Vyombo vya uzuri ni vipi vinavyotajwa katika biblia?

Vyombo vya uzuri ni vipi vinavyotajwa katika biblia?

SWALI: Shalom mpendwa katika Bwana , swali langu lipo katika kutoka 33:5 BWANA alipomwambia Musa vueni “vyombo vyenu vya uzuri” ili nipate kujua nitakalowatenda . Nataka kujua aliposema hivyo alikuwa na maana gani?


JIBU: Tusome habari yenyewe tokea mstari wa kwanza, lipo jambo zaidi ya hilo la kujifunza;

Kutoka 33:1 “Bwana akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii;

2 nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi;

3 waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia.

4 Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza WALA HAPANA MTU ALIYEVAA VYOMBO VYAKE VYA UZURI.

5 Bwana akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa VUENI VYOMBO VYENU VYA UZURI ili nipate kujua nitakalowatenda.

6 Basi wana wa Israeli wakavua vyombo vyao vyote vya uzuri, tangu mlima wa Horebu na mbele”.

Vyombo vya uzuri,ni  mapambo ya aina yote, ikiwemo mikufu, pete, hereni, vikuu, nguo za thamani n.k.. Wana wa Israeli baada ya kumkosea sana Mungu, kwa kutengeneza ndama  wa dhahabu, Mungu alikusudia kuanzia huo wakati kuwaacha  moja kwa moja asitembee nao tena, kinyume chake awape malaika wake wawe wanaenda badala yake, lakini sio yeye tena. Lakini wana wa Israeli waliposikia hivyo wakamlilia sana Mungu wasiachwe, ndipo watu wote wakavua vyombo vyao vya uzuri, yaani vitu vyao vya thamani, wakavaa nguo za maombolezo, wakamlilia sana Mungu na kutubu kwa uchungu mwingi ili tu wasiachwe.

Hiyo ilikuwa ni desturi ya Israeli tangu zamani, na hata mataifa mengine, inapofikia wakati wa kuomba toba, au kuomboleza, ni sharti uweke kando mavazi ya thamani, na mapambo yako, uvae nguo za magunia uomboleze.

Lakini ni nini, tunaweza kujifunza katika habari hiyo?

Wana wa Israeli walitamani waangukie mikononi mwa Mungu kuliko  mikononi mwa malaika zake, Kwasababu walimjua Mungu ndio uzima wao, licha ya kuwa ni mwenye ghadhabu nyingi, lakini pia bado ni mwenye rehema nyingi. Ni sawa na kilichomtokea Daudi kipindi kile, alipoambiwa na Mungu achague adhabu mojawapo kati ya zile tatu, yaani njaa miaka mitatu, au akimbizwe na adui zake miezi mitatu, au Tauni iletwe siku tatu juu ya nchi,. Daudi akachagua kuangukia mikononi mwa Mungu, kwa ile Tauni siku ya tatu, kwasababu alijua, mioyo ya wanadamu sio kama wa Mungu, kuliko kukimbizwa na maadui zake, ni heri aadhibiwe na Mungu..Na kweli japokuwa Mungu aliwaua maelfu ya watu, lakini baadaye aliuzuia mkono wake, akarehemu.

Je! Na wewe umechagua kuangukia mikononi mwa nani? Mungu, au mwanadamu?.

Daudi alisema..

Zaburi 118:18 “Bwana ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife”.

Inasikitisha kuona kwamba watu wanakataa kuongozwa na Mungu, wanataka waongozwe na wanadamu, wanachukia kuadhibiwa na Mungu, wanataka wakaadhibiwe na wanadamu. Wana wa Israeli waliomboleza kusikia tu wanakwenda kuongozwa na malaika,ambao hata hawana shida yoyote, lakini waliona bado hakuna kiongozi mzuri na bora zaidi ya Bwana.

Ndugu yangu huna kimbilio lingine lililo salama kwako, zaidi ya Mungu.. Si hata malaika wake, si mwanadamu, au kiumbe kingine chochote, au kitu kingine chochote. Mkimbilie Bwana leo hii akuokoe, na ayasafishe maisha yako. Usizifiche dhambi zako mbele za Mungu, kwa hofu ya kwamba atayakemea matendo yako, ni kweli lazima ayakemee, na wakati mwingine akuadhibu, lakini adhabu zake ni dawa, na sio mauti. Hivyo chagua kuangukia mikononi mwake, uwe salama.

Ufunuo 3:19 “Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu”.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

AINA TATU ZA WAKRISTO.

Swali: Je Ni sahihi kwa Mkristo kupeleka kesi mahakamani?

Je mtu anayeua anabeba dhambi zote za yule aliyemuua?

NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments