TUNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU.

TUNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU.

Jina la Bwana wetu, Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze biblia, neno la Mungu lililo hai, lenye nguvu na uwezo.

Tunapomwamini Bwana Yesu na kubatizwa, na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, biblia inasema tunatiwa muhuri mpaka siku ya ukombozi wetu.

Waefeso 4:30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi”.

Hapo biblia inasema tumetiwa muhuri hata siku ya ukombozi.. Ukombozi unaozungumziwa hapo ni ukombozi wa miili yetu, yaani siku ile tutakapovikwa miili mingine ya utukufu isiyoharibika.. Na tendo hilo litatokea siku ile ya unyakuo. Ambapo kama biblia inavyosema, kufumba na kufumbua parapanda ya mwisho italia, na wafu waliokufa katika Kristo watafufuka, na kwa pamoja miili yetu itabadilishwa na kuvaa kutokuharibika (1Wakorintho 15:52-54).

Upo ukombozi wa Roho zetu, ambao huo tunaupata pale tu tunapompokea Yesu na Roho Mtakatifu na kubatizwa. Hapo roho zetu zimekombolewa kwa damu ya Yesu.. Lakini ipo siku nyingine aliyoiandaa Mungu, kwaajili ya ukombozi wa miili yetu (ambayo ndio siku ile ya parapanda).

Ndio maana ijapokuwa tumempokea Yesu bado miili yetu hii wakati mwingine inapitia magonjwa, maumivu, mateso n.k..Ni kwasababu gani??..

Ni kwasababu bado ukombozi wake haujakamilika, siku ya ukombozi wa miili yetu itakapofika hatutaugua tena, hatutakuwa na maumivu, hatutasikia njaa, hatutashindana na mwili tena kama tunavyoshindana nao sasa.

Warumi 8:23 “Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, UKOMBOZI WA MWILI WETU”.

Kwahiyo kwasasa tunapookoka, (yaani tunapomwamini Yesu, na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu) tunapata ukombozi wa Roho zetu. Roho zetu zinakuwa zipo salama, haziteseki tena, haziteswi tena na adui, ndio maana mtu aliyeokoka japokuwa anaweza kulala njaa, lakini utaona bado ana furaha, ijapokuwa anapitia magonjwa lakini amani na furaha ndani yake bado vinatawala, ijapokuwa anapitia mambo yote ya kutesa katika mwili lakini roho yake bado haijakata tama, ipo salama (hata anafikia kusema na kuimba “Ni salama rohoni mwako”).. roho yake inakuwa ni ya ushindi siku zote.

Ni kwanini?..Jibu ni rahisi ni kwasababu kashapata ukombozi wa roho yake siku ile alipookoka na kupokea Roho Mtakatifu. Mtu wa namna hiyo biblia inazidi kusema kwamba uhai wake unakuwa umefichwa pamoja na Mungu (Wakolosai 3:3). Roho yake, adui hawezi kuipata tena.

Sasa kipindi hicho ambacho tumepata ukombozi wa roho zetu, huku tukisubiri ule wa miili yetu.. Kipindi hicho hapo katikati, biblia inasema tunakuwa tunalindwa na NGUVU ZA MUNGU.

1Petro 1:5 “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho”.

Hivyo pindi tu tunapopata wokovu wa roho zetu, hapo hapo nguvu za Mungu zinashuka juu yetu, kutufunika na kutulinda, mpaka siku ya ukombozi wa miili yetu. Maana yake ni kwamba, Majaribu yote kuanzia huo wakati yatakayokuja mbele yako yatakuwa ni kwa lengo la kukufundisha (yaani madarasa), na si kukuangusha au kukupoteza, na ni Mungu anakuwa ameyaruhusu.

Yakobo 1:2 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;

3 mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi”.

Lakini kama hujapata ukombozi wa roho yako (yaani hujamwamini Yesu na kubatizwa ubatizo sahihi, na kupokea Roho Mtakatifu).. Usijihesabie kwamba kuangukia kwenye majaribu ni furaha, bali huzuni!!… Kwasababu hayajatoka kwa Mungu hayo bali kwa adui shetani, na lengo la hayo majaribu ni kukupoteza.

Majaribu yote unayopitia kabla ya kumpokea Yesu, ni shetani ndiye aliyekuwa anakutesa nayo, na lengo lake lilikuwa ni ufe!! Na upotee kabisa…kwasababu ulikuwa umetoka nje ya nguvu za Mungu. Lakini Majaribu yanayokuja ukiwa ndani ya Kristo, lengo lake ni kukuimarisha na kukufanya imara na si kukuangusha au kukupoteza na mwisho wake yanakuwa na mlango wa kutokea. Lakini hayo mengine yanakuwa hayana mlango wa kutokea, Mlango wake wa kutokea ni aidha kumpokea Yesu au kufa!!.. Lakini hayatatuliki kwa njia nyingine yeyote.

Hivyo uchaguzi ni wetu!. Kumpokea Yesu, na kukaa CHINI YA NGUVU ZA MUNGU, tukilindwa mpaka siku ya ukombozi wa miili yetu, au kukaa nje ya nguvu za Mungu, tukiteswa na adui shetani bila kuwa na suluhu yoyote, mpaka tunakufa.

Kama leo hii unataka kukaa chini ya ulinzi wa Nguvu za Mungu, ni rahisi sana. Nguvu za Mungu hutazipata kwa kuombewa, wala kuwekewa mikono, bali utazipata kwa kulielewa na kulipokea Neno la Mungu, hilo tulilojifunza. Kwamba zitakuja juu yako kwa kumwamini Yesu kwanza kwamba ni Bwana na mwokozi, na kwamba anazo NGUVU NYINGI SANA, zisizo na ukomo!..na kwamba alizaliwa na bikira miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita, na akazikwa na siku ya tatu akafufuka, na sasa hivi yupo Mbinguni, hafi tena!!!. Na atarudi tena kwaajili ya kulinyakuwa kanisa lake (yaani wale wote waliompokea), na kuhukumu ulimwengu, na kwamba hakuna njia nyingine yeyote ya kumfikia Mungu zaidi yake yeye.

Ukishaamini hivyo hatua inayofuata ni ubatizo. Alisema katika Marko 16:16, kwamba aaminiye na kubatizwa ataokoka!!..maana yake ukombozi bila ubatizo haijakamilika. Hivyo unapaswa ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi (Yohana 3:23), na kwa jina la YESU KRISTO, ambalo ndio jina la Baba,Mwana na Roho Mtakatifu, hilo jina moja la Yesu ndio tunalopaswa kubatiziwa kwalo. Na Baada ya hapo Yule Roho ambaye ataingia ndani yako wakati unabatizwa au ambaye alishaingia kipindi kifupi kabla ya kubatizwa, atakuongoza na kukutia katika kweli yote ya kuyaelewa maandiko.

Na kuanzia hapo na kuendelea, NGUVU ZA MUNGU, zitashuka juu yako, zitakazokulinda kuanzia hapo na kuendelea, hivyo utakapoanza kuona unapitia majaribu Fulani madogo madogo, usiogope, yachukulie tu kama darasa, kwasababu ni Mungu kayaruhusu na zipo nguvu zake zinakulinda na kukushikilia, huwezi kuanguka wala kupotea.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

VAZI KUU AMBALO MUNGU AMETUANDALIA KILA MMOJA WETU.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

NI KWA NAMNA GANI ROHO HUTUTAMANI KIASI CHA KUONA WIVU?

TUMEPEWA AMRI YA KUKANYAGA NGE NA NYOKA.

KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments