Je udhaifu au ulemavu wangu unaweza kuzuia watu kumwamini Yesu?
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.
Lipo swali moja muhimu sana linaloulizwa na wengi?..Je kama mimi nina tatizo fulani labla la kuona, au kusikia, au nina ulemavu fulani ambao unaonekana kabisa…Je hali kama hiyo nikienda kuhubiri/kushuhudia watu wataokoka kweli?..Si wataniuliza mbona huyo Mungu hajakuponya wewe kwanza atawezaje kutuponya sisi?.
Hii ni mojawapo ya silaha ya shetani anayoitumia kuhakikisha injili haihubiriwi!…Na silaha nyingine anayoitumia ni sauti inayosema “umemkufuru Roho Mtakatifu”..ukisikia sauti yoyote unakuambia hayo maneno mawili kwamba “huwezi kuhubiri kutokana na udhaifu wako” au “umeshamkufuru Roho Mtakatifu”.. Basi jua moja kwa moja hizo ni sauti za Adui shetani, hivyo zipuuzie!.
Sasa kabla ya kuendelea mbele ni vizuri tukafahamu mambo machache yafuatayo.
Kwanza Aliyepewa jukumu la kuhubiria wanadamu injili, ni Mwanadamu huyo huyo na si malaika. Hakuna mahali popote Mungu amewahi kumtuma malaika akahubiri injili. Na hakuna mwanadamu aliyeumbwa na Mungu asiye na kasoro kabisa!..Hata yule mhubiri maarufu na mashuhuri unayemfahamu na kumsikia anayo mapungufu yasiyohesabika. Kwahiyo Mungu anajua kabisa wanadamu wote wanayo mapungufu lakini akawapa hivyo hivyo jukumu la kubeba maneno yake na kuwasambazia wengine wasiyo nayo. Hivyo angekuwa anaangalia udhaifu kama ndio kigezo cha mtu kwenda kulihubiri neno lake, hakuna mwanadamu angestahili kuwa mhubiri…pengine Mungu angewatumia malaika wake walio watakatifu huko mbinguni na wala si wanadamu.
Kwahiyo kumbe kasoro zetu hazihusiani na sisi kukidhi vigezo vya kuhubiri Neno la Mungu!..maana yake ni kwamba uwe mrefu, uwe mfupi, uwe unajua kuongea au hujui kuongea vizuri, uwe na kigugumizi, uwe mzungu, uwe mwafrika, uwe albino, uwe kiziwi, uwe kipofu, uwe huna miguu, uwe huna mikono, uwe maskini, uwe tajiri, uwe hujui kusoma, uwe mtu mdogo kabisa katika jamii, uwe mtu mkubwa.. uwe yoyote yule uwazaye kuwa, maadamu unaitwa MWANADAMU!. Basi umeshafuzu kuwa na uwezo wa kulibeba Neno la Mungu na kuwapelekea wengine.
Kigezo cha kwanza cha wewe kuweza kuwapelekea wengine NENO la Mungu ni wewe kwanza uwe na hilo Neno la Mungu ndani yako. Hicho ndio kigezo cha kwanza na cha Muhimu, kwasababu hata katika hali ya kawaida, hakuna mwalimu anaweza kumfundisha mwanafunzi maarifa ambayo yeye mwenyewe hana!. Hivyo ni lazima Neno la Kristo likae ndani yako, na hiyo inakuja kwa kumpokea Mwokozi Yesu Kristo na kulisoma Neno lake na KULIISHI HILO NENO!.
Baada ya hapo! Unaweza kuhubiri Injili kwa mtu yeyote yule.. Usisubiri Uone maono, au utokewe na Yesu au Malaika.. Wengi wanaisubiri hii hatua na hawaifikii..Wanatamani wasikie sauti KWANZA ikiwaambia nenda kahubiri!.. “Ndugu usiisubirie hiyo sauti “ hutakaa uisikie milele..Ni kwanini hutakaa uisikie?..Ni kwasababu tayari alishasema katika neno lake… “ENENDENI MKAWAFANYE MATAIFA YOTE KUWA WANAFUNZI..(Mathayo 28:28)”. Usisubiri sauti nyingine..hutaisikia!!
Sasa Swali lingine…Ni nini kinachomgeuza Mtu kama sio Ukamilifu wetu wa kuongea na kusikia vizuri?
Tusome mstari ufuatao kisha tutajua..
Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”
Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”
Hapo anasema “NENO LA MUNGU” Sio maneno yaliyopangiliwa vizuri, wala sio midomo yetu inayoweza kuumba maneno mwanana, wala sio rangi za nyuso zetu, wala sio masikio yetu yanayosikia vizuri maneno tunayoulizwa na wale tunaowahubiria, wala macho yetu yanayotazama vyema watu tunaowahubiria wala ufupi wetu, wala urefu wetu, wala elimu yetu…Bali NENO LA MUNGU!..Hilo ndio lenye nguvu…linapotajwa na mwanadamu yeyote ambaye kalishika…basi linapenya mpaka ndani ya ule moyo wa anayelisikia..linamchana chana na kumgawanya moyo wake…linapenya na kumfunulia yule anayelisikia mambo yake ya siri anayoyafanya atoke katika hali yake ya kawaida. Wakati wewe unafikiri anasikiliza kigugumizi chako, au anazitafakari kasoro zako… kumbe mwenzio Roho Mtakatifu anateta naye huko, anaugulia ndani kwa ndani..
2Wakoritho 10:4 “(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo”
2Wakoritho 10:4 “(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)
5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo”
Kwahiyo usikubali kusikiliza uongo wa shetani ambao unakukatisha tamaa kwenda kuhubiri injili..Kama husikii vizuri, wewe hubiri hivyo hivyo, yule unayemhubiria akikuuliza swali sogea karibu msikilize tena na tena, ukiona bado humsikiI, wewe endelea mbele..usianze kuutafakari udhaifu wako…kwasababu hata yeye wakati huo atakuwa hautafakari udhaifu wako!… na pia hatakuchukia ila lile Neno utakalomwambia hata kama ni moja tayari ni Nguvu ya Mungu..na ni mbegu..
Tatizo kubwa la wengi ni kufikiri kwamba Injili ni maneno mengi… jambo ambalo sio kweli!…Mtu anayehubiri maneno mengi basi ni kaongozwa na Roho kufanya hivyo…Lakini Neno moja tu la MUNGU!..Linatosha kubadilisha moyo mgumu wa jiwe na kuwa mlaini.. Kwa neno moja tu la Mungu na iwe Nuru!..ndio iliumba jua hili ambalo mpaka leo tunalo vizazi na vizazi.. Hivyo usitafute sana ujuzi wala utaalamu katika kwenda kulitangaza Neno la Mungu…Wewe Tafuta Roho Mtakatifu. Kisha itumie karama yako Mungu aliyokupa.
Mwanamke mmoja mashuhuri anayeitwa Fanny Crosby alizaliwa akiwa mzima lakini baada ya wiki mbili akawa kipofu, aliishi duniani katika hali hiyo hiyo ya upofu kwa muda wa miaka 95, lakini hakuacha kutafuta mahali ambapo angemtumikia Mungu licha ya kuwa alikuwa kipofu, alifanikiwa kuandika nyimbo zaidi ya 8,000, katika kipindi hicho cha karne ya 19, akajulikana kwa jina la malkia wa nyimbo za injili, na mwimbaji kipofu, moja ya tenzi mbili muhimu ambazo mpaka leo hii unazijua na kuziimba “Usinipite Mwokozi” na “Ndio dhamana Yesu wangu” pengine ulikuwa hujui ziliimbwa na huyu mama kipofu, na kwa kupitia uimbaji wake, na kuwahubiria wengine alifanikiwa kuwavuta watu wengi kwa Kristo.
Hivyo na sisi, kila mmoja wetu amesimame na kile Mungu alichokiweka ndani yake kuhakikisha injili inawafikia wengi.
Bwana akubariki.
www wingulamshahidi org
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
USINIPITE MWOKOZI Lyrics
REKEBISHA YAFUATAYO ILI MAMBO YAENDE SAWA.
MAPAMBANO DHIDI YA SHETANI.
Mti wa MLOZI alioonyeshwa nabii Yeremia 1:12 tafsiri yake ni nini?
Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!
WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU
Rudi Nyumbani:
Print this post
Nitafurahi kupokea masomo na mafunzo hayo. 0767637346 whatsapp
Sawa tayari tumeshakuunga