuangusha, na mitego hiyo shetani kaiweka makanisani, mashuleni, makazini na kila mahali.. hivyo lazima kuomba kwa muda mrefu kwaajili ya mahali ulipo, au unapokwenda ili kusudi usianguke katika mitego ya ibilisi. Na pia unapaswa uwaombee na wengine. (Wagalatia 6:2).

8. KWA KUWA UFALME NI WAKO, na Nguvu na Utukufu

Hii ni hatua ya mwisho ya kumtukuza Mungu na kumwadhimisha, na kumshukuru..hapa mtu anaweza kupaza Sauti yake kama Daudi kwa nyimbo au kwa kinywa na kusema  Bwana ni mwenye Nguvu, asikiaye maombi , ajibuye maombi..Bwana ni mwenye haki, Bwana ni mwenye enzi na mamlaka..utukufu una yeye milele na milele.

Tukisali kwa namna hiyo, au kwa ufunuo huo basi tutakuwa tumeomba sawa sawa na mapenzi yake.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kuna tofauti gani kati ya SALA na DUA?

SALA YA UPONYAJI/MAOMBI YA UPONYAJI.

NITAJUAJE KAMA MAOMBI YANGU YAMEFIKA (YAMEJITOSHELEZA)?.

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Stellah Gideon
Stellah Gideon
1 year ago

Be blessed.