NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

Shalom,

Kuna kipindi mitume walimpelekea Bwana hitaji hili;

Luka 17:5 “… Tuongezee imani”.

Kwao pengine hili lilikuwa ni hitaji jepesi sana , lakini kwa upande wa Bwana halikuwa ombi la kuwajibu kwa sentensi mbili, au kwa kuwawekea  mikono tu na kupokea, hapana, na ndio maana baada ya ulizo hilo, hakukuwa na jibu la moja kwa moja kutoka kwa Bwana.

Sehemu nyingine alipoona upungufu wa Imani yao Bwana Yesu aliwaambia , namna hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa “kufunga na kuomba”(Mathayo 17:21)  Na sehemu nyingine biblia inasema, Imani huja kwa kukisikia Neno la Mungu(Warumi 10:17).. Ikiwa na maana kuwa kwa jinsi unavyosoma Neno la Mungu, na kuona uweza wa Mungu alioufanya, tangu enzi na enzi, sasa kwa jinsi unavyosoma sana na kusikia Neno lake, ndivyo imani yako inavyojengeka kwake, na hatimaye unakuwa na imani timilifu, hata ya kuweza kuamishi milima kwa jina lake.

Lakini katika yote hayo utagundua kuna kitu kimoja kinachoitwa BIDII ndani yake..Ikiwa na maana imani haiwezi kuja hivi hivi tu kwa kukaa, kama hutakuwa na bidii ya kuitafuta, haitakaa ije kwako kamwe, haiji kwa kuwekewa mikono, wala haiji kwa kuombewa,..

Sasa Imani ni nguzo mojawapo ya Ukristo, zipo nguzo nyingine mbili za Ukristo nazo ni Upendo na Tumaini. Lakini leo hatutazungumzia juu ya Tumaini, bali tutazungumzia juu ya Upendo, ambao ndio mkuu kuliko hata Imani au tumaini.

Upendo ni kilele cha Ukristo, Kwasababu biblia inasema Mungu mwenyewe ni Upendo.

Na Mkristo aliyekuwa sana kiroho, atatambulika kwa kiwango chake cha Upendo. Lakini wengi wetu tunadhani upendo ni kuonyesha tabasamu zuri kwa mtu, au kumsaidia mtu sana. Hivyo ni kweli ni vimelea vizuri vya Upendo, Lakini Upendo wa ki-Mungu unavuka hapo, na kwenda zaidi.

Embu tuvipitie baadhi ya vipengele vikuu,na mwishoni kabisa tutajifunza jinsi gani tutaupata huu Upendo mkamilifu.

1 Wakorintho 13

13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.

2 Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.

3 Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.

4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika”.

Ukianzia kusoma ule mstari wa 4, utaona misingi inayoubeba upendo ikanza kuzungumziwa,  anasema huvumilia. Jiulize  je ndani yako ulishawahi kuvumilia mabaya mangapi pale ulipotendewa, je pale alipokuaibisha uliweza kutunza siri yake?, je, ulimsamehe pale alipokuaibisha, je ulivumilia yote hayo yote bila kuweka kinyongo, au kukomoa?

Anasema tena, Upendo hufadhili; Neno fadhili ni pana sana, ni zaidi ya kumfanyia mwenzako wema, ambao hauna malipo yoyote kwako. Anasema tena, hautakabari, haujivuni, huatafuti mambo yake mwenyewe, je maisha na namna hiyo yapo ndani yako? Wewe kama mkristo uliyeokoka?

Anasema Upendo haukosi kuwa na adabu, Je! Wewe wakati wote unayo adabu kwa watu wote?, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, yaani inafikia hatua hauoni mabaya bali mema tu mtu anayokufanyia, Je ulishawahi kuwa mtu wa namna hii?  Ulishawahi kuwa mtu wa kustahimili mambo yote, au kuvumilia mambo yote, au ni baadhi tu ya mambo umeyaweza? Kama ni baadhi tu basi Upendo wa ki Mungu bado haujakamilika ndani yako. Haijalishi utajiona ni mwema kiasi gani.

Hivyo utoshe tu kusema kwa namna ya kibinadamu  Pendo hili la Ki-Mungu, si rahisi kulipata kwa maneno tu, au kwa kuombewa au kwa kuwekewa mikono, , hauwezi kustahimili yote, yapo mengine ambayo yatakuudhi, upo wakati ambao utawahusudu wengine, upo wakati ambao, utahesabu mabaya tu n.k. Huo ndio ukweli.

Lakini sasa tufanyeje ili tuyashinde hayo yote?

Kanuni ni ile ile, kama ya IMANI, unapaswa uonyeshe bidii, katika kutekeleza hivyo vitu.

1Petro 4:8 “Zaidi ya yote IWENI NA JUHUDI NYINGI KATIKA KUPENDANA; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi”.

Inahitaji juhudi, mpaka ujijenge na kuwa tabia ndani yako, unapoona mwenzako amekutendea mabaya, unapaswa ujitahidi kwa nguvu zote, kuyaachilia yale mabaya anayokufanyia, na kujifunza kuyatafakari yale mazuri yake.. Ndio siku za mwanzoni mwanzoni, itakuwa ni ngumu lakini unavyojijengea utaratibu huo kwa nguvu, baadaye inageuka na kuwa ni tabia yako. Mpaka mwisho wa siku, hata jambo liwe ni gumu kiasi gani, utaona linatapita tu mbele yako kama upepo, bila kikusumbua hata kidogo .

Kumbuka tena vimelea hivyo vya upendo haviji hivi hivi tu, kwa kuombewa, au kusubiria, bali vinakuja kwa kuonyesha bidii, yaani kuvitendea kazi, mpaka ufikie hatua ya kutoona uchungu, au kutohusudu, kunahitaji kukataa usengenyaji kuanzia sasa, kukataa kusikiliza maneno ya watu mabarazani, pale wanapomzungumzia mtu mwingine kwa ubaya. Kunahitaji kujitoa kwa wengine, bila kujali unapata faida gani kwao..N.k.

Warumi 12:10 “Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu;

11 kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;”

Upendo ni kitu cha kujazilishwa, yaani kila siku unakiongezea nyama mpya, kimoja huzaa kingine, na kingine huzaa kingine, mpaka tunafikia vile viwango vya Upendo wa ki-Mungu

2Petro 1:5 “Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa,

6 na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa,

7 na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.

8 Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo”.

Hivyo mimi na wewe kuanzia leo tuanze kuyatendea kazi haya, tujazilishe upendo wetu, siku baada ya siku tuongeze kimelea kipya cha upendo, Kwasababu tujue kuwa kitu cha kwanza ambacho kitatusogeza kwa Mungu kwa urahisi na haraka si Imani au tumaini bali ni Upendo, kwasababu yeye mwenyewe ni Upendo, na ndio maana Paulo anasema, hata nijapokuwa na Imani timilifu ya kuamisha milima kama sina Upendo mimi si kitu. Maana yake ni kuwa, huwezi kumwona au kumjua Mungu ukiukosa huo,

1Yohana 4:8 “Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo”.

Hivyo jambo hili, na kuwa nalo siriazi, ni kulitendea kazi kwa bidii zote, kila wakati kila muda mpaka lijengeke na kuwa tabia yetu.

1Petro 1:22 “Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo”.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UPENDO WA MUNGU.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU UPENDO.

Sadaka ya kuinuliwa ni sadaka ya namna gani?

Mtu mwenye “kitango” ni mtu wa namna gani kibiblia?

TUSIWE WATU WA KUPUNGUKIWA AKILI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
1 year ago

Bwana akubariki sana mwalimu,kwa kweli kupitia somo nimejiona sina huo upendo wa ki-MUNGU japo natamani kuwa nao.Sasa naanza kufanyia kazi kanuni ulizozisema ili kuujenga huo upendo wa ki-MUNGU ndani yangu Mungu na anisaidie.

M
M
1 year ago

Ubarikiwe mtumishi wa Mungu