KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

Matendo 13:21 “ Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini.

22 Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, MTU ANAYEUPENDEZA MOYO WANGU, ATAKAYEFANYA MAPENZI YANGU YOTE”.

Japo Daudi hakuwa mkamilifu kwa viwango kama vya watumishi wengine wa Mungu waliomtangulia au waliomfuata mfano wa Musa, Samweli, Eliya au Danieli, lakini biblia inamshuhudia kuwa ni mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu.(Daudi Aliupendeza moyo wa Mungu sana)..

Je! Alimpendezaje Mungu? 

Embu tuangalie mambo baadhi yaliyomfanya Daudi awe vile, naamini yanaweza kutusaidia na sisi katika safari yetu ya kutafuta kumpendeza Mungu.

Jambo la kwanza: ni,Daudi alimwamini Mungu kwa moyo wake wote: Hakujali ukubwa wa tatizo lilolokuwa mbele yake, kwa jinsi tatizo lilivyoonekana kuwa kubwa ndivyo alivyomfanya Mungu wake kuwa mkubwa Zaidi ya hilo tatizo na hiyo ilimfanya asiogope chochote..

Anasema katika..

Zaburi 27:1 ‘Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?’

Wakati alipokuwa anapambana na Goliathi hakuogopa ukubwa wake na vitisho vyake ijapokuwa alikuwa hana silaha yoyote mkononi mwake lakini Daudi hakuogopa badala yake alimwambia maneno haya

1Samweli 17: 45 “Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.

46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.

47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.

Nasi tujiulize, majaribu makubwa yanaposimama mbele yetu je ndio tunamkimbia Mungu au ndio tunamwamini Mungu, na kumuacha ili aonyeshe yeye uweza wake?. Kumbuka Daudi hakufanya hivyo sio tu kwa Goliathi bali katika matatizo mengi yote aliyowahi kukumbana nayo alisema pia nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti sitaogopa mabaya kwa maana Bwana yupo pamoja nami, Gongo lake na limbo yake vyanifariji.(Zaburi 23).

Jambo la pili: ni kuwa Daudi aliipenda sheria ya Mungu kuliko kitu kingine chochote: Anasema..

Zaburi 119:47 ‘Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda.

48 Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako’.

Soma tena..

Zaburi 119:140 ‘Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda”.

Ukisoma sehemu nyingi katika Zaburi utaona Daudi akionyesha Upendo wake katika Neno la Mungu, na hiyo ilimfanya awe analitafakari sana, sio kulisoma tu kama gazeti hapana, bali alikuwa analitafakari sana mchana na usiku..

Na sisi je! Tunao moyo kama huo wa kulipenda Neno la Mungu, tunapoambiwa uzinzi ni dhambi, tunafurahia kusikia hivyo?, tunapoambiwa vimini ni dhambi tunafurahia kusikia hivyo?, tunapoambiwa usengenyaji ni dhambi Je tunazingatia kujirekebisha je, tunapoambiwa ulevi na uvutaji wa sigara ni dhambi tunasikiliza? tunalitafakari hilo usiku na mchanga..Kama ndio hivyo basi tujue kuwa tupo katika njia ya kuelekea kumpendeza Mungu..Daudi anasema hivi:

Zaburi ZABURI 1:1 “Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.

2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, NA SHERIA YAKE HUITAFAKARI MCHANA NA USIKU

3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.”.

Na pia alisema…

Zaburi 119:140 ‘Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda’

Tatu: Daudi alikuwa ni mtu aliyekubali na kuyakiri makosa yake haraka sana, na kutubu. Alipozini na mke wa Uria, baada ya kuletewa habari hizo na nabii Nathani ukisoma 2 Samweli 12: 13 utaona hilo, saa ile ile Daudi alikiri kuwa kweli ametenda dhambi…Lakini sisi ni mara ngapi tunamficha Mungu dhambi zetu, hata kama uthibitisho wote unaonekana, tutajaribu kutengeneza mazingira na kusema ni kwasababu ya hiki au kile ndio maana nimetenda hivi au vile kama tu vile walivyofanya Adam na Hawa pale bustanini..

Ukisoma Zaburi 51, utaona jinsi Daudi alivyoungama dhambi zake zote..Vivyo hivyo na sisi Mungu atusaidie tuwe na moyo huo huo, wa kukiri makosa yetu na hivyo kutubu, kwa kumaanisha kabisa kuacha.

Nne: Daudi alikuwa ni mtu wa kuustaajibu uweza wa Mungu, na hivyo hakuona aibu kuutangaza uweza huo kwa kila mtu:

Zaburi 119: 46 ‘Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu’.

Daudi alikuwa yupo radhi kumtukuza Mungu hadi nguo zinamtoka bila kujali yeye ni mfalme, (Daudi alicheza mpaka nguo zikaanguka)alimtukuza Mungu dunia nzima ilijua kuwa yeye kweli ni mtumishi wa Yehova. Ukisoma Zaburi sehemu kubwa utaona Daudi anavyoibiri kazi ya Mungu na uweza wake na utukufu wake duniani kote..

Na sisi Je! Tunaounea aibu ushuhuda wa Yesu Kristo?

Mtume Paulo aliandika katika Warumi 1:16 ‘Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia’.

Hivyo na sisi Tunapaswa kuitangaza injili kwa nguvu zetu zote Mungu alizotupa, ili na sisi tumpendeze Mungu.

Bwana atusaidie sote katika hayo. Naamini tutachukua hatua nyingine katika kuyarekebisha hayo machache, Mungu akubariki sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine.


Mada Nyinginezo:

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

Kwanini Mungu hakumuua Nyoka, akamwacha Hawa ajaribiwe katika bustani ya Edeni?

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

TUNAMHITAJI SANA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUYAELEWA MAANDIKO.

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
WILLIAMU PHILIPO MANG'UNDA
WILLIAMU PHILIPO MANG'UNDA
1 year ago

Nimebarikiwa sana kwa somo hili

Isaya Kemore
Isaya Kemore
1 year ago

Amina, ubarikiwe sana.