ALIJARIBIWA SAWASAWA NA SISI KATIKA MAMBO YOTE.

ALIJARIBIWA SAWASAWA NA SISI KATIKA MAMBO YOTE.

Alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote!!


Waebrania 4:14 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu.

15 Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi”.

Neno la Mungu linaposema, alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote..Linamaanisha kweli ni katika mambo yote, Kama ni njaa, Bwana Yesu anaielewa vizuri na alishawahi kuionja, kama ni kuumwa Bwana Yesu anaelewa vizuri nini maana ya kuumwa, Yeye alipoishi hapa duniani hakuwa kama kiumbe cha kipekee ambacho hakijawahi hata siku moja kujua shida tangu kuumbwa kwake, kwamba hajawahi kuisikia hata maumivu ya kichwa tangu kuzaliwa kwake hadi kufa kwake hapana, pale msalabani maumivu makali aliyokuwa anayasikia ni zaidi ya ugonjwa wowote duniani..

Kama ni kuwa na maadui yeye naye alikuwa nao wengi..Kama ni kuonekana si kitu alionekana sana mbele ya macho ya watu wengi (Soma Isaya 53), kama ni misiba yeye naye alipitia ya kufiwa na ndugu zake, ni vile tu biblia haiwezi kuandika habari zake zote..Hivyo hakuna jambo lolote au shida yoyote unayoipitia leo hii Bwana wetu YESU KRISTO asiielewe.

Na ndio maana tunamshukuru Mungu kwa ajili yake, kwasababu, pale tunapomwomba au kumlilia shida zetu tunajua kuwa ni mtu anayeelewa vizuri tunachokiomba kwake..Tofauti yake na sisi ni kwamba yeye katika majaribu hayo yote aliyoyapitia hakuwahi kutenda dhambi hata moja. Kwahiyo nataka nikutie moyo ndugu uliyemwamini Kristo, ujue kuwa umepata mwokozi kweli kweli anayoijua hali yako, Ni sawa na mtu ambaye alikuwa ni yatima akapitia maisha ya kuishi mtaani, chakula chake kilikuwa ni majalalani, kulala kwake ni kwenye mabaraza ya watu, lakini ikatokea siku moja kwa bahati tu akaokota almasi yenye thamani ya bilioni 5, akatajirika akawa maarufu sana katikati ya matajiri,(huo ni mfano tu!). wewe unadhani ni rahisi mtu huyo kuwasahau wale mayatima wenzake aliokuwa anahangaika nao mitaani? Kama ingekuwa hayajui hayo maisha isingekuwa rahisi kwake kuwajali, lakini kwasababu ameyapitia ni ngumu kuwasahau ndugu zake..

Hivyo Na wewe usiogope jaribu unalopitia sasa hivi kwasababu Kristo yupo pembeni yako kukusaidia anaelewa vizuri hali yako huhitaji hata kumweleza.. Yupo amesimama mbele za Mungu kama kuhani mkuu, kukuombea wewe.. Hivyo kaa ukijua tu, hata kama liwe bonde zito namna gani la mauti unalolipitia, ujue kuwa hatakuacha daima, yupo hapo kuhakikisha anakupigania, litadumu kwa kitambo tu, lakini nalo litapita.

Lakini kama wewe upo nje ya Kristo, fahamu kuwa kwa nguvu zako hutaweza kuyashinda mawimbi ya ibilisi katika huu ulimwengu.. Kristo hawezi kuwa mwombezi wako pale unapokwama, kwasababu hujataka awe rafiki yako.

Ukimkaribisha ndani ya moyo atakugeuza, na kuyaumba maisha yako upya tena. Atatembea na wewe, vilevile atakupa tumaini la uzima wa milele. Kwamba hata ukifa leo unaouhakika wa kwenda mbinguni. Lakini kama utautumikia ulimwenguni, ukifa leo huo ulimwengu umekuahidia nini baada ya hapa?. Yesu ni upendo anatupenda sote sawasawa wala hana ubaguzi, ukija kwake atakupokea haijalishi ni dhambi nyingi kiasi gani ulizowahi kufanya huko nyuma.

Anachotaka kwako ni moyo wa toba. Na ni kwanini utubu, kwasababu anataka kuanza na wewe ukiwa na dhamiri safi moyoni mwako. Unatubu kwa kumwomba msamaha, pili kwa kuacha yale mambo ambayo ulikuwa unayafanya huko nyuma.. Ukishafanya hivyo kwa moyo wako wote, kwasababu Mungu anaangalia moyo.. Basi Kristo saa hiyo hiyo atakuja na kufanya makao ndani yako.

Uthibitisho kuwa Yesu amekuja ndani yako na kufanya makao, ni kuwa utaona badiliko kubwa ndani yako, utaona shauku Fulani ndani yako, utaona amani Fulani ndani yako. Basi ujue kuwa Kristo ameshakuokoa na ameshakuja kufanya makao na wewe.

Lakini hiyo peke yake haitoshi..Unapaswa ukaukamalishe wokovu wako kwa kubatizwa ili kumpa Ruhusa Roho Mtakatifu kuja kufanya makao halali ndani yako. Hivyo nenda kabatizwe katika ubatizo sahihi, ambao ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi(Yohana 3:23) na kwa jina la YESU KRISTO sawasawa na (Matendo 2:38,8:16,10:48, 19:5).

Ukifanya hivyo kwa moyo wako wote basi wewe ni mwana wa Mungu, Hivyo Kristo atakuwa na wewe kukulinda dhidi ya Yule adui na yeye mwenyewe atakupa dawa ya misukosuko mingi ya huu ulimwenguni inayowatesa wanadamu wengi,.

Bwana akubariki sana.

Mada Nyinginezo:

HERI NINYI MLIAO SASA, KWA SABABU MTACHEKA.

NGUVU ILIYOPO KATIKA MAAMUZI.

YESU MPONYAJI.

NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments