Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?

Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?

SWALI: Kwanini Musa aliagizwa awaambie wana wa Israeli watengeneze madhabahu kwa mawe yasiyochongwa? Kwanini yawe mawe yasiyochongwa?


JIBU: Tusome vifungu vyenyewe;

Kutoka 20:24 “….. kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia.

25 Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi”.

Kumbukumbu 27:5 “Na huko umjengee madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake.

6 Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake;

7 ufanye na sadaka za amani, ukale huko; nawe furahi mbele za Bwana, Mungu wako”.

Yoshua 8:30 “Ndipo Yoshua alijenga madhabahu kwa Bwana, Mungu wa Israeli katika mlima Ebali.

31 Kama Musa, mtumishi wa Bwana, alivyowaamuru wana wa Israeli, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo mtu hakutumia juu yake chombo cha chuma; nao wakatoa juu yake sadaka za kuteketezwa kwa Bwana, na kuchinja sadaka za amani”.

Shalom,

Madhabahu sikuzote inasimama kama kiunganishi cha kufikisha maombi yetu, dua zetu, sadaka zetu na shukrani zetu kwa Mungu, na pia inasimama kama nyenzo ya sisi kuwasiliana na Mungu. Ni kama tu mnara wa simu, mahali ambapo hapana mnara unaorusha mawimbi ya sauti mbali, kamwe hatuwezi kuwasiliana haijalishi simu zetu zitakuwa za kisasa kiasi gani.

Sasa kwenye agano la kale madhabahu zilikuwa zinatengenezwa kwa kupanga mawe kuanzia chini, mpaka kimo fulani, na kisha juu ya mawe hayo zinapangwa kuni kavu, na juu ya kuni hizo panawekwa sadaka ya kuteketezwa ambayo ilikuwa ni aidha Wanyama au ndege, na sadaka hiyo inachomwa na moshi kupanga juu..

Hivyo katika agano la kale Wana wa Israeli walipewa maagizo kwamba mahali popote atakapopachagua Mungu ili wamjengee  madhabahu ya mawe ni sharti kwamba wasitumie ujuzi wao katika kuitengeneza, hii ikiwa na maana kuwa wakikutana na jiwe ambalo limezidi kimo kidogo katika ujenzi wao, walitumie hilo hilo, wasilichonge kulipunguza, wakikutana na lilililopungua vilevile walitumie hilo hilo, wasilichonge wala kulipiga nyundo, vinginevyo madhabahu hiyo itakuwa batili.

Sasa hicho kilikuwa ni kivuli cha jinsi madhabahu halisi ya Mungu itakavyokuja kujengwa katika agano jipya. Mungu aliwapa maagizo hayo kufunua madhabahu halisi ya agano lililo bora itakavyokuja kuwa.

Na YESU KRISTO ndiye madhabahu yetu kwasasa. Yeye ndio kiunganishi chetu sisi na Mungu.

Na tunamuunda kama madhabahu yetu kwa namna mbili;

Namna ya kwanza ni pale tunapokuwa kanisani, tunapokusanyika pamoja sisi tuliookoka, sasa kule kuja pamoja ni sawa na tunavileta viungo vyote sehemu moja na hapo mwili wa Kristo unaumbika, na Kristo mwenyewe anakuwepo, na madhabahu inatokea, Hivyo tunapokutanika ni wajibu wetu kujua kuwa karama zinatolewa na Mungu mwenyewe na si wanadamu..Pale tunapozizuia karama za Roho kujidhihirisha katikati ya viungo vya Kristo (mawe), badala yake tukaweka uongozi ambao tunaouna unafaa mbele ya macho yetu wenyewe na si mbele za Mungu, tunaweka vyeo vya kibinadamu vituongoze, vyeo vya kisiasa n.k…ni sawa na tumechonga mawe hayo wenyewe, na hivyo madhabahu hiyo inakuwa najisi mbele za Mungu. Uweza wa Mungu haushuki mahali hapo.

Na namna ya pili  ni tunaijenga sisi wenyewe (binafsi),

Pale tunapokuwa peke yatu aidha nyumbani, au mahali pa utulivu kuwasiliana na Mungu, ni lazima madhabahu iwepo na hiyo si nyingine zaidi ya Yesu Kristo moyoni mwetu, yeye ndiye jiwe ambalo halijatiwa unajisi kwa dhambi yoyote, halijachongwa na mwanadamu yoyote halijachongwa kwa siasa au kitu kingine chochote,

Hivyo ikiwa umempokea Yesu moyoni mwako na umebatizwa na umepokea Roho Mtakatifu, tayari Yesu kashaingia moyoni mwako na kuweka makao, na hivyo madhabahu imeshatokea, basi maombi yako, dua zako, sadaka zako zina uhakika kumfikia Mungu..Lakini ukiyachonga mawe yako mwenyewe, yaani unaenda mbele za Mungu kwa kumuonyesha matendo yako, uungwana wako, uzuri wako, sadaka zako unazozitoa na huku Kristo umemtupa nje, hana nafasi kabisa katika moyo wako, hapo unafanya kazi bure ndugu yangu. Mungu hapokei uso wa mwanadamu yeyote, anapokea uso wa Yesu Kristo tu.

Hivyo ni wajibu wetu kujua kuwa madhabahu sahihi inajengwaje mioyoni mwetu, na katika kanisa.. Tusipende karama za kuchonga, tusijitumaishe na matendo yetu na huku Yesu yupo mbali na sisi.

Kama bado upo katika dhambi ni heri umgeukie yeye leo kwasababu yeye ndiyo jumla ya mambo yote hapa duniani. Bila yeye leo hii dunia ingekuwa imebakia kuwa historia tu, hivyo na wewe usisibiri uwe historia siku za usoni, Mpe Yesu maisha yako leo ayaokoe, upokee uzima wa milele. Usidhani utaweza kushinda haya maisha bila Yesu. Hilo halipo, wala halijawahi kuwepo.

Wokovu unakuja kwa kumwamini Yesu, na  kutubu dhambi zako, kisha kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa Jina la YESU KRISTO,(Matendo 2:38, Matendo 8:16), Kama hujabatizwa na unahitaji kufanya hivyo, utawasiliana nasi inbox, au tutafute katika namba hii +255789001312.

Bwana akubariki.


Mada Nyinginezo:

TAFUTA KUWA NA AMANI NA WATU WOTE.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

YESU ANA KIU NA WEWE.

Nasaba ni nini kibiblia?(1Nyakati 9:1, Tito 3:9)

Kuna Mbingu ngapi?

Ni uthibitisho upi unaoonyesha kuwa kuna MBINGUNI na KUZIMU?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments