HERI NINYI MLIAO SASA, KWA SABABU MTACHEKA.

HERI NINYI MLIAO SASA, KWA SABABU MTACHEKA.

heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka.

Shalom, Jina la Bwana YESU libarikiwe. Ni siku nyingine tena, Bwana ametupa pumzi yake ya uhai, hivyo hatuna budi kumshukuru kwa hili, haijalishi tu wagonjwa kiasi gani, au tunapitia katika magumu kiasi gani, maadamu tu! pumzi ipo basi tumsifu Mungu.

Leo tutaangazia ni Kwanini biblia mara kwa mara inatumia semi kama hizi: “heri leo”… “maana baadaye”…..

Hiyo inatuonyesha kuwa kile tunachopita leo hii, basi kinyume chake ndicho tutakachokipitia baadaye..Kuna kanuni fulani Mungu ameziweka katika vitu vya asili ambavyo tukivichunguza vizuri tutapata picha ya mambo yanayoendelea rohoni..Kwa mfano kuna wakati utaona muda mfupi kabla mvua kunyesha joto huwa linaongezeka kwa ghafla na kuwa kali sana pengine dakika tano au 10 hivi.. na baada ya hapo mvua kubwa inashuka yenye upepo na baridi…

Au wakati mwingine wa jioni jua linapokaribia kuzama, utagundua kuna nuru inaongezeka kiasi fulani kwa jinsi isivyo ya kawaida kisha baada ya dakika chache tu giza linakuja kuu.

Hiyo inatuonyesha kuwa kabla ya jambo fulani zuri au baya kutokea huwa kinatangulia kilicho kinyume chake..

Na ndivyo hata katika mambo ya Mungu, sikuzote Mungu kabla hajambariki mtoto wake yeyote ni lazima kwanza apitie hali fulani ya uhitaji au dhiki ili aweze kukimudu kile alichomwandalia kule mbeleni.Ndivyo alivyofanya kwa Yusufu ndivyo alivyofanya kwa wana wa Israeli kule jangwani, na ndivyo alivyofanya kwa Ayubu,..ndivyo alivyofanya kwa Nebukadneza, na ndivyo atakavyofanya kwa mtoto wake yeyote yule atakayemwita..

Na ndio maana Bwana Yesu alisema ikiwa unapitia huzuni sasa, kwa ajili ya Imani yako, hajalishi ni katika afya yako,au katika uchumi wako maadamu wewe ni mkristo, basi fahamu kuwa ipo faraja kubwa Mungu kaiweka hapo mbele kwa ajili yako ..Hivyo usiogope..afya tele ipo mbele yako, vicheko tele vipo mbele yako, chakula tele kipo mbele yako.

Mathayo 5:4 “Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika”

 

Luka 6:21 “Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba.

Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka”

Ukiona leo, unayo kiu ya kuyasikia maneno ya Mungu, na unatamani kumfahamu sana Mungu kwa viwango vya juu…Basi usiogope kuonekana umerukwa na akili sasa, au mtu wa itikadi kali…fahamu tu kuwa hapo mbeleni hiyo kiu haitakuwepo tena, na utamfahamu Mungu kwa viwango ambavyo si vya kawaida vya yeye anavyotaka umjue yeye, utazamishwa katika vilindi vya moyo wa Mungu, na kuonyeshwa mambo ambayo ni makubwa na magumu wanadamu wasiyoyajua..

Ukiona leo unachekwa na kudharauliwa na kuonekana kuwa wewe ni takataka kwasababu umeamua tu kumfuata Kristo basi ujue kuwa hapo mbeleni kuna kuheshimiwa na kuogopwa, na kutukuzwa kwa ajili ya Jina la YESU KRISTO.. Hiyo ndiyo kanuni..

Ukiona leo umeacha kila kitu, umekuwa tayari kupoteza hata kazi yako, au biashara yako, au mali zako, au elimu yako au hadhi yako kwa ajili ya Yesu au kwa ajili ya Injili ya Kristo isonge mbele,.. basi fahamu kuwa kupata mara 100 ya hivyo ulivyovipoteza ipo mbele yako..haijalishi itachukua miaka 5,10 au 20 au 50 lakini kabla haujafa Mungu atahakikisha amelitimiza hilo neno lake juu yako.

Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.

29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele”.

Vivyo hivyo tukiona sisi wakristo tumeupoteza ulimwengu wote.,kwa ajili kumtazama Kristo na ufalme wake wa milele, mpaka tunaonekana kama vile watu tusiostahili kuwepo katika ulimwengu huu, basi tujue kuwa,.. Huu huu ulimwengu tutaupata, maana biblia inasema dunia hii itarithiwa na wenye upole( watakatifu)..Na hiyo itatimia katika utawala wa miaka 1,000 unaokuja huko mbeleni.

Mathayo 5:5 “Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi”.

heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka

Lakini kinyume chake pia ni kweli, ukiona sasa umeupata ulimwengu wote, basi ujue tayari umeshaupoteza,..Ukiona kila aina ya ouvu duniani unaokuja wewe ni wako, disko ni zako, uzinzi ni wako, ulevi ni wako, starehe zote ni zako, rushwa ni yako,… wizi ni wako, dhuluma ni zako, tamaa za ujanani ni zako, vimini na suruali ni zako, viduku, na milegezo ni yako..uzinzi ni wako, fashion ni zako…Basi ujue kuwa safari yako ni fupi hapo mbeleni, nyakati za shida zinakuongojea..

Mathayo 16:25 “Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

27 Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake”..

Unaona? Uamuzi ni wako,.. usifurahie kuwa unayo afya nzuri sasa na huku upo mbali na Kristo,.. usifurahie unayo elimu kubwa na huku yupo mbali.., unacho hichi aunacho kile, ni mrembo ni mzuri,..fahamu kuwa Mungu ameruhusu faraja yako ikujie sasa ili wakati wa wenzako kufarijiwa wewe uwe unalia na kusaga meno..

Zaburi 62:7 “Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele”

Kama wewe upo nje ya Kristo utajisikiaje usikie unyakuo umepita leo na wewe umebaki?., wakati wenzako wanafarijiwa milele mbinguni katika ile karamu ya mwana kondoo wewe upo hapa chini ukisubiri ziwa la moto wa milele. Ni majuto kiasi gani, ukikumbuka kuwa ulishahubiriwa injili mara nyingi na ukapashupaza shingo yako.

Embu leo sema Bwana Yesu usinipite, ninakukaribisha maishani mwangu tangu sasa. Sema hivyo ukimaanisha kabisa kutoka katika moyo wako kuwa kweli kuanzia leo umeamua kumfuata yeye..Ukiwa umepiga magoti yako mwombe akusafishe dhambi zako zote kwasababu hapo ulipo yupo ili kukusikia,.. tubu kabisa hata kwa machozi, na yeye hapo ulipo atakusamehe na kukupa amani ya ajabu ndani ya moyo wako..

Ukishaona hivyo, na amani imekuja ndani yako ujue amekusamehe,..unachopaswa kufanya usihangaike hangaike na huu ulimwengu bali haraka tafuta kanisa zuri la kiroho linalomuhubiri Kristo,.. uende pale, vilevile ukiwa hukubatizwa ipasavyo unapaswa ufanya haraka sana kutimiza agizo hilo muhimu Bwana Yesu alilotupa kwa kila mtu atakayeokoka, Kwamba wote tubatizwe katika ubatizo mmoja kwa jina lake..

Zipo batizo nyingi duniani ambazo si za kimaandiko lakini ubatizo sahihi ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi (Yohana 3:23), na uwe ni KWA JINA LA YESU KRISTO sawasawa na Matendo 2:38..

Baada ya hapo Roho Mtakatifu atakutia muhuri na atakuwa kiongozi wako milele kukuongoza na kukulinda mpaka ile siku ya Unyakuo itakapofika ikiwa bado utakuwa hai.

heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka

Bwana akulinde, Bwana akubariki.

Mada Nyinginezo:

Biblia inamaana gani kusema;aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi?

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA

https://wingulamashahidi.org/2018/06/27/maswali-na-majibu/

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments