WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

Shalom, jina la mfalme mkuu Yesu Kristo libarikiwe daima.Kama ukisoma kitabu cha Waebrania sura ile ya 11 yote, Utaona Mtume Paulo, akiwaelezea kwa mapana wale mashujaa wa Imani (Wingu kubwa la mashahidi) kuanzia wakati wa Habili kuelekea kwa Nuhu, mpaka kwa Ibrahimu, na manabii , jinsi walivyoipagania na kuishindania imani kwa ujasiri wote,..

Waebrania 11:4 “Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini…Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako…Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu….

24 Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;

25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;

26 akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo…..

36 wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;

37 walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;”

Wote hawa ni mashujaa wa Imani na Mtume Pauloa alianzana na utangulizi huo wa mashujaa hao ili mwishoni aufikishe ujumbe aliokuwa anataka kuufikisha, na ujumbe wenyewe tunausoma katika sura inayofuata..

Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,

2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu”.

Unaweza ukaona hapo lengo kubwa la Paulo kuwataja wale, ni ili kuwatia watu hamasa, kwamba wapige mbio kwa bidii kama wale walivyopiga…Kama wale walivyoshinda nao wao pia washinde, wapate wivu, hivyo kama kuna mizigo yoyote ya dhambi inayowalemea waitupe chini wapige mbio kwa saburi katika mashindani ya imani yaliyowekwa mbele yao.

Hivyo na sisi pia tumeona, tuanze kuandika, shuhuda mbali mbali za mashujaa wa Imani ambao habari zao zimethitishwa katika historia kuwa ni kweli.. wale ambao habari zao hazipo kwenye biblia, lakini utumishi wao wa injili umethibitishwa na maisha yao kwa ujumla.

Tunaandika hivyo ili kusudi na sisi ambao tunalegalega, tujifunze kwa wale, na vilevile tukijua kuwa ipo siku tutasimamishwa pamoja na wao kwenye viti vya hukumu kutoa hesabu ya mambo yetu yote tunayoyafanya sasa hivi duniani..Hivyo basi na sisi kwa kuwatazama hao tupate nguvu ya kukaza mwendo katika safari yetu ya wokovu na kuweka kando kila mzigo wa dhambi.

Leo kwa Ufupi tutamwangalia mtu mmoja anayeitwa JOHN WESLEY.

Baadhi yetu tunamfahamu, kama muasisi wa makanisa ya ki-Methodist. Huyu alizaliwa huko Epworth, nchini Uingereza mwaka 1703. Akiwa ni mtoto wa 15 kati ya watoto 19 waliozaliwa katika familia yao. John Wesley alianza kuwa na kiu ya kumtafuta Mungu tangu akiwa mdogo. Lakini ndoto zake za kuifanya kazi ya Mungu zilikuja kutimia baada ya kuhitimu chuo Oxford,alipokuwa chuoni Oxford ndipo Bwana alipoanza kuyabadilisha maisha yake kwa kasi ya ajabu. Baada ya hapo yeye na kaka yake aliyeitwa Charles waliunda kikundi cha kikristo pamoja na wenzao wawili chenye kauli mbiu ya “Kuishi maisha kama Kristo aliyoishi”, kuliko kuishi maisha ya kidini, safari yao ilianza kidogo kidogo walianza kwenda kuwatembelea wagonjwa mahospitalini, na wafungwa, na kuwahurumia maskini, n.k na kujifanya wao wenyewe kuwa vielelezo(njia ya kufuata) hivyo wakajiundia utaratibu wa kiroho ambao waliuita “(METHOD yaani NJIA”)..na kuanzia huo wakati wakazoeleka kuitwa WAMETHODISTI. Methodist ilivyoanza na akina Wesley sivyo ilivyo leo…Leo hii imebakia kuwa ni dini tu kama zilivyo dini nyingine. Katika safari yao walikumbana na vipingamizi vikali vya wakuu wa dini..lakini walishinda safari yao..

Baada ya hapo Wesley na wenzake Bwana aliwagusa kwa namna ya kipekee, wakaona umuhimu wa kwenda kufanya kazi ya umishionari duniani kote. Hapo ndipo injili ikaanza kupelekwa duniani kote kwa nguvu, kasi na kwa bidii ya ajabu hata zile sehemu ambazo zilikuwa ngumu kufikiwa kama Afrika zilifikiwa na nuru ya neno la Mungu. Huo ndio ule wakati wamisionari wengi walisafiri mabara ya mbali kama vile Asia na Afrika na Amerika ya kusini kusambaza injili. Walilenga kufundisha UTAKATIFU, Kama ndio nyenzo muhimu ya mtu kuokolewa sawasawa na (Waebrania 12:14 inayosema.. “ Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”).

John Wesley daima alikuwa anatumia farasi wake kwenda kuhubiri injili, inakadiriwa mwendo aliozunguka na farasi kuhubiri sikuzote za maisha yake ni zaidi ya Km laki 4 ambayo ni sawa na kuizunguka dunia mara 10 kwa farasi..Nyakati hizo magari na ndege hizi tulizonazo hayakuwepo.

Wesley alikuwa ni mtu aliyeimarika kiroho sana, anasema hakumbuki kama alishawahi kupungua nguvu rohoni hata kwa robo saa tangu siku aliyozaliwa. Alisema hakuwahi kulala zaidi ya masaa 6 siku zote za huduma yake, kila siku alikuwa akiamka saa 11 alfajiri, na kwenda kuhubiri zaidi ya mara nne kwa siku, ili kwamba kwa mwaka afikishe kwa wastani wa mafundisho 800.

Mtu kama huyu kama angekuwa na usafiri tulio nao leo hii wa haraka kama gari au ndege angeshaizunguka dunia mara ngapi kuhubiri? Lakini sisi tunaokila kitu hatuwezi, Bwana atusaidie sana..

Kama ulikuwa hufahamu huyu ndiye mjumbe wa kanisa la 6 lijulikanalo kama Filadelfia linalozungumziwa katika kitabu cha Ufunuo 3.. Na hili ndio kanisa pekee ambalo Kristo alilisifia kwa matendo yake mema,

Ufunuo 3:7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.

8 Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.

9 Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda.

10 Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.

11 Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.

Yeye ndiye aliyechochea moto wa injili ya Kristo kupelekwa ulimwenguni kote, na wale walioshirikiana naye walifanya kazi kama yeye aliyoifanya…Wakati sisi waafrika tunaabudu miungu na kufanya matambiko ya kichawi, watu kama hawa walijitoa kwa hali na mali kutoka katika bara la Ulaya kama wamisionari kuja kutuletea sisi mwanga wa Injili. Na sisi je! tunafanya kipi ili kuwapelekea wengine injili?.

Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,

2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu”.

Bwana akubariki.. Tutaendelea na mashujaa wengine wa Imani kwa jinsi Bwana atakavyotupa neema…


Mada Nyinginezo:

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA TATU WA YOHANA.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

NUHU WA SASA.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:

JE ADAMU ALIKUWA NA KITOVU?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments