TUFANANE NA WATAKATIFU WA MAKEDONIA.

TUFANANE NA WATAKATIFU WA MAKEDONIA.

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maandiko. Sisi kama wakristo, ili tuweze kukua kutoka utukufu hadi utukufu, na imani hadi imani, hatuna budi kuyatafakari maneno ya Mungu sana kwa kadiri tuwezavyo.

Leo tutajifunza tabia za kipekee walizokuwa nazo watu wa Makedonia nyakati zile za mitume.

Makedonia iliundwa na makanisa makuu matatu, (Kanisa la Wathesalonike, Wafilipi, na Waberoya). Hawa watu walikuwa ni wa kipekee sana, Kwamfano watu wa Beroya, tabia yao ya kupenda kuchunguza maandiko pengine iliwasaidia kutambua jukumu kubwa sana ambalo walipaswa walitimize katika utakatifu wao. Na jukumu lenyewe lilikuwa ni katika suala la UTOAJI.

Sasa kwa ufupi tutatazama waliwezaje kulitimiza hilo jukumu katika mazingira magumu waliyokuwa nayo. Naamini na sisi lipo la kujifunza kwa watu hawa, ili tusijikute tunakwamishwa na jambo lolote katika kuuelekea ukamilifu wetu. Embu tuzisome tabia zao ambao zinazungumziwa katika kitabu cha 2Wakorintho 8:1-15

  1. Tabia ya kwanza ni kuwa Wamakedonia ni watu waliokuwa katika dhiki nyingi na umaskini mkubwa.

Lakini hawakusahau kumtolea Mungu, katika umaskini wao, kiasi kwamba wao ndio wakaongoza katika kuitimiza huduma hiyo kuliko makanisa mengine yote .

2Wakorintho 8:1 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;

2 maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.

Mfano mzuri wa kuiga, kumbe umaskini wetu, hauwezi kuwa kikwazo katika  kumtolea Mungu.. Mtume Paulo anatuthibitishia kuwa maskini ndio walioongoza kumtolea Mungu miongoni mwa makanisa yote aliyoyahudumu mataifa mbalimbali.

       2) Licha ya kuwa katika umaskini mwingi, lakini bado walikuwa tayari kutoa hata zaidi ya uwezo wao.

2Wakor 8:3 “Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao;”

Embu tutengeneze picha, maskini pengine anayo sh.100 tu lakini anaona hiyo bado haistahili kuipeleka kwa Mungu, anakwenda kuuza hata ile baiskeli yake, anayoitegemea kwenda nayo shambani kila siku, ili tu apate kiasi kingi kidogo  cha pesa akamtolee Mungu, awe radhi kutumia miguu yake kwenda shambani, kuliko kupeleka kiwango kidogo kwa Mungu wake. Unadhani huko tukuiteje, kama sio kutoa zaidi ya uwezo wako.

Sasa mambo kama haya, yalikuwa ni kawaida kwa watakatifu wa Makedonia.

Tujipime na sisi wakristo wa leo hii, pengine Mungu amekubariki gari, tuachilie mbali kwenda kuliuza na kumletea Mungu thamani yake je! Tunaweza kupanda daladala wiki 2 mfululizo, halafu hiyo pesa ambayo tungetumia katika kununua mafuta kila siku  tukaipeleka kanisani? Je hilo linawezakana? Au utampelekea Mungu elfu 1, na huku wiki nzima umetumia elfu 50 ya mafuta?. Je tunaweza kuwafikia watakatifu hawa, ambao walijitoa kwa Mungu zaidi ya uwezo wao?

      3) Walifurahia kumtolea Mungu, kwa moyo wa furaha, licha ya kuwa walikuwa ni maskini, na walitoa zaidi.. 2Wakor 8:3

Tabia nyingine ni hii, walifurahia kufanya hivyo. Hawakuwa wanung’unikaji, walipomtolea Mungu, ndivyo walivyopata amani mioyoni mwao, lakini ni rahisi sana kuona mtakatifu wa leo anatoa malalamiko kwa kila anachokitoa, utasikia, Yule mchungaji anakula sadaka zetu, mbona hatuoni matumizi ya pesa zetu kanisani. Na kwa kawaida ukiangalia hao wanaonung’unika hivyo, asilimia kubwa huwa si watoaji.

       4) Wao wenyewe waliomba na kusihi katika kutoa.

8:4 “Wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu”.

Unaona? Waliwasihi mitume, waitimize huduma hiyo, kana kwamba wanachokifanya ni kwa faida yao,. Embu fikiria wewe leo, mtu anakuja kukuomba akupe pesa tena kwa kukusihi, Unaweza kudhani ni tajiri sana, au ana pesa za mchezo, lakini kumbe sio, hawa watu walikuwa maskini kama tunavyosoma, lakini walijua wajibu wao kwa Bwana.

Na sisi je! Tutamsubiri mpaka mchungaji wetu atukumbushe, kwa habari za zaka? Atukumbushe kuwa kuna kazi ya injili inahitaji fedha? Hapana, ni wajibu wetu kukumbuka, na kumtolea Bwana, pale anapotuamrisha.

       5) Pia Utoaji wao ulianza kwanza na kujitoa kwa Bwana.

2Wakor 8:5 “Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu”.

Kuonyesha kuwa, tabia ya utoaji, huwa chanzo chake ni kujitoa kwanza kwa Bwana.. Hawa watu walikubali kujibidiisha na mambo yote ya Mungu. Na ndio maana hawakuona ugumu wowote na kutoa hata zaidi ya uwezo wao kwa Mungu.

Hivyo mwisho kabisa mtume Paulo alipoona mwenendo wa watakatifu hawa wa Makedonia alitaka na makanisa mengine yote yaige mfano wao, hususani kanisa la Korintho, litimize karama hiyo pia, “ili auone unyofu wa upendo wao”.

2Wakor 8:8 “Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu”.

Hata leo, wapo watakatifu ambao katika roho wapo Makedonia, watu kama hao utawaona tu, kazi ya Mungu, hawaichukulii kama kazi-baki, bali kama ni kazi ya kuthaminiwa sana, wanaelewa kuwa ina gharama zake na mahitaji yake, Hivyo hata kama wapo katika umaskini, hawana kazi, au wana kazi, wanakuwa na moyo kweli kwa kuijali kazi ya Mungu kwa vyovyote vile Mungu anavyowabariki, na wengine wanajitoa hata zaidi ya uwezo wao, ukidhania kuwa ni matajiri sana kumbe, hata kesho hawajui watakula nini, ni moyo wao tu wa upendo kwa Mungu.. Mungu azidi kuwabariki sana watu kama hawa.

Lakini wapo watakatifu wengine ambao kiroho wapo Korintho, ambao utoaji kwao ni jambo lisilo la umuhimu sana. Watakuwa tayari kusikiliza injili, na kulishwa vya rohoni kanisani, kufundishwa miaka nenda rudi, lakini wasijitoe hata kwa lolote kwa Mungu. Kisingizio chao kikubwa ni sina kazi, au ninapitia shida hii au ile, au nina madeni, nina mikopo nahitaji kurejesha..Ni kweli kama utakuwa unafikiria hilo, basi usiwasahau pia na watu wa Makedonia. Ambao walikuwa katika majaribu makubwa na umaskini wa kupindukia, pengine kuliko wewe, lakini hawakuzihusisha shida zao na kumtolea Mungu wao aliyewaumba.

Kumtolea Bwana, si kuchangia mabilioni, lakini kumtolea kinono kwa kile anachokujalia ndicho anachothamini, mfano wa Yule mwanamke mjane aliyemtolea Bwana senti mbili. Unaona> Kama Mungu anakujalia sh. 100 kwa siku, ukimtolea Mungu hata 50, Mungu anathamini sana. Kushinda Yule anayejaliwa bilioni 1 halafu anamtolea Mungu milioni 1 tu..

Hivyo tujitahidi sana, tufanane na watakatifu wa Makedonia.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments