RACA

RACA

Mathayo 5: 20 “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

21 Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.

22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; NA MTU AKIMFYOLEA NDUGU YAKE, ITAMPASA BARAZA; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto”.

Umewahi kujiuliza kumfyolea ndugu yako ni kufanya nini?

Siku moja, kuna mtu aliniudhi sana nikakasirika sikumwambia chochote ila nilimwonyesha hisia ya kukasirika… Sasa wakati naongea na mtu mwingine nikamtaja na kusema mtu fulani ameniudhi sana ni “mpumbavu sana” nikamtajia na sababu ya alichonifanyia…Baadaye kidogo hasira zilivyoanza kupungua nikaanza kusikia kukosa amani na kuhukumiwa ndani…

sikujua tatizo liko wapi lakini nilijua kuna tatizo…Nikaanza kujitafakari tukio lilolopita nikasema moyoni mimi ni mkristo sipaswi kuwa na hasira hivi..Baadaye nikaenda kutubu..lakini ndani nilikuwa bado najihisi sijatatua tatizo, Nikachukua biblia nikamwomba Bwana azungumze na mimi juu ya hii hali.

Nikafungua biblia mstari wa kwanza niliokutana nao ndio huo…”21 Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. 22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; NA MTU AKIMFYOLEA NDUGU YAKE, ITAMPASA BARAZA; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto”.

Baada ya kuusoma huo mstari, nilijisikia vibaya sana…nikaanza kujiuliza ni nini maana ya “kumfyolea ndugu yangu” kwamaana siku zote nasomaga lakini sielewi, maana ndio sentensi ya kwanza kukutana nayo nilipofungua biblia,Nikaenda kutafuta kwenye kamusi na kwenye biblia ya kiingereza na nyingine tafsiri yake…Nikapata tafsiri. Neno kufyolea linatoka kwenye Neno la Kigiriki linaloitwa “RACA”..Na maana ya Neno hilo “RACA” ni kichwa kisichokuwa na kitu, au kichwa maji kwa lugha zetu. Au “mpumbavu” kwa neno rahisi zaidi.

Kwahiyo maana ya kumfloyea ndugu yako ni kumpa Neno baya linaloonyesha udhaifu wake..kama vile mpumbavu, mjinga, tahira, mshenzi, mpuuzi…n.k Hayo ni maneno yanayoonyesha moja kwa moja udhaifu wa mtu, na Bwana katuonya tusiyatumie kabisa hayo..Na mtu anayeyatumia hayo itampasa Baraza, maana yake kikao cha hukumu, baada ya kujua hilo nikatubu tena kwa mara ya pili, nikaacha kutumia hayo maneno nikasema sitakaa tena nitumie hayo maneno na Bwana anisaidie…hata kama nimeona mtu ni kweli kafanya upumbavu lakini sitamwita mpumbavu….labda ninaweza kumwambia jambo ulilolifanya ni la kipumbavu kwa nia ya kumrekebisha sio kumkosoa ili abadilike lakini sio kumwita mpumbavu au mjinga au mshenzi.

Unajua ni kweli Biblia kwenye agano la kale sana sana kwenye kitabu cha Mithali na Zaburi imetaja sana juu ya watu wapumbavu na wajinga…Ni kweli Daudi na Sulemani walitoa hekima zao kwa wajinga na werevu…lakini hao hawakuwa utimilifu wa mambo yote..walimjua Mungu kwa sehemu, yupo mmoja ambaye aliyekuja kuitimiliza torati yote mwenye hekima kuliko Sulemani ambaye alimjua Mungu kwa utimilifu wote..”ndiye anayetuambia TUSIMWITE MTU YOYOTE MPUMBAVU WALA MJINGA”…Daudi aliua lakini yupo mmoja anayetuonya “hata tusimwonee ndugu yetu hasira kwasababu ni sawa na kuwa muuaji”…Musa alitoa ruhusa ya kuoa wake wengi lakini yupo mmoja anayetuambia “hapo mwanzo Mungu alimwumba mwanamke na mwanamume, kwahiyo ndoa ni mke mmoja na mume mmoja tu“

Kwahiyo tumsikilize Daudi au Musa au tumsikilize Yesu ambaye ni Bwana wa Daudi na Musa?..Yohana mbatizaji alisema “Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua Yohana 3:30”…Na hata Daudi au Musa au Sulemani au Eliya wangekuwepo leo hii wangesema maneno hayo hayo..”kwamba sisi hatunabudi kupungua bali yeye kuzidi”.

Kwahiyo Ndugu unayesoma ujumbe huu,usitumie agano la kale, kuhalalisha laana juu ya ndugu yako wala kumdhihirishia udhaifu wake kwa kumwambia yeye ni mjinga, au ni mpumbavu, au mshenzi au kichwa maji au kichwa hewa n.k NI DHAMBI, hauhitaji uwe muuaji ndio ihesabike kuwa wewe ni muuaji! Kitendo cha chuki tu kujengeka ndani yako au Neno la kudhalilisha likitoka kinywani mwako tayari ni picha tosha ya mambo yaliyopo moyoni mwako, wewe na mtu anayeua hamna tofauti..wote wawili asili ya dhambi yenu ni moja! Chuki au hasira ndani ya moyo…isipokuwa mmoja hasira yake imeishia kutukana mwingine kuua! Kwahiyo wote ni sawa na wauaji tu! Maandiko yanasema hivyo.

Ni matumaini yangu kuwa umepata kitu, na Bwana atusaidie sote tuishi katika njia inayompendeza yeye kila siku. Tukue toka utukufu hata utukufu tukijifunza kutokana na makosa.

Mungu akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Sephania
Sephania
1 year ago

Amen nashukuru kwa ujumbe huu !Mungu wa !Mbingu na !Nchi !Bwana !Yesu na akubaliki