NAFASI YAKO NI IPI KATIKA MWILI WA KRISTO?

NAFASI YAKO NI IPI KATIKA MWILI WA KRISTO?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, lihimidiwe milele.

Kwanini leo hii tunaona kama vile utukufu wa Mungu umepungua makanisani?..Tunamwita Yesu aponye lakini haponyi, tunamwita atende miujiza lakini hatendi, tunamwita afungue watu lakini hawafungui kikamilifu? Ni kwanini?

Ni kwasababu yeye mwenyewe ni mgonjwa, yeye mwenyewe ni mlemavu, ana chechemea, hana masikio, yeye mwenyewe ni kipofu, yeye mwenyewe ana kisukari, amepooza, ana saratani, na homa ya ini, sasa atawezaje kuwaganga wengine? Angali yeye mwenyewe ni muathirika wa hayo mambo?

Tunashindwa kufahamu sisi tuliookoka ni viungo vya Kristo, na kila mmoja anayo nafasi ya kuujengwa mwili huo mpaka ukamilike, ili yeye kama kichwa atakaposhuka juu ya mwili wake, awe na uwezo na nguvu za kutosha kutembea na kutimiza wajibu wake, wa kuwahudumia na kuwafungua watu wake, kama alivyofanya alipokuwa hapa duniani.

Lakini changamoto tuliyonayo, ni pale tunapodhani kuwa wote, tunaweza kuwa miguu, wote tunaweza kuwa macho, wote tunaweza kuwa midomo,..Hivyo tunaelekeza bidii zetu zote, kuwa kiungo kimojapo ya hivyo.. Na hiyo yote ni kwasababu hivyo ndivyo vinavyoonekana vina utukufu kuliko vingine, kisa tu vipo kwa nje.

Lakini tunasahau kuwa mwili, hauundwi kwa viungo vya nje tu, bali pia na vile vya ndani. Na zaidi sana vile vya ndani ndio vinaumuhimu sana, na ndio maana vimefichwa na kufunikwa na vya nje, kwasababu hivyo vikipata hitilafu tu..hata hivi vya nje haviwezi kufanya lolote.

Kwamfano moyo, ukifeli, jiulize macho yako, mikono yako, miguu yako, itakuwa na kazi gani?.. Uti wa mgongo ukifeli, mwili wote utapooza, huo mkono utawezaje kusogea?..figo zimefeli, ni nini utakachokuwa unasubiri kama sio kifo..Lakini mguu mmoja ukifeli, mwili bado unaweza kuendelea kuishi..

Biblia inasema..

1Wakorintho 12:22 “Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi.

23 Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana”.

Si kila mtu, atakuwa mchungaji katika kanisa ndio awe kiungo bora cha Kristo, si kila mtu atakuwa mwalimu, si kila mtu atakuwa nabii, au shemasi au mwimbaji..ikiwa wewe unajiona kama huwezi kusimama katika mojawapo ya nafasi hizo, haimaanishi kuwa wewe sio kiungo, suluhisho sio kujitenga na mwili wa kristo..huwenda wewe ni moyo, au figo au ini, au uti wa mgongo.. embu angalia ni nini unaweza kukifanya ukusanyikapo na wenzako..ni nini unaweza kuchangia katika mwili huo uliowekwa na Bwana..

kama ni kufuatilia na kusimamia ratiba na vipindi vyote vya kanisani, kama ni kuhamasisha na kuwaunganisha washirika, kama ni kuchangia kwa bidii kwa mali zako, kama ni kuongoza watoto, kama ni ulinzi, kama ni usafi, kama ni kuongoza maombi na mifungo..n.k. uwapo mbali au uwapo karibu. Hakikisha unafanya kwa bidii zote na sio kwa ulegevu..

Wafilipi 4:8 “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.

9 Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, YATENDENI HAYO; NA MUNGU WA AMANI ATAKUWA PAMOJA NANYI”.

Lakini usikae tu, mwenyewe, na kuwa mtu wa kwenda tu kanisani na kurudi nyumbani, kama mtembeleaji tu..miaka nenda miaka rudi, utawalaumu viongozi, utalilaumu kanisani, kumbe shida ni wewe ambaye hujasimama katika nafasi yako.  Kama ‘mapafu’ umejitenga kivyao,unaliangalia kanisa la Kristo likipumulia mirija.

Tubadilike, sote tujiwajibishe, ili Kristo ashushe utukufu wake kama kanisa la mwanzo. Hivyo ili Kristo atukuzwe, na aweze kutenda kazi yake, sote kwa pamoja tuje katika nia moja ya Kristo, kisha kila mtu asimame katika nafasi yake, Kristo akamilike, ndipo tuone matendo yake makuu, akiyatenda kama alivyofanya katika kanisa la mwanzo.

Bwana awe na nasi. Bwana awe na kanisa lake takatifu.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Matulizo ya mapenzi ni nini? (Wafilipi 2:1).

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

Maongeo ni nini?(Wakolosai 2:19)

USHAURI KWA MWANAMKE WA KIKRISTO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments