KWANINI AWE PUNDA NA SI MNYAMA MWINGINE?

KWANINI AWE PUNDA NA SI MNYAMA MWINGINE?

Kwanini awe Punda na si mnyama mwingine?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu tujifunze Maandiko.

Tunaona kipindi kifupi kabla Bwana Yesu kuingia Yerusalemu aliwatuma wanafunzi wake wakamletee Mwana-punda ili alingie naye mjini..Ipo sababu kwanini alimtumia yule mtoto wa punda na si mama yake (Mathayo 21:4-5)..lakini leo hatutakwenda kuiangalia hiyo sababu..kama utapenda kufahamu ni kwanini hakumtumia Mama-punda bali mwanae…unaweza akatuambia inbox tukakutumia ujumbe wake…

Pamoja na hayo pia ipo sababu kubwa sana ni kwanini hakutumia mnyama mwingine yoyote kama vile Farasi au Ngamia kuingia naye Yerusalemu badala yake akatumia PUNDA, kwanini awe punda.. Na hali tunajua kuwa punda si mnyama wa heshima…Walau ingekuwa ni Farasi ingeleta heshima kidogo…lakini si punda?..Tofauti na wahubiri wengi waa leo hii ambao ukiota tu punda au ukifuga tu punda licha ya kumpanda ni rahisi kuambiwa una nyota ya punda!..(utaambiwa utakuwa mtumwa milele)…

Lakini haikuwa hivyo kwa Bwana wetu Yesu,..Yeye alimpanda huku akijua kuwa yeye ni mfalme anayesubiriwa mjini, na muda mfupi tu baadaye aliimbiwa na umati mkubwa kwa shangwe na vigelegele kwamba yeye ni Mfalme!!, Hosana juu mbinguni..watu walitandika mavazi yao chini na kukata matawi ya miti na kuyatandaza chini, Mfalme mkuu juu ya punda apite, na kumwimbia…Mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana!..Hivyo punda sio mnyama wa laana kama upotovu uliozagaa leo….

Tabia ya Punda;

Hivyo kuna ufunuo hapo kwanini awe ni punda Bwana Yesu alimtumia na si mnyama mwingine..Na leo tutajifunza kwa ufupi siri hiyo, ambapo tukishaijua tutafahamu ni jinsi gani KRISTO alikuwa ni chombo ya muhimu sana kwetu.

Pamoja na tabia nyingine nyingi Punda alizonazo…lakini anayo tabia moja kuu ambayo imewazidi Wanyama karibia wote..Na tabia hiyo ni tabia ya KUHISI HATARI ILIYOPO MBELE, AU KUHISI KITU KINACHOKUJA MBELE…Chochote cha heri au cha shari kinachokuja mbeleni Punda ni mwepesi sana kukihisi…Jambo ambalo litamfanya aidha Agome kuendelea mbele au Aende huko anakokwenda kwa Furaha…. Jamii zote za Punda wanayo hiyo tabia, hata farasi anayo lakini si kwa kiwango alichonacho Punda…(kwasababu farasi naye ni jamii ya Punda).

Biblia inasema katika

Ayubu 39:19 “Je! Wewe ulimpa farasi uwezo wake? Au, ni wewe uliyemvika shingo yake manyoya yatetemayo?

20 Ndiwe uliyemfanya aruke kama nzige? Fahari ya mlio wake hutisha.

21 Hupara-para bondeni, na kuzifurahia nguvu zake; Hutoka kwenda kukutana na wenye silaha.

22 Yeye hufanyia kicho dhihaka, wala hashangai; Wala hageuki kurudi nyuma mbele ya upanga. ……

25 Kila ipigwapo baragumu yeye husema, AHA! NAYE HUSIKIA HARUFU YA VITA TOKA MBALI, Mshindo wa maakida, na makelele”.

Unaona! Farasi anauwezo wa kusikia harufu ya vita toka mbali..Kesho kutapiganwa vita farasi leo kashajua!! (Ni kipawa ambacho Mungu kawapa)..Sasa hisia za Punda ni kubwa kuliko za Farasi. Wafugaji wazoefu wa punda wanajua!..huwa punda akigoma kufanya kitu au kwenda mahali huwa hawamlazimishi..kwasababu wanaelewa hisia alizonazo punda..

Tunasoma mfano mmoja katika Biblia wa mtu anayeitwa Balaamu, huyu alitaka kwenda kuwalaani Israeli, jambo ambalo Mungu alimkataza kulifanya..lakini yeye akashupaza shingo,..wakati akiwa njiani anaelekea kwenda kuonana na mfalme Balaki kwa lengo la kuwalaani Israeli, akiwa amempanda punda wake…Njiani alikutana na Malaika ambaye alitaka kumwua lakini cha ajabu ni kwamba Balaamu hakumwona yule malaika lakini punda alimwona!..Japokuwa Balaamu alikuwa ni mtu wa kiroho sana aliyezoea kuona malaika lakini siku hiyo hakumwona…Punda alimsaidia kumwepushia ile ajali ya kuuawa. Mpaka alipofunguliwa macho na kuiona hatari iliyopo mbele yake..hivyo asingekuwa punda Balaamu angekufa..(Kasome Hesabu 22 yote). .

Nakumbuka ilikuwa mwaka 2015, mwezi wa 10 tarehe 14..Tulikuwa tupo wawili tunapita mahali fulani huku tunazungumza habari za Mungu..Sehemu hiyo ilikuwa ni mbali kidogo na mji ni kama nusu Kijiji hivi…Ni sehemu ambayo ina wafugaji na wachungaji…Siku hiyo jua lilikuwa linawaka sana wakati tunatembea huku tunaongea..mbele yetu walitokea watu ambao walionekana wametoka porini kukusanya nyasi za ng’ombe hivyo wameziweka kwenye kigari ambacho mbele kilikuwa kinavutwa na punda watatu waliofungiwa nira. Binafsi sikuwahi kuona punda watatu wakiwa wamefungwa nira pamoja..Nimezoea kuona wawili tu…Na hata mwenzangu na yeye hakuwahi kuona hicho kitu…Basi wote kwa pamoja tukasema ngoja tusogee mbele kidogo tuona jinsi walivyozifunga hizo nira katikati ya hao punda watatu..

Wakati tunaendelea kusogea..

wale mabwana walikuwa wanawachapa waendelee kusogea mbele..maana ule mzigo ulikuwa ni mzito kidogo..Sasa wakati tunakazana kutazama zile nira katikati ya wale punda watatu, yule punda wa katikati akatoweka!. Wakabaki wawili tukaduwaa kidogo ni nini kinaendelea…Lakini wale mabwana wao ni hawakuona lolote…

Wakati tunaendelea kuangalia

tuligundua kuwa wale punda walikuwa na uwezo fulani ambao haukuwa wa kawaida..kwasababu mzigo ulikuwa mzito na viboko vingi lakini walitembea vizuri kama kawaida…Sasa kwa haraka haraka kama si mtu wa rohoni unaweza kuhisi umeona uchawi!!..lakini haukuwa uchawi, Roho Mtakatifu muda mfupi baada ya hilo tukio alizungumza na sisi kutufundisha jambo…

Tulichokiona kilikuwa ni ono!..Kwamba Bwana hata katikati ya Wanyama yupo kuwasaidia,..Na pia akatufundisha kuwa “walipo wawili au watatu yeye yupo katikati yao”..Ulikuwa ni uthibitisho tu kuwa Mungu yupo katikati yetu wakati tunazungumza habari zake… na wengine wakusanyikao katika Bwana yeye anakuwa katikati yao, mfano wa wale punda..Na wakati wale mabwana wanadhani wale punda wapo wawili tu…kumbe wale punda walikuwa wanamwona mwingine watatu akiwa katikati yao, akiwachukulia mizigo yao na maumivu yao… Haleluya!!, Hicho ndicho Roho Mtakatifu alichotufundisha siku hiyo.

Sasa tukirudi kwa kile kilichotokea wakati Bwana anaingia Yerusalemu…Unaweza kufikiri ni nini wale Punda walikiona mbele??..Farasi wangenusa vita lakini si WOKOVU uliokuwa unakwenda Yerusalemu..Ngamia wangenusa jangwa lakini Punda waliona wokovu…Waliona Amani, walimwona huyu tuliyembeba Anakwenda kuleta Ukombozi kwa viumbe vyote.

Punda alitii;

Hivyo wasingeweza kugoma..kama walivyogoma kwa Balaamu..Mbele ya Balaamu waliona kifo lakini mbele ya MASIHI YESU KRISTO WALIUONA WOKOVU!!! Haleluya. Waliona wokovu unaingia Yerusalemu, kipindi kifupi tu kijacho Roho Mtakatifu atashuka ndani ya watu kuanzia hapo Yerusalemu..waliona mabadiliko makubwa ya nyakati yanakwenda kuanza..Punda Waliona huyu atupandaye ataleta amani si tu kwa wanadamu bali hata kwa viumbe vyote..kwamba wakati utafika viumbe vyote vitawekwa huru kupitia huyu..Hivyo punda yule alitembea mbele kwenda Yerusalemu kwa furaha yote wala hakusimama njiani..

Kwasababu Biblia inasema katika..

Warumi 8:19 “Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.

20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini;

21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

22 Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa”.

Ndugu kama Punda wameouona wokovu wewe kwanini usioune wokovu!..Punda walikubali kutumika wewe kwanini usikubali leo!..Punda waliupata ufunuo wa Yesu wewe kwanini hauuoni leo…Bado unaitumikia dunia ambayo mshahara wake ni mauti!!..bado mwasherati, mlevi, mzinzi, mla rushwa, msengenyaji, mwizi, mlawiti, mtoaji mimba, mvumishaji habari za uongo na mshirikina?..Utaficha wapi uso wako siku ile!..

Sasa lengo kuu sio kuwasifia punda, au kuwafanya kuwa viumbe wa kiungu!.. Kwamba wanastahili kuheshimiwa..au kutumika katika masuala ya utambuzi…Hapana! hakuna mnyama yoyote anayestahili kupewa heshima hiyo wala kuhusishwa na masuala ya Ibada…Lengo kuu ni kujifunza ni UTUKUFU ALIOUBEBA YESU KRISTO, Na kwamba kila kitu, ikiwemo viumbe vyote vimebeba ushuhuda wake…Kila mahali kwenye miti, miamba, bahari, mbingu, milima, sayari n.k kumeandikwa ushuhuda wa Yesu Kristo. Hivyo Yesu Kristo ni muhimu sana katika Maisha yetu.

Bwana anasema..

Mathayo 11:28 ‘’Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi’’

Hivyo Kama hujamkabidhi Maisha yako…Mlango upo wazi sasa, ila hautakuwa hivyo siku zote…itafika wakati utafungwa na ukishafungwa itakuwa haiwezekani tena kuupata wokovu…Hivyo unachopaswa kufanya kama hujakoka ni hapo ulipo utubu dhambi zako zote bila kuacha hata moja…mwambie Bwana Yesu akusamehe na kwamba hutafanya tena hizo dhambi..na ukishatubu kwa kumaanisha kabisa, kuna msukumo wa ajabu utakuja ndani yako wa kukufanya utamani kumjua Mungu Zaidi…

Mkumbuke mtu yeyote ambaye hapo kwanza uliwahi kumwona ni mkristo wa kiroho, na matendo yake ni mazuri…kajiungamanishe naye huyo, na kuanzia hapo Roho Mtakatifu ataanza kutembea na wewe kukuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko…Pia katika hatua hizo zingatia kutafuta ubatizo haraka sana kama hukubatizwa..Ubatizo sahihi ni ule wa maji tele (Yohana 3:23),..na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na Matendo 2:38, Na Roho Mtakatifu atafanya yaliyosalia ndani yako.

Kumbuka Yesu Kristo, ndiye NJIA, KWELI na UZIMA…Hakuna njia nyingine ya kuokolewa isipokuwa kwake yeye.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Maran atha!

Mada Nyinginezo:

KWANINI AWE NI PUNDA NA MWANA-PUNDA?

JE! MTUMISHI KUTOKUWA NA FEDHA NI ISHARA KUWA KUNA TATIZO KATIKA IMANI YAKE?

USISIKILIZE DHIHAKA ZA SHETANI, ZITAKUKWAMISHA.

TUMAINI NI NINI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Grace Manangu
Grace Manangu
4 years ago

Bwana Yesu asifiwe sana! Kwanini Yesu alimpanda mwanapunda na si mama yake?