Sadaka ya Amani ilikuwaje?

Sadaka ya Amani ilikuwaje?

Sadaka ya amani, ilikuwa ni sadaka inayotolewa kwa Mungu kutokana na amani mtu aliyoipata; Tofauti na ambavyo ingeweza kutafsirika kuwa ni sadaka ambayo mtu angeitoa kwa Mungu ili kupatana naye! (yaani kurejesha amani na Mungu), lakini sivyo, haikuwa na maana hiyo!.

Wana wa Israeli walitoa aina hii ya sadaka, pale ambapo ndani yao walipata amani. Na amani hiyo ilitokana na Mungu kuwafanyia jambo Fulani zuri katika Maisha yao labda kuwafanikisha, au kuponywa magonjwa au kupatanishwa na maadui zao n.k.

Hivyo kutokana na amani hiyo walimtolea Bwana sadaka ya kumshukuru, ndio iliyojulikana kama sadaka ya Amani. (Na sadaka Hii ilikuwa ni sadaka ya hiari na haikuwa ya amri, maana yake mtu hakulazimishwa kumtolea Mungu, ni kwajinsi atakavyojisikia yeye, kama ameona kuna sababu ya kumshukuru Mungu kwa amani basi alimtolea, kama aliona hakuna sababu basi aliacha!, hakulazimishwa).

Tofauti na sadaka nyingine ambazo mtu akipeleka mbele za Bwana, kama ni ng’ombe au mbuzi au kondoo au njiwa, mnyama yule anakuwa anateketezwa wote juu ya madhabahu baada ya kuchunwa,  lakini sadaka hii ya Amani ilikuwa tofauti kidogo!, kwani baada ya mtu kumleta mbele za Bwana katika hema, kuhani alimchuna yule mnyama, na kutoa baadhi ya viungo vichache vya ndani tu!, ambavyo ni FIGO, MAFUTA YAFUNIKAYO MATUMBO, na KITAMBI KILICHOPO KATIKA INI. Na viungo hivyo ndivyo alivyokuwa anaviteketeza juu ya madhahabu, sehemu iliyobakia yaani nyama ya mwili, ilikuwa ni kwaajili ya makuhani, na mara chache sana iliteketezwa kwa moto.

Walawi 3:1 “Na matoleo yake kwamba ni SADAKA ZA AMANI; kwamba asongeza katika ng’ombe, mume au mke, atamtoa huyo aliye mkamilifu mbele ya Bwana.

2 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake huyo aliyemtoa, na kumchinja mlangoni pa hema ya kukutania; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.

3 Naye atasongeza katika sadaka hiyo ya amani, dhabihu kwa Bwana itakayofanywa kwa njia ya moto; yaani, mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo juu ya matumbo,

4 NA FIGO ZAKE MBILI, NA MAFUTA YALIYOSHIKAMANA NAZO, YALIYO KARIBU NA KIUNO, NA HICHO KITAMBI KILICHO KATIKA INI, PAMOJA NA HIZO FIGO; HAYO YOTE ATAYAONDOA.

5 Na wana wa Haruni watayateketeza kwa moto juu ya madhabahu, juu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo katika kuni zilizo juu ya moto; ni dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana”.

Sadaka hii inatufundisha nini sisi watu wa agano jipya?

Je inatufundisha na sisi tukachune ng’ombe na kuwatoa sadaka ya kuteketezwa?.. La!, haitufundishi hivyo, bali inatufundisha kuzijali Fadhili za Bwana.

Kama Bwana amekupa amani katika Taifa unaloishi huna budi kumshukuru kwa matoleo yako kwa chochote kile angalau kila mwaka au kila mwezi..(Hiyo ni sadaka ya amani kwako kwa Bwana, usipomtolea hutendi dhambi ila pia hupati thawabu).

Vile vile kama Bwana kakupa Amani na nyumba yako, au ndoa yako..basi mshukuru kwa chochote, mtolee sadaka hiyo ya amani, naye ataona umemheshimu, na utapata baraka.

Kama Bwana amekupa amani mahali unapoishi, au unapofanyia kazi, au unapomtumikia yeye.. basi mtolee sadaka ya Amani, sadaka ya namna hiyo inaugusa sana moyo wa Mungu kwasababu anaona unazithamini Fadhili zake.

Na eneo lingine lolote la Maisha yako ambalo unaona umepata amani kwalo, mtolee chochote yeye.. Na kipeleke kwenye nyumba ya Mungu.

Na katika matoleo kumbuka jambo hili siku zote!, sadaka za amani zinapelekwa kwenye nyumba ya Bwana au kwenye utumishi wa Bwana, usipeleke kwa maskini, wala kwa ombaomba barabarani!!..

Israeli kulikuwa  na maskini wengi, lakini Bwana alimwagiza Musa na Haruni kuwa wawaambie Israeli wote wapeleke sadaka zao NYUMBANI KWAKE!..sio kwamba Mungu alikuwa hawaoni maskini!, aliwaona lakini alikuwa na sababu kubwa kwanini awaambie wapeleke nyumbani kwake!.. Ni kwasababu nyumbani kwake ndipo kunapotoka uzima!, ndipo ibada za kuwaombea Israeli wote zinapofanyika!, (ikiwemo na maskini ndani yake), ndipo walipokuwepo makuhani wa Bwana ambao muda wote wanafanya kazi ya Mungu, kuwapatanisha na kuwarejesha kwa Mungu wao!. Pasipo ile hema kuwepo ya kufanya upatanisho, Israeli ingeshafutika kitambo..Hiyo ndio maana Bwana alisema sadaka zote ziende pale, ili ule utumishi wa ukuhani uendelee kuwepo, usife wala kupotea.

Hivyo ukiwa na chochote tofauti na sadaka ya shukrani, wapelekee maskini, na wasiojiweza mitaani, lakini sadaka! Ipeleke madhabahuni kwa Bwana!..itakuletea matokeo makubwa Zaidi.

Usianze kusema, wala kufikiri sadaka yako inaliwa na wachungaji!, hiyo sio kazi yako, mwachie Bwana yeye anajua kushughulika na madhahabu yake, aliwaadhibu wana wa Eli waliokuwa makuhani kwa kuidharau sadaka ya Bwana, pasipo kusaidiwa na mtu, atashughulika na viongozi wa namna hiyo hiyo siku hizi za mwisho, lakini wewe uliyetoa hutakuwa na hatia, thawabu yako ipo pale pale.

Hivyo usisikilize uongo wa shetani uliozagaa kila mahali unaosema..nikipata sadaka napeleka kwa mayatima na ombaomba, kwasababu wachungaji ni wahuni!! Utajipunguzia thawabu zako!..Toa sehemu nyingine na kuwapa hao, lakini sadaka yako ambayo itaambatana na shukrani na maombi, ipeleke madhabahuni kwa Bwana. (HIYO NI KULINGANA NA NENO LA MUNGU!!).

Bwana atusaidie tuzijali Fadhili za Bwana.

Maran atha

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

Sadaka ya kutikiswa ilikuwaje?

Sadaka ya kuinuliwa ni sadaka ya namna gani?

SHINA LA UCHUNGU, LISICHIPUKE NDANI YETU.

Nini maana ya.. “Utoapo sadaka mkono wako wa kuume usijue ufanyalo mkono wako wa kushoto”

Mshahara wa Mbwa ni upi? Kama tunavyousoma katika Kumbukumbu 23:18

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments