PENDA KUHAKIKI MAMBO KABLA YA KUYAAMINI

PENDA KUHAKIKI MAMBO KABLA YA KUYAAMINI

 

Jina la Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe sana, karibu tujifunze biblia neno la MUNGU wetu (Zab 119:102).

Siku zote penda kuhakiki jambo kabla ya kuliamini, au kulipokea.. Taarifa yoyote inayokufikia, au unayoihisi kabla ya kufanya maamuzi ya kuamini au kutenda jambo, fanya uhakiki kwanza, Desturi ya kuhakiki jambo sio “kukosa imani” kama inavyoaminika na wengi bali ndio kipimo cha “ukomavu”.

Katika Biblia tunajifunza kwa MUNGU wetu kuwa naye pia ni Mungu wa kuhakiki mambo.. kwamfano zile taarifa za maovu ya watu wa Sodoma na Gomora zilishatangulia kumfikia, lakini kabla ya kufanya maamuzi ya kuiangamiza miji ile pamoja na watu wake, alishuka kwanza yeye mwenyewe kuhakiki kwa kile kilichotangulia kumfikia.

Tusome habari..

Mwanzo 18: 20 “Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana,

21 BASI, NITASHUKA SASA NIONE KAMA WANAYOTENDA NI KIASI CHA KILIO KILICHONIJIA; NA KAMA SIVYO, NITAJUA.

22 Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana”.

Kupitia habari hiyo sio kwamba Bwana MUNGU alikuwa hayaamini masikio yake, wala malaika wake wala mashitaka yoyote yaliyopandishwa mbele zake juu ya watu wa Sodoma na Gomora, alikuwa anawaamini sana, lakini ilibidi yeye mwenyewe akahakiki ukweli na uzito wa mambo, ili hukumu yake iwe ya haki na kweli.

Ni mara ngapi umesikia habari za mtu fulani kuwa yuko hivi au yuko vile, na kabla haujachukua maamuzi juu yake umelifuatilia kwa undani uhakika wa maneno hayo?.. utaona kuwa ni mara chache sana.. Wengi tunaziamini sana taarifa za kuambiwa au kusimuliwa na si zile tulizozithibitisha wenyewe.

Tunapenda kuthibitishiwa mambo na si kuyathibitisha wenyewe, ni mara ngapi umefuatilia ukweli wa mambo kuhusu Mke wako kwa yale unayoyasikia?, au ya mume wako, au ya watoto wako au wazazi wako?.

Tumewahi kukutana na visa vya watoto kuaminishwa kuwa wazazi wao ni wachawi kwa maneno tu!, au kwa ndoto tu, na mwisho kuishia kuwachukia na kuwatenga wazazi wao jambo linalofunga Baraka na neema kwa mtoto asilimia mia moja.

Jifunze kuhakiki mambo yote, hata yale ya kiMUNGU, si kila hubiri ni la kuliamini au kulipokea asilimia zote bila kulihakiki, Ondoa ile desturi ya kuamini kila kitu, ndio tunajiandaa kuamini lakini si kuruhusu kuamini kila kinachotujia.

Kuhakiki mambo si dhambi.. Na kipimio kizuri cha kuhakiki mambo ni NENO LA MUNGU, kama wale watu wa Beroya.

Matendo 17:10 “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.

11 Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo”.

Ukiwa na uwezo mkubwa wa kulijua NENO la MUNGU, utakuwa na uwezo mkubwa pia wa kuhakiki mambo, kwani Neno la Mungu (Biblia) ni kitabu kulichojaa mafunzo ya kila aina ya maisha.

Ukitaka kuhakiki ndoto unazoziota kama ni halisi au batili, Biblia pekee ndio kipimio chako, ukitaka kuhakika fundisho au hubiri unalolisikia kama ni halisi au gugu, ni Biblia tu, ukitaka kuhakiki njia yako ya kiroho, kibiashara, au kielimu kama ni sahihi, ni Biblia tu.

Ukitaka kuhakiki mke, au mume au mtoto kama yupo katika njia sahihi au sio sahihi ni Biblia, ukitaka kuhakiki taarifa za unazozijua kama ni njema au za kupotosha ni Biblia tu.

Biblia ndio kitabu cha Maisha, imejaa hekima, maarifa, mwanga, mashauri, na maelekezo sahihi ya maisha, ikiwemo majibu ya maswali magumu, Biblia pekee ndio kitabu kinachoelezea mambo yajayo kwa usahihi kwa mtu mmoja mmoja, au kundi na hata Taifa na Dunia kwa ujumla.

Ndio kitabu pekee ambacho ukikisoma ni kama yupo mtu mwingine pembeni yako anakusemesha, tofuati na vitabu vingine vyote, ndio kitabu pekee chenye taarifa zisizofifia uhalisia kwa jinsi muda unavyozidi kwenda.

Anza uhakiki wa mambo leo kwa kusoma Biblia, sauti ya MUNGU iliyo wazi.

Ikiwa utahitaji kusaidiwa mwongozo wa usomaji wa Biblia, basi waweza wasiliana nasi kwa namba hizi 0789001312.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAMBO MANNE(4) YAFANYAYO NENO LA MUNGU.

NENO LA MUNGU NI UFUNUO MKAMILIFU.

Ipi tofauti ya Juhudi na bidii kibiblia. (Warumi 12:11)

Tofauti kati ya maandiko na Neno ni ipi?

Mgawanyo wa Vitabu vya Biblia

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply