YESU ANA KIU NA WEWE.

YESU ANA KIU NA WEWE.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tuyatafakari maandiko pamoja.

Kama tunavyojua hakuna wokovu kwa mwingine yoyote, isipokuwa kwa Bwana wetu Yesu, haijalishi dunia itasema nini, haijalishi imani nyingine zote zitasema nini lakini ukweli upo pale pale, Kristo alikufa, akafufuka, akapaa mbinguni na sasa YU HAI.. Na yupo pamoja na wale aliowaita akitembea nao mpaka ukamilifu wa Dahari. Na wote wamtumainiao, ni kama mlima wa Sayuni, hawatatikisika kamwe, wanadumu milele..(Zab.125:1).

Kuna tukio lililotokea pale msalabani..ambalo liliwashangaza wengi…Lakini kabla hatujalizungumzia hilo jambo hebu tuyazungumzie kwanza mateso ya Bwana wetu Yesu pale msalabani.

Siku ile ya mateso ya Bwana, bila shaka mimi na wewe tungekuwepo pale..tungemwaga machozi yasiyokuwa ya kawaida ya uchungu kwa jinsi alivyojeruhiwa…Biblia inasema “uso wake uliharibiwa sana kuliko watu wote”( Isaya 52:14), wengi wetu ng’ombe wakati anachinjwa tu hata hatudhubutu kutazama, ajali ikitokea mahali, hata hatudhubutu kuzitazama zile maiti, mwizi akipigwa tu na kuingizwa kwenye tairi achomwe, hisia tunazozipata hazielezeki……Sasa siku ile Bwana anasulubiwa laiti tungekuwepo wengine tungezimia.

Kwanza jana yake hakulala usiku kucha, alikuwa akizungumza na wanafunzi wake na kuwapa wosia mrefu, na kuomba… mpaka ilipofika alfajiri jogoo wa kwanza anawika, alikuwa tayari kashashikwa na wale maaskari, kulipopambazuka tayari alikuwa ameshateswa vikali, wakaanza kumtembeza na kumwangaisha, kwa miguu kutoka kwa mfalme huyu kwenda kwa huyu…kutoka kwa Pilato kwenda kwa Herode, halafu anarudishwa tena kwa Pilato, huku kichwani anataji ya miiba..na huku anapigwa na kutemewa mate…Baadaye anapewa msalaba aubebe…na apande nao Golgotha…Pale Golgotha ni eneo la kilima kirefu…Mwili wote ulikuwa umeshaishiwa nguvu hata kutembea alishindwa ikabidi asaidiwe ule msalaba.

Na baadaye akitundikwa msalabani…Damu ilimwagika nyingi na mwili uliishiwa nguvu na maji.

Sasa Yule Yesu aliyesema maneno haya….

“Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure! (Ufunuo 21:6)”

Na tena aliyesema maneno haya…..

Yohana 7:37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, MTU AKİONA KİU, NA AJE KWANGU ANYWE.

38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake”.

Na leo hii anakuja kusema maneno haya…

Yohana 19:28“Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, NAONA KİU”

Ni jambo la kushangaza kidogo! Ambalo hata sisi tunaweza kulihoji..Siku chache nyuma alisema “wote wenye kiu waje kwangu kunywa maji, na leo anasema ANAONA KIU, yaani anataka sisi ndio tumpe maji??”..Bila shaka huyu anaweza kuwa amerukwa na akili… Na kweli! Anavyoonekana ameshochoka na kakauka mwili, ni lazima atataka maji ya kunywa tu!..bila shaka wengi walicheka na kubeza…Na ili kumkomoa kabisa wakampa SIKI, ili ikaushe maji yote mwilini, ili ASIKIE KIU KISAWASAWA.

Lakini baadaye kidogo kuna jambo lilitokea lililowashangaza na kuwabadilisha mitazamo yao…na wengine waliokoka pale pale..

Ule mwili waliounyesha siki!, Ule mwili uliokuwa umeonekana umekauka maji yote, na damu yote…Ule mwili ulioonekana umekufa kwa KIU kikali na kwa KUMWAGIKA DAMU nyingi, na kwa maumivu makali…dakika chache baadaye, ULIMWAGA LITA KADHAA ZA MAJI MBELE YA MACHO YAO. Ndipo walipojua kuwa huyu Mtu alikuwa hasikii KIU cha MAJI, bali alikuwa anasikiu kingine.

Hebu tusome kidogo..

Yohana 19:32 “Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye.

33 Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;

34 lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; NA MARA İKATOKA DAMU NA MAJİ.

35 Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki”.

Achana na zile picha unazoziona kwenye tamthilia, kimchirizi kidogo tu cha maji kinatoka ubavuni mwa Bwana.. Haikuwa hivyo ndugu!…ingekuwa hivyo huyu askari, asingeokoka hapo!..Pale maji yaliyotoka ni mengi mno, na yalitoka kwa presha nyingi..ndio maana askari huyu aliamini pale pale, kwasababu alishachoma maiti nyingi lakini kwa hiyo ya Bwana kwake lilikuwa ni tukio jipya.

Ndipo wale askari walipojua kuwa Yesu Kristo ni chemchemi ya Maji yaliyo hai..Na pale hakuwa anasikia kiu cha maji yao, bali kiu cha kuwapa wao maji ya uzima!…Na pale pale msalabani akaanza kuwapa, wakanywa yale maji, nao pia wakatoka kwenda kushuhudia habari za mwokozi.

“Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki”

Na leo hii Kristo yu hai, na tangazo lake ni lile lile…

Ufunuo 21:6 “Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure!”

BWANA ANA KIU NA WEWE NDUGU…ANA KIU YA KUKUPA WEWE MAJI YA UZIMA. Maji haya aliyatoa baada ya kupigwa kwake, Ndio shauku yake kuona unayapata hayo maji, anakuona una kiu, hivyo anataka kuikata hiyo kiu…Una kiu ya kupata furaha, yeye anayo furaha, una kiu ya kupata amani, yeye anayo amani, una kiu ya kupata raha, yeye anatoa raha (Mathayo 11:28), Una kiu ya kuthaminika, yeye anaweza kukuthaminisha…Anatamani kukupa hayo yote kuliko wewe unavyotamani.

Hivyo unachopaswa kufanya ni kumkaribisha tu katika maisha yako kama bado hujafanya hivyo, na unafanya hivyo kwa kutubu na kuziacha dhambi zako, kwa moyo wako wote, ili umsafishie sehemu ya kuwekea maji atakayokupa…Na ukishatubu, tafuta ubatizo sahihi wa kimaandiko ambao ni wa maji tele na wa kuzamishwa kwa jina la Yesu, na baada ya hapo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako, kukusaidia kuishi maisha yanayompendeza yeye pamoja na kukupa zawadi zote hizo hapo juu…Atakata kiu yako kwa namna ambayo utashangaa wala haihitaji mtu kukuhadithia.. Wewe onja tu!maji ya Bwana halafu utakuja kutoa ushuhuda mwenyewe…

Zaburi 34:8 “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

MASHAHIDI 40 WALIOUAWA MJINI SEBASTE, NI UJUMBE KWETU.

JIEPUSHE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

USO WAKE ULIKUWA UMEHARIBIWA SANA ZAIDI YA MTU YE YOTE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Napenda sana mafundisho yako
0763518736
Kamanakilagalila36@gmail.com

luzalia
luzalia
3 years ago

Ningependa kupata watsap mafundisho haya namba ni 0622491873

Rogath
Rogath
3 years ago

Amina. Bwana azidi kukubariki.