PALE ADUI YAKO, ANAPOKULETEA ZAWADI YA UPENDO.

PALE ADUI YAKO, ANAPOKULETEA ZAWADI YA UPENDO.

Sauli alikuwa ni adui mkubwa sana wa Daudi, kiasi cha kumfanya maisha yake yote yawe ni mafichoni tu na ugenini kwa miaka mingi. Lakini cha ajabu ni kuwa uadui aliokuwa anauongeza kwa Daudi, uliongeza pia upendo mwingi kwa Daudi kupitia mwanawe Yonathani.

1 Samweli 19:1-2

[1]Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi.

[2]Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha;

1 Samweli 20:17

[17]Naye Yonathani akamwapisha Daudi mara ya pili, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake; kwa maana alimpenda kama alivyoipenda roho yake mwenyewe.

Upendo ambao Daudi mwenyewe baadaye anashuhudia ulizidi upendo wa mwanamke..

2 Samweli 1:26

[26]Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa ukinipendeza sana;

Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa wanawake.

Naam, Familia moja inatoa uadui uliozidi na wakati huo huo inatoa upendo usio na kifani.

Na hatimaye upendo ukazidi nguvu uadui wote..

Popote unapojikuta hupendwi, unapigwa vita, unatendewa mabaya, unaonewa wivu, bila sababu yoyote, fahamu kuwa hapo pia pana upendo mwingi sana nyuma yake uliojificha.

Kwanini pengine huuoni?

Ni kwasababu unashindana na maadui zako badala ya kuwaombea mema. Mwangalie Daudi hakudhubutu kushindana na bosi wake, ijapokuwa alijua anawindwa naye ili auawe, hata yule mtu aliyejifanya amemuua mfalme, Daudi hakufurahishwa naye, kinyume chake alimwua huyo, hata alipothibitisha kifo mfalme Daudi hakucheka bali aliomboleza na kulia.

Hatimaye Mungu akampa zawadi ya upendo kupitia mtoto wa huyo huyo adui yake, ndiye Yonathani.

Hii ndio sababu kwanini Bwana Yesu anasema wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi. Kwasababu ndani yao pia upo upendo mwingi sana usiouona.

Mathayo 5:43-44

[43]Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;  [44]lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

Ikiwa ni boss wako, anakupiga vita mwombee kwa kuugua kabisa, sio kinafki mnyororo ulio nyuma yake utakupenda kwa upendo mkuu, unaorudisha kwake.

Mungu anapenda, tuitafute amani kwa bidii zote(Waebrania 12:14). Je! Unamwona adui yako kwa jicho lipi?

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply