WANAWAKE WAOMBOLEZAJI

WANAWAKE WAOMBOLEZAJI

(Masomo maalumu kwa wanawake)

Wanawake waombolezaji maana yake nini?, Na je hadi leo wapo?, au wanapaswa kuwepo?.

Kabla ya kuingia ndani kuhusiana na wanawake waombolezaji, hebu tujue kwanza maana ya neno kuomboleza.

Kuomboleza maana yake “ni kuingia katika sikitiko kuu, kutokana na tukio ambalo limetokea au litakalotokea!”.. Sikitiko hili linaambatana na Toba, na Majuto.

Kwamfano mtu anayeomboleza kutokana na msiba alioupata anakuwa katika hali ya huzuni kuu, akitafakari kwa undani tukio lililotokea huku akiomba rehema na msamaha kwa Mungu, na huku akiomba Mungu amponye majeraha yake na pia akiomba jambo kama hilo lisijirudie tena, (huyo ndio mtu anayeomboleza kibiblia kutokana na tukio lililotokea).Na mtu anayeomboleza kwajili ya tukio lijalo pia anakuwa katika hali hiyohiyo.

Hebu tuangalie mifano ya watu walioomboleza kabla ya tukio Fulani/msiba Fulani kutokea na watu walioomboleza baada ya Tukio kutokea.

1.KABLA YA TUKIO.

Mfano wa watu waolioomboleza kabla ya Msiba kutokea ni wana wa Israeli kipindi cha Malkia Esta, wakati ambapo waraka wa kuuawa wayahudi uliposomwa katika majimbo yote ya Mfalme Ahasuero, ambapo uliasisiwa na Hamani, aliyekuwa adui wa wayahudi.

Lakini tunasoma mara baada tu ya waraka ule kutolewa, Wayahudi wote wakiongozwa na Mordekai walifunga, kwa kulia na kuomboleza.

Esta 4:1 “Basi Mordeikai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu.

 2 Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme hali amevaa magunia. 

3 Na katika kila jimbo, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, PALIKUWAKO MSIBA MKUU KWA WAYAHUDI, NA KUFUNGA, NA KULIA, NA KUOMBOLEZA; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu”

Na matokeo ya maombolezo haya ni USHINDI KWA WAYAHUDI, na Mauti kwa maadui zao.

2. BAADA YA TUKIO.

Mfano wa maombolezo ambayo yalifanyika baada ya tukio Fulani/msiba Fulani kutokea ni yale ya NABII YEREMIA.

Baada ya wana wa Israeli, kuuawa kikatili na Mfalme Nebukadreza na baadhi yao kuchukuliwa mateka mpaka Babeli, tukio hilo lilikuwa ni tukio baya ambalo halikuwahi kutokea kama hilo katika Israeli, kwani wanawake wajawazito walipasuliwa matumbo yao, na vijana na wazee walichichwa kikatili pale Yerusalemu, na zaidi sana kundi dogo lililosalia lilipelekwa utumwani kwa aibu, kwani walikuwa uchi kabisa na wengine nusu uchi. Na wachache sana ambao walikuwa ni maskini na walemavu ndio waliobakishwa Israeli ili wayatunze mashamba.

Sasa miongoni mwa waliobaki alikuwa ni Yeremia, yeye hakuwa maskini wala mlemavu, lakini Mungu alimlinda na maangamizi hayo kwasababu alikuwa anamcha yeye,  Kwasababu hiyo basi YEREMIA, baada ya kulishuhudia tukio hilo, alilia kwa machozi mengi na kuomboleza siku nyingi.. (na ndio akaandika maombolezo yake katika kitabu, ambacho ndio sisi leo tunakisoma kama kitabu cha Maombolezo).

Maombolezo 3:47  “Hofu imetujilia na shimo, Ukiwa na uharibifu. 

48 Jicho langu lachuruzika mito ya maji Kwa ajili ya uvunjifu wa binti ya watu wangu. 

49 Jicho langu latoka machozi lisikome, Wala haliachi; 

50 Hata Bwana atakapoangalia Na kutazama toka mbinguni. 

51 Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu, Kwa sababu ya binti zote za mji wangu.

 52 Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege”

Sasa ni Maombolezo gani kati ya hayo mawili, Mungu anayotaka sisi tuyafanye??

Jibu ni “Maombolezo ya kabla ya tukio”. Mungu hataki tuomboleze baada ya tukio, bali anataka tuomboleze kabla ya tukio..

Leo hii dunia tayari imeshatamkiwa hukumu na Mungu, huenda Taifa lako limeshatamkiwa hukumu, huenda familia yako imeshatamkiwa hukumu na Mungu, huenda Nyumba yako imeshaandikiwa hukumu na Mungu, kutokana na mambo yanayoendelea humo yasiyompendeza yeye.

Huenda Kanisa lako limeshaandikiwa hukumu, washirika wenzako wameshaandikiwa hukumu, mchungaji wako kashaandikiwa na kashakusudiwa kuadhibiwa na Mungu hapa hapa duniani kabla hata hajaondoka..Hivyo kabla hukumu hizo hazitimia, Bwana Mungu anataka tuwe na jicho la kuona na KULIA NA KUOMBOLEZA KWA TOBA NA MSAMAHA, NA KWA KUTAKA REHEMA kwa Mungu ili Mabaya haya yasitokee, Kama Akina Esta, Mordekai na Wayahudi wote walivyofanya kipindi cha Hamani.

Sasa pamoja na hayo, lipo kundi moja la Watu, ambalo  ni rahisi kuzama katika Maombolezo na hata kuvuta rehema za Mungu, na fadhili za Mungu upesi.

Na kundi hilo si lingine zaidi ya kundi la Wanawake.. Mwanamke anapoomba kwa hisia (iliyo ya kiMungu), basi ni rahisi maombi yake kufika kwa Baba mbinguni zaidi ya wanaume.. Hivyo biblia imewataja wanawake kama viungo vifaavyo kusimama katika hii nafasi ya kuomboleza.

Hebu tulithibitishe hili kimaandiko…

Yeremia 9:17 “Bwana wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje; 

18 na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji. 

19 Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa! tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao yetu”. 

Umeona Nafasi yako wewe mwanamke?..Wewe umewekwa na Mungu katika hilo kanisa ili ulie na kuomboleza kwaajili ya Uovu, ili Bwana akumbuke rehema, wewe umewekwa katika hilo Taifa ili ulie na kuomboleza Bwana aachilie neema na rehema.. Hiyo ndio nafasi yako ambapo usipoitumia siku ile utakwenda kuulizwa!!.

Biblia haijashindwa kuwaweka hapo wanaume, na kusema wao ndio waomboleze!!.. lakini imewaweka pembeni na kuwapa vipaumbele wanawake!..Sasa sio kwamba ina upendeleo haina upendeleo..bali ni kutokana na jinsi wanawake walivyoumbwa!.. Kadhalika mwanamke usikimbilie kuwa mchungaji, hiyo ni nafasi ya wanaume..(kasome 1Wakorintho 14:34). Kwahiyo biblia imetoa majukumu kwa kila jinsia..

Je umewahi kulia na kuomboleza kwaajili ya Nyumba yako, au kanisa lako au Taifa lako? Kama bado halafu wewe ni mwanamke unayesema umeokoka, basi badilika leo.. Litii Neno na lifuate hilo, usijiamulie utumishi au usijitwike wito ambao hujawekewa juu yako.. kaa katika nafasi yako hiyo na Mungu atakutumia.

Na baada ya kujua nafasi yako hii basi wafundishe na wanawake wengine kuwa kama wewe (mwombolezaji)..ndivyo biblia inavyoelekeza..

Yeremia 9:20 “Lakini lisikieni neno la Bwana, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani yake kulia.

  21 Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu”.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TUKIO LA MUSA NA ELIYA KUMTOKEA BWANA, LIMEBEBA UJUMBE GANI?

NAFASI YAKO NI IPI KATIKA MWILI WA KRISTO?

MAOMBOLEZO YA HADADRIMONI.

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

Sadaka ya Moyo ipoje? (Walawi 22:21).

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Getruda pius
Getruda pius
6 months ago

Barikiwa sana mtumishi wa BWANA Mungu aliye hai, nimeipenda sana nimejifunza kitu kikubwa hapo 🙏🙏🙏