KWANINI AWE NI PUNDA NA MWANA-PUNDA?

KWANINI AWE NI PUNDA NA MWANA-PUNDA?

Tukisoma injili ya Mathayo 21:2-7, tunaona Bwana akiwaambia wanafunzi wake maneno haya:

“2 Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona PUNDA AMEFUNGWA, NA MWANA-PUNDA PAMOJA NAYE; wafungueni mniletee.

3 Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka.

4 Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,

5 Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda.

6 Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru,

7 wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake.”

*** Lakini tukirudi kusoma kwenye Injili ile ya Marko na Luka utaona waandishi wale wanamtaja mnyama mmoja tu kana kwamba hakukuwa na mwingine pamoja naye kwamfano tukisoma ile injili ya Luka 19:30 inatuambia ..

“30 akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa.

31 Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji.

32 Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia.

33 Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda?

34 Wakasema, Bwana ana haja naye.

35 Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu.

36 Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani”.

Unaona? Ni rahisi kusema maandiko yanajichanganya, lakini si kweli maandiko yapo sawa siku zote, embu jaribu kuwazia mfano huu, watu wawili walioshuhudia ajali iliyotokea mpanda wiki 2 zilizopita waliitwa kituo cha polisi ili kutoa taarifa ya tukio lilivyotokea..Mmojawapo akasema: niliona fuso iliyobeba mizigo ikienda moja kwa moja kuivaa gari ndogo ya abiria, na ghafla nilichokiona ni watu wakitoa nje ya vioo, wakirushwa huko na huko na wengine wakipondwa vibaya na ile fuso iliyokuja kulala juu ya lile gari la abiria hivyo ikapelekea kusitokee abiria yoyote aliyepona.,. Lakini shahidi wa pili naye alipoitwa atoe taarifa zake alisema, niliona gari kubwa likiwa katika mwendo wa kasi sana likitokea upande wa juu, lakini ghafla pikipiki ikakatiza mbele yake, na yule dereva alipokuwa katika harakati za kuikwepa pikipiki ile, alijikuta anaacha njia yake na kuingia upande wa pili na hapo ndipo alipokutana na lile gari dogo la abiria na kusababisha ajali.

Sasa kama ukiangalia mfano huo utaona mtu wa kwanza hakutoa habari za mwendesha pikipiki, yeye alitoa hasa maelezo ya ajali ilivyotokea lakini wapili alizungumzia zaidi chanzo cha ajali kuliko ajali ilivyokuwa, lakini hiyo haiwafanyi mashahidi wale wawili kuwa waongo kwasababu maelezo yanayotofautiana, wala hauufanyi ushuhuda wao kujichanganya.

Na ndivyo ilivyo katika habari hii ya punda, kulikuwa na sababu Mungu kuruhusu waandishi hao watoe taarifa kwa jinsi tofauti ili atufundishe sisi kitu..Ni kweli kabisa punda aliyechukuliwa pale hakuwa punda mmoja, Bwana aliwaagiza mitume wake wamlete Punda,akiwa na mtoto wake, japo shabaha yake ilikuwa ni Yule mtoto wa punda, na sio Yule punda mkubwa na ndio maana waandishi wale wengine hawakusumbuka kueleza habari za wote isipokuwa yule mwana-punda tu peke yake kwasababu yeye ndio ilikuwa shabaha kubwa katika habari ile , lakini tukisoma huku kwingine kumbe Bwana hakuona vema aende peke yake, bali pamoja na mama yake..

Hiyo ni kutupa sisi picha zaidi, juu ya mazingira yaliyokuwa yanamzunguka mwana-punda yule, kutuonyesha ni jinsi gani yule mwana-punda alivyokuwa bado ni mdogo, bado ni mchanga hawezi pengine kwenda mahali popote peke yake bila mama yake,hajafikia hatua bado ya kutumia katika utumishi wowote, bado ananyonya, hivyo alihitaji msaada mkubwa sana wa mama yake pembeni au kama si msaada basi alihitaji walau faraja ya mamaye.

Biblia inatuambia alikuwa bado hajakomaa kuweza kubeba mizigo wala kupandwa na mtu yeyote.

Bado alikuwa ni mchanga kabisa, lakini ndiye huyo Bwana aliyemuhitaji. Tunaweza kujiuliza ni Kwanini Yesu hakumwonea huruma walau angempanda mama yake, Yule mtoto apumzike pembeni mwa mamae…Lakini hilo halikuwa chaguo lake mambo yalikuwa kinyume chake..

Ndugu/Kaka, kumbuka mahali ulipo, katika udogo wako, katika uchanga wako wako uwe ni wa kimwili au wa kiroho kiasi cha kwamba huwezi kuenenda mwenyewe bila kutegemea msaada wowote kwa walio juu yako, hujawahi kutumika katika utumishi wa aina yoyote ile, lakini Bwana anakuita umtumikie katika hali hiyo hiyo uliyopo, chini ya huyo huyo kiongozi wako wa kiroho ambaye anakufundisha..Bwana anakuita ukamtumikie, hivyo usikwamishwe na chochote, Bwana aliyemwita Yule ndiye anayekuita na wewe, (wote wawili amewaita)….Yeye hana upendeleo wala jicho lake si kama macho yetu, haangalii cheo, umaarufu wala uzoefu…

Lakini tukiurudi kwenye hiyo habari…kiukweli hawezi kuwapanda wote wawili kwa wakati mmoja, bali amekuchagua wewe ULIYE MDOGO UMTUMIKIE, Ili Yule mkubwa asimame pembeni yako kukufariji ,.. Bwana hawezi kumtumia Yule kwa viwango vya sasa anavyovihitaji kwasababu kashatumika tayari..Ni zamu yako sasa, leo hii wewe bado ni fresh, anakuhitaji sana katika utumishi wake, wa kumtukuza yeye katika nyakati hizi za mwisho za kumalizia, Mteule wa Bwana.

Umekuwa ukiwaangalia viongozi wako kama kitu cha kurejea, ni jambo jema, sio jambo baya,umekuwa ukijiona hujafikia bado viwango vya kutumika mbele za Mungu, mpaka utakapipitia pengine madarasa Fulani au chuo fulani au hatua Fulani kama za mchungaji wako au mwalimu wako, hiyo ni kweli kabisa, lakini Yesu amekuchagua wewe sasa katika udogo huo, ukamtukuzwe katikati ya mataifa. Hivyo Ndivyo ilivyompendeza yeye…Bwana Yesu alisema hivi.

“Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, UKAWAFUNULIA WATOTO WACHANGA. 26  Naam, Baba, KWA KUWA NDIVYO ILIVYOPENDEZA MBELE ZAKO.(Mathayo 11:25).

Unaona? Hivyo ndugu ikiwa utausikia ujumbe huu, ikiwa utasikia wito wa Mungu ndani yako, usikawie kawie, wala kujiuliza uliza mara mbili eti mimi nafaa, au nitaweza?, ingia gharama ya kumfuata Kristo, jitwike msalaba wako, umfuate sasa, neema hiyo haitadumu milele juu yako ukichelewa chelewa shetani naye yupo pembeni kutaka kukutwika mizigo yake, au akupande ili akutumie katika mambo yake maovu, na kama unavyofahamu Kristo hatampanda punda Yule ambaye tayari kashatumiwa, wakati ndio huu uusikiapo ujumbe huu.. chukua uamuzi sasa. Kwasababu yeye mwenyewe alisema..

Mathayo 28:29 “JITIENI NIRA YANGU, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Sasa usisubiri shetani akutie nira yake ngumu katika uchanga wako, huu ni wakati wa kusema mimi na YESU tumefunga pingu za maisha milele..Na kuanzia sasa namaanisha kumfuata YESU katika hali zote zitakazokuja mbele yangu. Na hakika atakuangazia wema wake kwa wakati wake aliouweka juu yako..Kumbuka Punda Yule mdogo aliyekuwa akikaa mabandani tu na kula majani, muda mfupi baadaye tunamwona akitembea juu ya red-carpet, Hiyo ni kututhibitishia kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kumtumikia Bwana akaja kujuta maishani.

Na kumbuka leo Tarehe 14, mwazi huu wa Nne ni sikukuu ya Mitende…wakristo wote duniani wanaadhimisha siku ile kuu Bwana aliyoingia Yerusalemu huku akiwa amempanda mwana-punda…Hebu huyo mwanapunda leo awe wewe…Mwambie Bwana nipo mimi, nitwae jinsi nilivyo, niwe chombo chako, wewe Mfalme wa wafalme, Na hakika utauona wema wa Mungu kwa viwango ambavyo havipo.

Marko 11: 7 “Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake.

8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani.

9 Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;

10 umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. HOSANA JUU MBINGUNI.”

Ni matumaini yangu, utafanya hivyo sasa.

Bwana akubariki na Jina la BWANA YESU libarikiwe daima. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TUSIFUNGWE NIRA PAMOJA NA WASIOAMINI.

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

TABIA YAKO NI YA MNYAMA GANI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments