SHINA LA UCHUNGU, LISICHIPUKE NDANI YETU.

SHINA LA UCHUNGU, LISICHIPUKE NDANI YETU.

Biblia inasema;

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;

15 mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo”.

Mistari hiyo kwa namna nyingine tunaweza kusema; Tukikosa amani, na watu wote, tukikosa utakatifu pia basi tutapungukiwa na neema ya Mungu, na matokeo yake ni kuwa shina la uchungu litachipuka ndani, na kuwasababishia watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.

Ni kweli mstari huu unalenga watakatifu wa Mungu..

Tukikosa, mambo hayo mawili, yaani Amani na watu wote, na Utakatifu, kuna uwezekano mkubwa sana wa hili shina la uchungu kuchipuka ndani yetu.

Jiulize kama wewe ni Mtakatifu je, una amani na watu wote? Ikiwa na maana una amani na watakatifu wenzako na watu wengine wa nje?..Ni jambo la kujitahidi sana, hata kama ni gumu ni lazima ujitahidi kama biblia inavyosema, kwasababu ukiukosa tu huo, matokeo yake ni kuwa  UCHUNGU uchungu utaanza kuchipuka ndani yako.

Kibiblia Uchungu, ni hali ambayo inakuwa na  mchanganyiko wa hasira, kinyongo, wivu, chuki, ghadhabu, na maumivu kwa mtu mwingine.

Na biblia inatuonyesha huwa linaanza kama mbegu, mpaka baadaye linachupuka na kuota mizizi mpaka kuwa shina nene. Na likishafikia hatua hiyo ya kuwa shina, kuliondoa ndani yako ni ngumu sana, litakusumbua kwa muda mrefu kweli, kwasababu tayari limeshakita mizizi kwenye moyo wako.

Hili shina limewasumbua sana wapendwa, hivyo tujitahidi sana tusilipe nafasi mioyoni mwetu..

Mfano mmojawapo katika biblia wa mtu aliyesumbuliwa na shina hili ni Mfalme Sauli.

Lilimwanza pale alipomwacha Mungu, na Mungu kuuhamisha ufalme wake kwenda kwa Daudi. Utaona alipojua hilo alianza  kumchukia Daudi kidogo kidogo, badala akatae ile hali, akaendelea kumchukia Daudi kwa kila kitu mpaka baadaye akaonyesha kwa nje sasa yale yaliyokuwa ndani ya moyo wake, akaanza kuweka mikakati ya kumwinda na kumfukuza maporini na majeshi yake ili amuue, bila sababu yoyote. Ikawa ni ngumu tena, kulishinda lile shina la uchungu lililokuwa ndani yake.

Hata alipojaribu kutubu mara ya kwanza na ya pili juu ya jambo hilo la kumwinda Daudi bado alishindwa, kwasababu shina hilo limeshakita mizizi mkubwa ndani yake (1Samweli 24).

Hivyo na sisi, tumeonywa, tujitahidi sana, tena sana tuwe na amani na kila mtu, ni jukumu la kila mtakatifu, kila mshirika, kila mtumishi, si mchungaji, si nabii, si mtume, wote,  jukumu hili ni letu, kuwa na amani na watu wote, tusiruhusu chuki, hasira, vinyongo, na wapendwa wenzetu, au ubaya wowote, vilevile na watu wa nje wa kidunia, tusigombane nao.

Kama wewe ni mchungaji, hakikisha huna neno la mshirika yoyote, au mchungaji mwenza, kama wewe ni mtendakazi kanisani, ondoa uadui wa siri na mtendakazi mwenzako, hata kama hakupendezi, jitahidi kwa upande wako uwe na amani na kila mtu kanisani.

Hiyo itatufanya tuwe mahali salama. Tuliepuke hili shina baya la adui mioyoni mwetu.

Yakobo 3:14 “Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli.

15 Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani.

16 Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.

17 Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki”.

Waefeso 4:26 “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;

27 wala msimpe Ibilisi nafasi”.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KIFAHAMU KIGEZO  CHA KUSAMEHEWA NA MUNGU.

 Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati”

TULITAFUTE KWA BIDII TUNDA LA ROHO.

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Joram masinga
Joram masinga
1 year ago

Amina kazi yenu Ni njema Mungu awabariki

Joram maainga
Joram maainga
1 year ago

Amina kazi yenu Ni njema Mungu awabariki