NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe,  Nakukaribisha katika kujifunza elimu ya ufalme wa mbinguni. Kumbuka kila habari katika biblia inayo ujumbe fulani nyuma yake. Hakuna habari isiyo na maana.

Leo kwa ufupi tutatazama habari ya mwamuzi mmoja aliyeitwa, Ehudi. Sasa wakati tunakwenda kutafakari habari zake naomba ufahamu kuwa Lengo la somo hili, ni kuamsha ile karama iliyo ndani yako ili  itende kazi..

Kuna wakati wana wa Israeli walimkosea sana Mungu, hivyo Mungu akawaweka chini mkono wa adui yao aliyeitwa Elgoni mfalme wa Moabu kwa muda wa miaka 18. Lakini walipomlilia Mungu, Mungu akawasikia  na kuwatumia huyu mwamuzi aliyeitwa Ehudi.

Biblia inatuambia Ehudi alikuwa ni mtu anayetumia SHOTO. Sasa biblia mpaka iandike habari kama hizo za mkono mtu anaotumia, inamaana kuwa lipo jambo la kujifunza. Ukisoma habari yenyewe pale utaona walimchukua huyu na kumpeleka kwa huyo mfalme wa Moabu ili awasilishe tunu zao ambazo walikuwa wanazipeleka kwa huyo mfalme mara kwa mara.

Sasa siku alipoenda, aliundaa upanga mrefu, kisha akauficha kwenye paja lake la kulia. Na alipofika mbele ya askari wake akazitoa zawadi hizo mbele yao..Lakini alipomalizia, hakuondoka bali aliomba aongee na mfalme faragha, kana kwamba kuna ujumbe amepewa na wakuu wa Israeli utokao kwa Mungu, amwambie, hivyo haipasi kila mtu asikie.

Ndipo mfalme akamchukua peke yake katika ukumbi wake, akawaondoa askari wake, akafunga milango. Sasa biblia inatuambia huyu Elgoni alikuwa ni mtu mkubwa sana, mwenye mraba minne, kiasi kwamba ili kumdondosha mtu kama huyo ilihitaji watu wengi, na sio mmoja tena wenye nguvu.

Lakini Mungu alilijua hilo,  na ndio maana akawatumia mtu kama Ehudi anayetumia shoto na si kilia ili kumdondosha huyo.

Kama tunavyosoma habari, aliutoa ule upanga wake, na kwa nguvu aliuzamisha kwenye Tumbo lake, ambalo pengine lilikuwa limefunikwa kwa nguo nzito, lakini upanga  ule ulipita kwa jinsi zile nguvu zilivyokuwa nyingi, kisha ukaenda kushikamana na mafuta ya tumboni na kutokea upande wa pili.. Lakini ni heri tu ungeingia upanga peke yake, biblia inasema, mpaka ule upini wa upanga ulizama ndani kabisa, usionekane. Jambo ambalo si rahisi hata kidogo kwa mtu kuuzamisha upini kwenye tumbo. Inahitaji presha kubwa sana ya kusukuma, ambayo kwa nguvu za kawaida za kibinadamu haiwezekani.

Waamuzi 3:21 “Ehudi akaunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kuume, akamtia tumboni mwake;

22 hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma”.

Unaona, ukisoma tena, utaona tena hata katika vita zamani, wana wa Israeli waliwachagua mashujaa wanaotumia shoto, kwasababu aliweka uwezo mkubwa sana wa shabaha ndani yao.

Waamuzi 20:15 “Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, watu waume ishirini na sita elfu waliotumia upanga, zaidi ya hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba.

16 Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose”.

Tukiyafahamu haya turudi sasa katika kiini cha ujumbe wetu wa leo, kwasababu lengo sio kueleza umahiri wa watu wanaotumia shoto au kulia, hapana. Bali ni kutufundisha sisi mambo ya rohoni yahusuyo wokovu wetu.

Kumbuka mkono huu wa kushoto huwa haupewi heshima, wala hauwezi kutumiwa sehemu zote, hauwezi kutumia kulia chakula, au kumpia mtu mkono, n.k. Lakini uwezo na nguvu Mungu alioupa unazidi hata ule wa kulia.

Hiyo ni kuonyesha pia, Mwili wa Kristo unao viungo vingi, vingine Mungu amevikusidia kabisa vipewe  heshima, lakini vingine Mungu amevikusudia pia visiwe na heshima yoyote, lakini vimepewa nguvu na ufasaha wa hali ya juu.

1Wakorintho 12:23 “Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana.

24 Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa;

25 ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe”

Umeona? Ni lazima tufahamu si kila mtu atakuwa mchungaji, si kila mtu atakuwa mtume, si kila mtu atakuwa nabii, si kila mtu atakuwa mwalimu, zipo karama nyingi nzito na zenye nguvu  ambazo watu wanazo lakini wamezizimisha ndani yao kwasababu  wanachofikiria tu ni kuwa pale watakapokuwa wakristo basi ni kwenda kuwa wachungaji, au mitume au watu fulani maarufu wanaojulikana.

Na ndio maana karama nyingi za kipekee kama za miujiza, uponyaji, karama za ufasiri wa lugha, karama za faraja, za kukirimu n.k. hazionekani au zimekufa kabisa katika kanisa, kwasababu hatuziangalii hizo sote tunataka tukawe mitume, wachungaji na manabii.

Ukiona lipo jambo linaamka ndani yako kwa ajili ya Mungu, ambalo pengine lipo tofauti na wengine na unaona kabisa  linakupa furaha kulifanya, usilizimishe, lifanye hilo kwa bidii kwasababu huo ndio mwanzo wa kuijua karama yako. Na Mungu ameiweka hiyo ndani yako ili ilisaidie kanisa kwa sehemu kubwa sana. Fanya kile kitu kinachougua ndani yako sana.. Kama ni kumtolea Mungu, basi mtolee sana, kama ni kufundisha basi fundisha sana, kama ni kufanya uinjilisti ufanye huo kwa bidii, kama Mungu anakuonyesha mambo ya rohoni, yachochee hayo ili yakawe faida kwa mwili wote wa Kristo.

Kumbuka hakuna kiungo kisichokuwa na kazi  kanisani, maadamu umeokoka na umejazwa Roho, umuhimu wake ni lazima utaonekana tu. Lakini kazi ya kiungo ni ngumu kuonekana kama kitakuwa chenyewe chenyewe, hivyo kaa na watakatifu wengine, ndipo hapo utajua kwa urahisi karama yako ni ipi. Karama nyingine haziwezi kufanya kazi kama zitakaa zenyewe nyumbani,

Jitahidi ujue nafasi yako ni ipi ili umtumikie Mungu katika hiyo. Kwasababu kila mmoja wetu anatarajiwa na Bwana amzalie matunda.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

NITAIFAHAMU VIPI KARAMA YANGU?.

NINI TOFAUTI KATI YA KARAMA, UTENDAJI KAZI NA HUDUMA.

Vyombo vya uzuri ni vipi vinavyotajwa katika biblia?

USINIE MAKUU.

Neno “Via” linamaanisha nini katika biblia?

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

Mchokoo ni nini katika maandiko? (Matendo 26:14)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments