BWANA UNIJULISHE MWISHO WANGU.

BWANA UNIJULISHE MWISHO WANGU.

Karibu tujifunze biblia..

Daudi anasema..

Zaburi 39:4 “Bwana, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani……..”

Hapa si kwamba Daudi anataka aijue siku ya kufa kwake!, Hapana!, Mungu hajawahi kumwahidia mwanadamu hayo maarifa..(Hakuna maombi ya mtu kufunuliwa siku yake ya kufa).  Bali hapo Daudi anaomba Mungu ampe KUZIJUA SIKU ZAKE DUNIANI KWAMBA SI NYINGI, Kwamba siku za mwanadamu ni kama maua! Si wa kudumu (Zaburi 103:15).

Hivyo Daudi alijua Mungu akimpa moyo wa kuelewa kuwa “Yeye ni kama mpitaji tu hapa duniani, na siku zake si nyingi”.. basi atakuwa mnyenyekevu zaidi, na ataishi maisha ya kumtafuta Mungu, kumcha Mungu na kuishi kwa hekima duniani..

Zaburi 90:12 “Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima”.

Na sio tu yeye aliyepaswa kuomba maombi kama haya, bali hata sisi pia watu wa siku za Mwisho, ni lazima tumwombe Mungu atujulishe siku zetu! (Yaani atupe mioyo ya hekima kujua kuwa sisi ni wapitaji tu, na siku zetu za kuishi si nyingi).

Faida ya kuomba Moyo huu kutoka kwa Mungu, ni kwamba tutakuwa watu wa kutazama maisha yajayo zaidi kuliko maisha haya ya hapa duniani ya kitambo!.. Kwasababu ndani ya akili zetu tutajua kuwa siku zetu si nyingi!..kwamba siku yoyote safari ya maisha yetu itafikia mwisho.

Watu wengi wenye huu moyo, utaona ndio watu wenye mioyo ya kumtafuta Mungu kwa kujikana nafsi kwelikweli…ndio watu wenye mioyo ya kusaidia wengine, ndio watu wenye mioyo ya kuwahubiria wengine mwisho wa maisha haya.

Na watu kama hawa, hata kama wakiambiwa kuwa watapewa miaka elfu moja ya kuishi duniani, bado tu!, watajiona kuwa siku zao ni chache, kwasababu tayari ndani yao wamepewa mioyo ya “kuzihesabu siku zao na kujijua kuwa wao si kitu, ni kama maua tu, yaliyopo leo na kesho kutupwa kwenye tanuru” hivyo maisha yao yatakuwa ni yale yale siku zote ya kutafuta kutengeneza maisha yajayo ya umilele.

Shetani hapendi watu wawe na moyo huu, anataka watu wawe na moyo wa kufikiri kwamba wataishi milele katika hii dunia, hataki watu wajue kwamba siku yoyote safari ya maisha yao itafikia ukingoni, kwasababu anajua watu wakilijua hilo, basi watatengeneza maisha yao hapa kwaajili ya huko waendako, na hivyo atawapoteza wengi. Na yeye (shetani) hataki kumpoteza mtu hata mmoja, anataka wote waende katika ziwa la moto kama yeye!!.

Kwahiyo kila siku ni muhimu sana kuomba Bwana atupe huu moyo.. “Atujulishe miisho yetu, na siku zetu za kuishi” ili tufahamu kuwa “sisi ni wapitaji tu”.

Moyo huu utaupata kwa kufanya mambo yafuatayo matatu (3)

1.Kwa kuomba

Majibu ya mambo yote tunayapata katika maombi, kama vile Sulemani alivyoomba kwa Mungu apewe moyo wa hekima na Mungu akamsikia, vile vile pia Moyo wa kujua kuwa wewe ni mpitaji tu, unatoka kwa Bwana, ndio maana hata hapo Daudi anaonekana kama anaomba.. “Bwana nijulishe”..Na wewe siku zote sema “Bwana nijulishe”

2. Kwa kutafakari matukio ya vifo yanayotokea.

Unapotenga muda wa kutafakari matukio ya Ajali yanayotokea, au unapotazama wagonjwa mahututi, au unapokwenda kwenye nyumba za misiba..sehemu hizo ni sehemu ambazo Mungu anaitengeneza mioyo ya wengi.. Hivyo na wewe huna budi kuhudhuria misiba, au kufuatilia matukio (Wengi hawapendi kufuatilia haya), kwasababu hawataki kuumia moyo, lakini ndani ya mioyo yao wana viburi vya maisha, wanajiona kama wao wataishi milele.. Biblia inatufundisha pia tuhudhurie sehemu za Misiba, sio kwenye karamu tu, ili tukajifunze huko..

Mhubiri 7:2 “Heri kuiendea nyumba ya matanga, Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake. 

3 Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo”.

3. Kwa kusoma Neno.

Unaposoma Biblia, huko ndiko utakapopata Maarifa kamili ya Neno la Mungu, na maneno ya kuunyenyekeza moyo wako, biblia ndio kioo kamili cha kujijua wewe ni nani?.. ukitaka kujijua wewe ni mtu wa namna gani, basi soma Biblia.

Bwana atubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?

KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

Je mwanamke anaruhusiwa kupanda madhabahuni akiwa katika siku zake?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments