YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

Madhabahuni ni mahali ambapo Mungu amepachagua kukutana na mwanadamu. Hivyo palipo na madhabahu ya Mungu mtu anaweza kuwasilisha dua zake, ibada yake, na shukrani zake, na Mungu akazipokea. Mahali pasipo na madhabahu haiwezekani kukutana na Mungu, na kama ikitokea hivyo basi ujue ni kwa neema zake tu, kakujibu pengine kwasababu hukuujua ukweli. Lakini hakuna njia mtu anaweza kuwasiliana na Mungu pasipo madhabahu.

Sasa tunapozungumzia madhabahu hatumaanishi lile eneo la mbele kanisani linalopambwa, hapana, hicho ni kivuli tu cha madhabahu, madhabahu halisi kwasasa ipo rohoni kule mbinguni, kiti cha enzi cha Mungu kilipo. Na Yesu mwenyewe ndio nyenzo ya kutufikisha hapo, Ikiwa na maana ili uweze kumfikia Mungu ni sharti DAMU ya Yesu ikutangulie kwanza kuzifunika dhambi zako. Hapo ndipo utajua ni kwanini alisema yeye ndio njia kweli na uzima, mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye.(Yohana 14:6) .Watu wengi wanadhani wanaweza kumkaribia Mungu kwa matendo yao wenyewe au dini zao. Hilo halipo kabisaa.

Sasa turudi kwenye kiini cha somo. Ni nini kinaendelea sasahivi  katika madhabahu ya Mungu rohoni. Kama tulivyotangulia kusema madhabahuni ni mahali ambapo watakatifu wanafikisha Maombi yao au  haja zao kwa Bwana.

Na ni vizuri kufahamu watakatifu wamegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni watakatifu walio hai duniani, na kundi la pili ni watakatifu waliokufa. Na wote hawa wanawasilisha mahitaji yao mbele ya madhabahu ya Mungu mbinguni. Na leo kwa ufupi tutajifunza ni mahitaji gani wanayasalisha mbele za Mungu.

Utakumbuka Bwana Yesu alitufundisha kuomba, na katika kuomba kule alisema tutamke maneno hili..

Mathayo 6:9 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, UFALME WAKO UJE,…

Hii ikiwa na maana kuwa kila mtakatifu aliyepo duniani, kumwomba Mungu ufalme wake uje, ni sehemu ya maisha yake ya kila siku. Hivyo mbele ya madhabahu ya Mungu iliyopo mbinguni, maombi haya yanafikishwa na malaika na kuwekwa mbele ya madhabahu ya Mungu,..Na hivyo Mungu anachofanya ni kuiharakisha ile siku ya kurudi kwake, ifike upesi.

Ufunuo 8:3 “Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi”.

Unaona? Lakini si hilo tu, bado upande wa pili wa watakatifu nao waliokufa katika dhiki, wanayo maombi yao wanayoyapeleka..embu tusome..

Ufunuo 6:9 “Na alipoifungua muhuri ya tano, NIKAONA CHINI YA MADHABAHU ROHO ZAO WALIOCHINJWA KWA AJILI YA NENO LA MUNGU, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao.

10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?

11 Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao”.

Unaona, hawa nao wanaonekana wapo chini ya madhabahu, wakiomba.. Hivyo wakati watakatifu wa duniani wanaomba ufalme wake uje..Watakatifu walio ardhini wanaomba mwisho wa waovu ufike.

Walio mbele ya madhabu wanalia Unyakuo ufikie upesi, utawala wa amani wa miaka 1000 uje haraka, karamu ya mwanakondoo ianze upesi.. wakati huo huo waliochini ya madhabahu wanaomba, waovu walipizwe kisasi, wauaji, wafikishwe katika kiama chao, mbingu zikunjwe kunjwe kama ukurusa, mapigo ya vitasa saba yamiminwe juu ya nchi, ili isafishwe, waje wastarehe na Bwana ulimwenguni milele.

Haya ni maombi mazito sana, na yanausumbua moyo wa Mungu, usiku na mchana, vilio vyao na vyetu vinamfikia kila dakika kila sekunde, kutoka huku duniani na kule peponi walipo watakatifu waliokufa.

Na tunasoma majibu Bwana aliyowapa wale waliolala yalikuwa ni haya..”WASTAREHE KIPINDI KIFUPI SANA”.. Kumbe kimebaki kipindi kifupi, majibu ya maombi yote yajibiwe, ndugu yangu, siku isiyokuwa na jina Yesu atarudi, Kama tunavyoona dalili zote, jinsi zinavyotimia kwa kasi sasa, mfano wa gonjwa hili la Corona (Luka 21:11). Hii ni kuonyesha kuwa siku yoyote tutashuhudia tukio la UNYAKUO.

Siku hiyo pengine ni leo usiku, tutashangaa ghafla kundi fulani dogo sana la watu halipo. Ukiona hivyo basi ujue umebaki, na utakachokuwa unasubiria ni kisasi cha Mungu mwenyewe duniani.  Ambacho kitatanguliwa kwanza na ile dhiki kuu ya mpinga-kristo (666), ile ambayo Bwana Yesu alisema haijawahi kutokea wala haitakaa itokee . Na baada ya hapo ndipo mapigo ya vitasa saba yafuate (Ufunuo 16), Kisha, ulimwengu wote kumalizwa. Watu watatamani mauti lakini itawakimbia, ni kilio na kusaga meno.

Usifikiri tuna muda mrefu tena kama zamani, injili ya sasa sio ya kubembelezewa wokovu. Ni wewe mwenyewe ushtuke utoke usingizini, utengeneze mambo yako na Mungu wako. Ukipumbazwa na injili za manabii wa uongo, wanaokufundisha, ustarehe hapa duniani, kana kwamba hii dunia ni urithi wako utaishi hapa milele. Jihadhari sana, kwasababu Yesu alishatuonya juu yao kwamba watawadaganya hata yamkini walio wateule(Marko 13:22).

Hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kugeuka, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi, wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. Na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu. Hapo ndipo utakuwa umezaliwa mara pili. Na ukiendelea kudumu katika wokovu na utakatifu basi hata Kristo akirudi usiku wa leo, unakwenda naye mbinguni.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

TUFANANE NA WATAKATIFU WA MAKEDONIA.

Je! Mwandishi wa kitabu cha Warumi alikuwa ni Paulo au Tertio?

Ni nani aliyesema “Nitume mimi”? katika (Isaya 6:8)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Amen…Mbarikiwe Sana…kwa masomo mazuri

Kaungwa Johnson
Kaungwa Johnson
2 years ago

Nimependa sana masomo yenu. Nami nimetubu na kuishi maisha ya kumpendeza MUNGU kwa kadri ya baraka zake na uwepo wake katika maisha yangu naiona sana. Jambo ambalo umelieleza la kubatizwa kwa maji mengi sijafanya, nimebatizwa toka utoto na naamini moyoni mwangu kuwa nimebatizwa. Je nikosa?