TOFAUTI KATI YA SHERIA YA ROHO WA UZIMA NA SHERIA YA DHAMBI NA MAUTI!

TOFAUTI KATI YA SHERIA YA ROHO WA UZIMA NA SHERIA YA DHAMBI NA MAUTI!

Shalom! Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze maandiko, Katika kitabu cha Warumi Mlango wa 7, tunaona biblia imetaja kuwepo kwa vitu viwili, ambapo cha kwanza ni SHERIA YA DHAMBI NA MAUTI, na cha pili ni SHERIA YA ROHO WA UZIMA Hizi ni sheria kuu mbili zinazofanya kazi ndani ya mtu. Leo tutazitazama hizi sheria ni zipi, na ni jinsi gani zinafanya kazi. Naomba usome taratibu, ukisoma haraka hutaelewa chochote!

Sasa kabla ya kuingia kuzitazama hizi sheria mbili hebu kwanza tujifunze nini maana ya sheria?..

Sheria ni mfumo au utaratibu uliowekwa na jamii Fulani au mtu Fulani ufuatwe bila shuruti, kwamfano jua kuchomoza mashariki na kuzama magharibi hiyo ni sheria iliyowekewa jua, ni lazima litii hiyo sheria pasipo shuruti, kadhalika maji ya mvua kutoka juu kuja chini hiyo ni sheria iliyowekewa, ni lazima yatii, haiwezekani siku moja mvua ikanyesha kutoka chini kwenda juu…kadhalika giza kukimbia mwanga hiyo ni sheria iliyowekewa giza, haiwezekani hata siku moja giza likazidi mwanga kwa nguvu….n.k, Sasa katika maandiko pia zipo sheria hizi mbili zinazotenda kazi katikati ya wanadamu..

1)SHERIA YA DHAMBI NA MAUTI.

Hii ni sheria ya kwanza inayotenda kazi ndani ya mtu. Sheria hii kama jina lake lilivyo ni sheria ya dhambi na Mauti, yaani maana yake ni kwamba sheria hii inamlazimisha mtu kutenda dhambi hata kama hataki…kama vile jua linavyotii sheria ya kulimulikia jua, hiyo litatii hata kama lingekuwa na uwezo wa kukataa lisingeweza kubatilisha hiyo sheria..Na kadhalika sheria hii ya dhambi ilianza kufanya kazi baada ya anguko pale Edeni.

Adamu na Hawa walipokula tunda sheria hii iliingia kwao na kwa Watoto wao, kwamba ni lazima utende dhambi tu hata kama hutaki, na sheria hii inatenda kazi katika viungo vya mwili….

Ndio maana utaona mtoto mdogo anapozaliwa tayari kitendo cha kuzaliwa tu, hapo hapo anaanza kutenda dhambi, utaona siku kadhaa au miezi kadhaa, anaanza kuwa na hasira zisizokuwa na sababu, kabla hajaelewa jema na anaanza kuwa na kiburi ukimwita anakataa, ukimwambia afanye kitu saa nyingine hafanyi au anasusa vitu na kuwa na chuki na vitu visivyokuwa hata na sababu…. au utaona anaanza kuwa mkatili, anaweza kuona mjusi pale akamrushia hata jiwe na kumwua kikatili, Watoto wengine utaona wana miaka 5 lakini wameshaanza kutamani uasherati.n.k…Hiyo yote hafanyi kwa kupenda! Hapana! Ni sheria ambayo tayari kashazaliwa nayo ambayo inafanya kazi katika mwili wake…Inamlazimisha yeye kufanya dhambi hata kama hapendi au hajui. Hata kama mtu moyoni mwake hapendi hicho anachokifanya atajikuta tu anarudi kukifanya tena na tena…

Mtume Paulo aliitaja sheria hii na kusema katika

Warumi 7:20

“Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.

21 Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya.

22 Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani,

23 lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.

24 Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?”

Na sheria hii mtu anazaliwa nayo na anaendelea nayo mpaka siku ile atakapozaliwa mara ya pili..na kupokea sheria mpya ya pili ambayo tutakuja kuiona mbeleni kidogo. Na kama mtu hatazaliwa mara ya pili basi sheria hii ya dhambi na mauti ataendelea nayo mpaka siku anakufa..Hakuna namna yoyote mtu wa kawaida anaweza kushindana na dhambi!! Hakuna!, Mtu yeyote hawezi kuishinda dhambi kwa nguvu zake, ni lazima atakuwa chini ya utumwa wa sheria ya dhambi…

Na kumbuka sheria hii haiitwi tu sheria ya dhambi peke yake hapana bali inaitwa sheria ya dhambi na mauti! Ikiwa na maana kuwa, ni sheria inayozaa mauti! Ya kimwili na kiroho…Kama Biblia isemavyo “Mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23)”..Na tena “roho itendayo dhambi itakufa (Ezekieli 18:4)”

Sasa mtu anayefanya punyeto, anayefanya uasherati unaojirudia rudia, anayetazama mara kwa mara picha za ngono, anayerudia rudia kutukana, anayerudia rudia kusengenya na kuchukia watu, na anayerudia rudia kuwekea watu vinyongo, na hapendi kufanya hivyo lakini anajikuta anafanya, mtu huyo yupo chini ya HII SHERIA YA DHAMBI NA MAUTI! na ANAKUWA NI MTUMWA WA DHAMBI..Na mshahara wake ni MAUTI na ZIWA LA MOTO!!..

Lakini ipo sheria ya pili ambayo ilitengenezwa na Mungu mwenyewe kuimaliza nguvu hii sheria ya dhambi na Mauti, na hiyo si nyingine Zaidi ya SHERIA YA ROHO.

2) SHERIA YA ROHO

Sheria hii ilikuja Baada ya Bwana Mungu, kuona hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kushindana na dhambi wala kuishinda dhambi kwa nguvu zake..Kwa kupitia Roho wake Mtakatifu aliileta sheria hii mpya, ambayo ilimpasa Kristo aje kufa msalabani, na kutuachia sisi kipawa cha Roho wake Mtakatifu, Roho huyu Mtakatifu kazi yake ni kuleta sheria ambayo itatufanya sisi KUTIMIZA Sheria za Mungu na amri zake pasipo kusukumwa sukumwa wala pasipo kutumia nguvu nyingi…Yaana mtu tu unajikuta unaichukia dhambi na kuipenda haki!….wakati sheria ya dhambi na mauti ni kinyume chake, yenyewe inakufanya uchukie haki na kupenda dhambi hata kama ndani ya moyo wako huipendi ile dhambi. Lakini sheria hii ya Roho inafanya kazi kinyume chake..

Inamfanya mtu kujikuta tu! Anampendeza Mungu hata kama hajahubiriwa! Inamfanya mtu anajikuta anauchukia uasherati hata kama hajahubiriwa, inamafanya mtu anajikuta anamwogopa na kumheshimu Mungu pengine Zaidi hata ya mchungaji wake..Ndio hapo unamkuta binti anavaa tu nguo za kujisitiri hata kama hajaonyeshwa andiko lolote kwenye biblia. Kwanini? Kwasababu sheria ya mpya ya Roho inafanya kazi ndani yake…na hiyo ndio maana ya kuishi kwa Roho, kuishi kwa Roho sio kuishi kwa kuona maono! Au kwa kunena kwa lugha! Au kwa kutabiri hapana bali ni kuishi katika sheria mpya ya Roho wa uzima haleluya!!

Waefeso 5: 16 “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.

17 Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.

18 Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sharia”.

Sasa jambo pekee la kufahamu lisilojulikana na wengi ni kwamba Mtu aipokeaye sheria hii mpya ya Roho wa Uzima ndani ya moyo wake, haimaanishi kwamba ile ya kwanza ya dhambi imeondolewa!! Hapana sheria ile ya dhambi na mauti bado ipo!, isipokuwa imefunikwa na sheria hii mpya! Ikiwa na maana kuwa endapo mtu huyu aliyeipokea sheria hii mpya ya Roho akizembea na kumhuzunisha Roho Mtakatifu hata kuondoka basi huyu mtu anairudia ile sheria ya kwanza ya dhambi na mauti ambayo bado ipo ndani yake! Ndio maana inahitajika umuhimu mkubwa sana wa kushika kile tulichozawadiwa.

Ndio maana utaona mtu alikuwa moto! Hata uasherati alikuwa hafanyi lakini kapoa na kuanza kuwa baridi na kurudia matapishi ya kwanza! Kuna hatari kubwa sana juu ya huyu mtu!!

Kwahiyo sheria hii mpya ya Roho kazi yake sio kuondoa sheria ile ya zamani ya dhambi bali kazi yake ni kuifunika!

Sasa swali linakuja nitaipataje sheria hii mpya ya Roho ndani ya Moyo wangu itakayonisaidia kushinda sheria hii ya dhambi?

Mtume Paulo aliendelea kusema katika…

Warumi 7:24 “Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?

25 Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.…..

Warumi 8 :1 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.

2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.

3 Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili;

4 ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho”

Umeona hapo? Dawa ya dhambi ni Kristo Yesu, kwanza kumwamini yeye, pili kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi! Wengi hawapokei msamaha wa dhambi kwasababu wanatubu tu kwa midomo na si toba halisi itokayo mioyoni mwao inayoambatana na kuacha vile walivyokuwa wanavifanya…Na cha tatu baada ya Toba, ni ubatizo sahihi, na cha mwisho ni kupokea Roho Mtakatifu…

Na baada ya kupokea Roho Mtakatifu ni kuishi kwa kutomzimisha Roho Mtakatifu(Waefeso 4:30)..hapo dhambi haitakuwa na nguvu juu yako! Hutahitaji mhubiri akuhubirie kuwa ulevi ni dhambi, hutahitaji askofu akuambie kuwa kuishi na mwanamke/mwanamume ambaye hamjaoana ni dhambi! Hutahitaji mtu akuhakikishie katika maandiko kwamba uvaaji mbaya ni dhambi na upakaji uso rangi, hamu ya kuwa mtakatifu na ya kujiepusha na uovu itakuwa inamiminika tu ndani yako…Msukumo wa kutamani uasherati wala wa kufanya punyeto na kutukana hutauona tena. Hilo Ndio agano jipya lililoletwa na Bwana wetu Yesu Kristo kwamba sheria za Mungu tuzimize ndani yetu pasipo kusukumwa sukumwa wala pasipo kuwa watumwa wa sheria..

Yeremia 31:31 “ Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.

32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.

33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”

Bwana akubariki.


Mada zinazoendana:

JE! “MAJIRA NA SHERIA” MPINGA-KRISTO ATAKAYOKUJA KUBALISHA NI KUPINDUA SIKU YA SABATO NA KUWA JUMAPILI?

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?

BIBLIA ITUAMBIA TUSALIMIANE KWA BUSU TAKATIFU. HILI BUSU NDIO LIPI?


 

Rudi Nyumbani:

 

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Cassian rogatus komba
Cassian rogatus komba
2 years ago

Sasa kila nikijaribu kuwa chini ya sheria ya roho mtakatifu nashindwa kipi nifanye