TULITAFUTE KWA BIDII TUNDA LA ROHO.

TULITAFUTE KWA BIDII TUNDA LA ROHO.

Wagalatia 5:22 “Lakini TUNDA LA ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Hapo biblia inasema inasema  “Tunda la Roho” na si “Tunda la roho”.. Roho hapo imeanza kwa herufi kubwa, vile vile inasema “Tunda” na si  “Matunda”.. maana yake lipo moja tu!.. Hivi ni vitu viwili vya msingi kuvijua, katika andiko hili kabla ya kuzidi kuendelea kusoma..

Leo kwa neema za Bwana tutajifunza kwa ufupi, tofauti ya vitu hivi viwili, ili itusaidie kujua ni nini tunachopaswa kuwa nacho sasa!.

  1. Tunda la Roho.

Ikumbukwe kuwa popote pale neno “Roho” linapoandikwa likianza kwa herufi kubwa “R” linamaanisha Roho Mtakatifu, lakini mahali linapoanza kuandikwa kwa herufi ndogo “r” linamaanisha aidha roho ya mwanadamu au roho ya mwovu. Hivyo katika mstari huo Roho imeanza kwa herufi kubwa ikimaanisha ni Roho Mtakatifu na si la roho ya mwanadamu.

Mahali pengine ambapo unaweza kusoma kuhusu hilo ni (Yohana 16:13,Yohana 15:26, Matendo 2:18, Matendo 6:10).

Kwahiyo Roho Mtakatifu anapoingia ndani yetu ndipo Tunda hili linapozaliwa, hatuwezi kuwa na Tunda lolote ndani yetu linalompendeza Mungu bila kupokea Roho Mtakatifu… Sasa hebu tusogee mbele kidogo kujifunza ni kwanini sio Matunda bali ni Tunda.

  1. Tunda la Roho

Labda katika mstari huo, tungeweza kuusahihisha na kusema.. “Lakini MATUNDA ya Roho ni Upendo, furaha, uvumilivu, fadhili n.k”.. lakini biblia haijasema hivyo!, bali imesema “TUNDA la Roho ni upendo, furaha, uvumilivu n.k”.. Ikimaanisha kuwa tunda ni moja tu na si mengi!.

Jambo ambalo ni sahihi kabisa, hata katika uhalisia wa maisha, hakuna mti ambao unaweza kuzaa matunda aina mbili.. mti mmoja unazaa tunda la aina moja tu!, haiwezekani katika Mchungwa, ukakuta maembe katika shina moja, na katika shina lingine ukakuta, papai au pera, hapana!, bali utakuta kama ni mchungwa, unazaa machungwa tu!, kama ni mpera utakuta ni mapera tu mti mzima!..

Luka 6:44 “kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu”.

Sasa na katika maandiko tunda la Roho Mtakatifu ni moja tu!, kama tulivyojifunza..Sasa kama ni hivyo basi hayo yaliyotajwa mbele yake ni nini?

Jibu ni kwamba, hayo yaliyotajwa ni LADHA ZA HILO TUNDA!. Maana yake ni kwamba Tunda ni moja lakini ndani yake lina ladha hizo nyingi..(ambazo ndio Upendo, furaha, amani, fadhili, kiasi, utu wema n.k).

Ni sawa niseme leo, Tunda la muembe ni tamu, zuri, laini, chachu kidogo, lenye harufu nzuri n.k. Hapo nimetaja tabia za tunda moja tu na si mengi!.

Sasa na Tunda la Roho ni hivyo hivyo, Mtu mwenye Roho Mtakatifu anazaa tunda lenye mchanganyiko wa ladha hizo: yaani upendo,  amani, furaha, fadhili, utu wema, kiasi, KWA UFUPI UTAKATIFU!. Hivyo tabia zote hizo zipo ndani ya tunda moja.

Haiwezekani mtu awe na upendo halafu akose fadhili, kama hana fadhili maana yake hana upendo, haijalishi atauigiza upendo kiasi gani, vile vile haiwezekani mtu awe na amani akose utu wema au kiasi..Mambo hayo yote yanakwenda pamoja kwasababu yote yanapatikana katika tunda moja la Roho Mtakatifu.

Hivyo siku zote kumbuka mtu wa Mungu, kwamba kama huna Roho Mtakatifu ndani yako huwezi kuwa na amani, upendo, uvumilivu, ambayo yote hayo kwa ujumla ni utakatifu. Na vile vile unapopokea Roho Mtakatifu ni lazima tabia zote hizo zionekane, haitakiwi kupunguka hata mojawapo!!.

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”

Umeona umuhimu wa Roho Mtakatifu???…Je umepokea Roho Mtakatifu?.. kwa kutubu na kumwamini Yesu, na kubatizwa??.. kama bado kumbuka huwezi kamwe kuzaa tunda lolote katika Roho, vile vile biblia inasema wote wasio na Roho Mtakatifu hao sio wake (soma Warumi 8:9). Je na wewe ni miongoni mwa ambao sio wake?.. Habari njema ni kwamba, Mungu anatupenda wote, na ahadi hiyo ya Roho Mtakatifu sio ya watu Fulani baadhi tu!, hapana! Bali ni ya watu wote watakaomkimbilia yeye, haijalishi ni warefu, wafupi, wanene, wembamba, wazima, wagonjwa, maskini, matajiri, waliosoma au ambao hawajasoma.. Hiyo ni ahadi ya Baba kwa kila mtu anayepumua!..

Matendo 2:38  “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39  KWA KUWA AHADI HII NI KWA AJILI YENU, NA KWA WATOTO WENU, NA KWA WATU WOTE WALIO MBALI, NA KWA WOTE WATAKAOITWA NA BWANA MUNGU WETU WAMJIE”.

Lakini huna budi kwanza kumkubali Yesu moyoni mwako, na kwenda kubatizwa ubatizo sahihi ili ahadi hii ya Roho Mtakatifu ije juu yako. Na kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na mstari huo hapo juu!.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

AHADI YA ROHO ILIYOSALIA SASA KWA KIPINDI CHETU.

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments