Nini maana ya.. “Utoapo sadaka mkono wako wa kuume usijue ufanyalo mkono wako wa kushoto”

Nini maana ya.. “Utoapo sadaka mkono wako wa kuume usijue ufanyalo mkono wako wa kushoto”

Jibu: Tusome kuanzia juu kidogo,

Mathayo 6:1“ Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.

2 Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu

3 Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume;

4 sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”.

Kwa namna ya kawaida haiwezekani kufanya jambo mkono wako mmoja usiwe na mawasiliano ufanyalo mkono wako wa pili, Kwasababu mwili wako wote umeungamanishwa na kuwa kitu kimoja. Kwahiyo Bwana Yesu alipotoa huo mfano hakumaanisha kuwa tutafute namna ambayo wakati tunatoa sadaka mkono wa kushoto usijue ufanyalo mkono wa kulia. Bali alitumia huo mfano kama kionjo tu!. Ambacho kingetusaidia kuelewa kwa kina anachotaka kumaanisha.

Kwamba sadaka zetu ziwe za siri za hali ya juu, zisiwe za kutangaza tangaza, kiasi kwamba hata wewe mwenyewe kwenye nafsi yako (mwili wako) huitangazi tangazi…Unakuwa unaitoa na kuisahau..

Luka 18:10 “ Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.

Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.

12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma; HUTOA ZAKA KATIKA MAPATO YANGU YOTE.

13 Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.

14 Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa”.

Sasa sio kwamba huyo mtoza ushuru hapo juu, hakuwa anatoa zaka, au sadaka.. Alikuwa anazitoa, pengine zaidi hata ya huyo Farisayo, lakini kila alipotoa katika nafsi yake anakuwa anazisahau, hajinyanyui mbele za Mungu, wala hazitaji taji mbele za Mungu, kila siku anajiona kama hajamtolea, anakuwa hazihesabu, anajiona kama bado ana deni kubwa la kumtolea Mungu…. Hivyo hiyo ikamfanya awe wa haki zaidi kuliko ya yule Farisayo, ambaye alikuwa anajiinua inua katika nafsi yake.

Lakini zama hizi ni kinyume chake, hebu mtu amtolee Mungu sadaka Fulani, labda kiwango Fulani cha fedha, utaona jinsi atakavyotangaza kwa watu, atawejiwekea mazingira kila mtu ajue, na hata wakati mwingine kunung’unika nung’unika, anapoona jambo Fulani halipo sawa (kila mara utasikia anataja..sadaka zetu zinafanyiwa hichi au kile!!).. na hata akifaulu hilo (akawa hanung’uniki), utaona anavyojinyanyua kila siku mbele za Mungu katika sala zake.. Akisali utasikia, mwezi uliopita nilikutolea sadaka hii!..wiki iliyopita nikakutolea tena.. jambo hilo atalirudia rudia mara nyingi…kila sadaka anayotoa anaihesabu na anaona ni kama anamnufaisha Mungu kwa sadaka zake na wala si kama ni wajibu wake.

Lakini wakati huo huo yupo mwingine ambaye hawezi kupitisha wiki, hajamtolea Mungu sadaka nono, na kila anapopiga magoti mbele za Mungu anajiona kama hajawahi kumtolea chochote. Sadaka aliyoitoa wiki iliyopita hata haikumbuki! (Huyo ndio mfano wa mtu yule anayetoa sadaka ambayo hata mkono wake mmoja haujui ifanyacho mkono wake wa pili).

Hivyo Neno hilo ni kutufundisha tu, jinsi ya kuenenda mbele za Mungu, ili tupate thawabu, tufahamu kuwa tunapomtolea Mungu, au tunapowapa vitu watu, tusijionyeshe mbele za watu wala mbele za Mungu, Ukishatoa sahau kama umetoa, zaidi ya yote tutafute kumtolea tena na tena.. Ndivyo tutakavyopata thawabu kutoka kwa Mungu, lakini kinyume cha hapo, Bwana Yesu alisema, tumekwisha kupata thawabu zetu.

Bwana atubariki na kutusaidia.

Kumbuka, kama unaisikia injili leo na kuipinga, kama unahubiriwa uache uzinzi, na hutaki kuamua kuacha makusudi, kama unahubiriwa uache ulevi, na wizi na mambo yote machafu hutaki na unatafuta kumtolea Mungu sadaka, biblia inasema “kutii ni bora kuliko dhabihu (1Samweli 15:22)”.. na pia inasema…

Mhubiri 5:1 “Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili usikie, Kuliko kutoa kafara ya wapumbavu; Ambao hawajui kuwa wafanya mabaya”.

Na pia inasema “Sadaka ya wasio haki ni chukizo;..(Mithali 15:8)” Na tena…

Kumbukumbu 23: 8 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili”.

Usichukue mshahara wako wa kazi ya Bar na kumpelekea Mungu, ukidhani inamfurahisha sana hiyo sadaka.. Yeye anaihitaji roho yako ipate wokovu na si fedha yako. Sadaka ni matokeo ya shukrani, sasa utamshukuru vipi mtu ambaye umemkataa moyoni mwako?..si utakuwa ni mnafiki na kumfanya ahuzunike juu yako?.

Hivyo kama hujampokea Yesu, leo unayo nafasi, kabla ya kufikiria kwenda kumtolea Mungu, fikiria kwanza kuondoa roho ya uasherati, ulevi, kujichua, wizi na nyinginezo ndani yako. Baada ya hapo ndipo fikiria kwenda kumtolea Mungu, na unapomtolea hakikisha hujinyanyui mbele zake.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

NGUVU YA SADAKA.

Sadaka ya kuinuliwa ni sadaka ya namna gani?

2Samweli 24:1-14,inasema ni jambo la kutisha kuangukia katika mkono wa Bwana je! inakinzana na Waebrania 10:31?.

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

Kwanini Yesu aliwakataza mitume wake kumdhihirisha?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments