Yerusalemu ni nini?

Yerusalemu ni nini?

Yerusalemu, ni Neno la kiyahudi linalomaanisha  “Mji wa amani” au “msingi wa amani” .

Kabla ya mji huu kupata sifa tunayoifahamu sasahivi, awali ulikuwa ni mji wa wakaanani, waliojulikana kama wayebusi, kipindi ambacho wayahudi bado hawajaimiliki nchi yao.

Hivyo baada ya wana wa Israeli kuiteka nchi ya kaanani, eneo ambalo lilikuwepo huu mji, liligawanya kwa kabila la Yuda. Lakini hawa wayebusi hawakuondolewa moja kwa moja katika mji huo wa Yerusalemu, bado ukaendelea kuwa chini ya milki yao.

Mpaka baadaye, Daudi alipouvamia na kuwaondoa wayebusi. Ndipo Mji huo ukaitwa “Mji wa Daudi”.(2Samweli 5:6-10) Baadaye akalihamishia Sanduku la Mungu la agano, mpaka mji huo,  hivyo kidogo kidogo ukaanza kupokea sifa ya kuwa kiini cha dini (2Samweli 6:1-19). Daudi akaazimia kumjengea Mungu hekalu ambalo, atamwekea Mungu agano lake huko. Lakini hakuruhusiwa kwasababu ya mauaji mengi aliyoyasababisha, Mpaka mtoto wake Sulemani, alipokuja kulijenga, Hapo ndipo wana wote wa Israeli wakapafanya Yerusalemu kuwa kitovu cha kumwabudia Mungu. Na Mungu pia akapabariki na kupachagua pawe mji wake mtakatifu, kati ya miji yote, ambapo ataliweka jina lake, lijulikane kwa mataifa yote ya ulimwengu..

Japokuwa eneo la mji huu, lilibomolewa na kujengwa mara kadhaa, lakini hapo ndipo mfalme  wetu Yesu Kristo atakapokuja kutawalia dunia yote katika ule utawala wa miaka 1000 kama mfalme wa wafalme na Bwana wa Mabwana, atakaporudi mara ya pili.

Lakini biblia inatuonyesha kuwa upo mji mwingine wa kimbinguni, ambao Mungu amewaandalia watu wake,..ujulikanao kama YERUSALEMU MPYA.

Umechukua jina la Yerusalemu hii ya duniani, ili kutupa picha tuelewe vizuri utakavyokuwa.  Mji huo utashuka kutoka mbinguni kwa Mungu mwenyewe na kuja hapa duniani. Ndani ya mji huo maandiko yanasema “hakitaingia chochote kilicho kinyonge”. Isipokuwa watu maalumu sana wajulikanao kama bibi-arusi wa Kristo.. Kumbuka si kila atakayepokea uzima wa milele, atakuwa na daraja sawa na mwenzake..Uaminifu wako, na utumishi wako sasa, vinaeneleza wewe utastahili kukaa wapi utakapofika kule ng’ambo. Wapo ambao watastahili kukaa ndani ya mji, na wapo ambao watakaa nje ya mji huo mtakatifu. Japo wote watakuwa ni watakatifu.

Ndani ya huo mji ndio yatakuwa makao mapya ya Mungu milele (Ufunuo 21:3), Mambo yaliyopo huko ni mazuri biblia inasema jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia(1Wakorintho 2:9). Kwa ufupi ni kwamba kila mmoja wetu atajuta, kwanini hakujibidiisha kwa Mungu sana kwa uzuri atakaokutana nao huko.

Huu ndio mji ambao Ibrahimu aliuona..ukamfanya aishi kama mpitaji tu hapa duniani, japokuwa alikuwa na mali nyingi na utajiri mwingi..

Waebrania 11:9 “Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

10 Maana alikuwa AKIUTAZAMIA MJI WENYE MISINGI, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu”.

Tafakari maandiko haya;

Ufunuo 21:1 “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.

2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.

3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.

5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.

6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.

7 Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Je! Na wewe utakuwa na sehemu ndani ya mji ule?

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Ninawi ni nchi gani kwasasa?

Sadaka ya Amani ilikuwaje?

Israeli ipo bara gani?

JINSI MUNGU ANAVYOIPIGA NA KUIPONYA AFRIKA.

Mretemu ni mti gani?

Hisopu/ Hisopo ni nini katika biblia?(Zaburi 51:7)

Neno ‘Kima’ linamaanisha nini Katika biblia? (Mathayo 27:9 )

Uchaga ni nini? (Luka 12:24)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments