AKAMSHIKA MKONO YULE KIPOFU, AKAMCHUKUA NJE YA KIJIJI.

AKAMSHIKA MKONO YULE KIPOFU, AKAMCHUKUA NJE YA KIJIJI.

Shalom.

Marko 8:23-26 Inatuambia Yesu alipokutana na Yule kipofu kule Bethsaida, Hakumponya palepale kama ilivyokuwa desturi yake ya kuponya watu wote wanaomfuata, bali biblia inatuambia alimchukua kwa kumshika mkono na kuanza kumtoa kwanza nje ya kijiji.

“22 Wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse.

23 Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu?

24 Akatazama juu, akasema, Naona watu kama miti, inakwenda.

25 Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi.

26 Akampeleka nyumbani kwake, akisema, Hata kijijini usiingie”.

Jaribu kutengeneza picha, wewe ni kipofu, unapelekwa kwa daktari kwa ajili ya kupewa dawa uondoke, badala ya kukutibu anakuchukua anaondoka na wewe, bila maelekezo yoyote, na kibaya zaidi afadhali angekuwa anakupeleka hospitali nyingine badala yake anakupeleka mahali ambapo hata husikii tena sauti za watu, nje kabisa ya mji, ni rahisi kudhani huyu mtu hana nia nzuri na mimi.. Lakini tunaona huyu kipofu alitii, japokuwa hajui ni wapi anapelekwa, pengine alitembezwa na Yesu kilometa kadhaa, mpaka wanafikia mahali ambapo hamna makazi ya watu, ni mashamba tu, hata wale watu waliompeleka kwake walishamwacha, amebaki yeye tu na Yesu, na pengine na wanafunzi wake tu.

Akiwa sasa hana tumaini lolote, haelewi ni kitu gani kinaendelea hapo ndipo Yesu anamwekea mikono yake, na kumponya..Lakini utajiuliza tena, ni kwanini biblia inatuaeleza aliponywa mara ya kwanza na ya pili?..Ni kwasababu kuna jambo Yesu alitaka tujue kuhusu upofu wa Yule mtu..Ukiyatafakari vizuri maneno yake utagundua kuwa mtu Yule hakuwa kipofu tangu alipozaliwa, bali aliupata upofu wake wakati Fulani katika maisha yake. Kwasababu kama angekuwa ni kipofu wa kuzaliwa asingesema naona watu kama miti inakwenda..Mtu aliyezaliwa kipofu hawezi kutofautisha mti na mtu.

Hivyo upofu wake hakuzaliwa nao, aliupata sehemu Fulani, na huko si kwingine zaidi ya kule kijijini alipokuwepo. Na ndio maana utaona Bwana Yesu alimpomaliza kumponya akamwambia..Hata kijijini usiingie.

Hichi ndicho kinachoendelea sasahivi rohoni, ulimwengu huu umewapofusha watu wengi rohoni, masumbufu ya ulimwengu huu, anasa, mambo ya kidunia, hawaoni tena kuwa hizi ni siku za mwisho, hawaoni tena kuwa unyakuo upo karibu, hawaoni tena kuwa dunia hii imeshaoza, haijalishi watasikia injili ngumu kiasi gani bado wataona ni kawaida tu..

2Wakorintho 4:3 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;

4 AMBAO NDANI YAO MUNGU WA DUNIA HII AMEPOFUSHA FIKIRA ZAO WASIOAMINI, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”.

Lakini kama tunavyosoma hapo, mtu akitaka Yesu amfumbue macho, hakuna njia ya mkato vigezo ni sharti Yesu akuchukue nje ya kijiji..Ni lazima kwanza katika upofu wako ukubali Yesu akutoe katika ulimwengu, ni sharti ukubali kujitenga na anasa, lazima ukubali kuacha fashion na kuvaa mavazi ya kikahaba, ni lazima ukubali kuachana na marafiki wabaya, na mambo yote yasiyompendeza Mungu, yaani kwa ufupi ukubali kuipoteza nafsi yako kwenye mambo ya kidunia, na hapo ndipo Bwana YESU atakapokufumbua macho yako, na kuona mambo yote ya rohoni WAZI WAZI,

Kumwona shetani jinsi anavyofanya kazi katikati ya watu wa ulimwengu huu, kuona jinsi unyakuo ulivyo karibu, kuona jinsi ulivyokuwa hatarini kuelekea kuzimu.. Hapo ndipo utajijua kweli ulikuwa kipofu, lakini sasa hivi upo kwenye ulimwengu huwezi kujiona kwasababu tayari umepofushwa macho.

Ndugu pengine hii ni mara yako ya elfu kulisikia hili Neno kuwa hizi ni siku za mwisho, Hata kama Unyakuo hautakukuta, basi ujue hata siku zako za kuishi hapa duniani si nyingi, hujui kesho utaamkia wapi? Wanaokufa na kushuka kuzimu idadi yao haihesabiki, ukifa leo katika upofu ulio nao, hakuna tumaini tena la uzima baada ya hapo.

Kama wewe ni mkristo na unajua kuwa hili ndio kanisa la mwisho la 7 lijulikanalo kama Laodikia (Ufu.3:14) na kwamba hakutakuwa na kanisa lingine baada ya hili (Ufu.10:7), halafu bado huyathamini maisha yako ya rohoni, hiyo ni dalili kubwa kuwa umepofushwa macho na ulimwengu huu.

Huu ni wakati ambao tayari magugu na ngano vimeshajitenga, wale walio hapo katikati (yaani vuguvugu), upande wao ni wa shetani, kwasababu Bwana Yesu alishasema atawatapika..Ni heri utemwe, kuliko kutapikwa, matapishi hata kuyaangalia huwezi, sembuse kuliwa tena?.Usisibiri utapikwe, Tubu mtafute Bwana Yesu hichi kipindi cha kumalizia.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

SABATO TATU NI NINI?

Wanaowachukua wanawake wajinga mateka ni akina nani?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 8 (Kitabu cha Ezekieli)

JE TATIZO LA KULA KUCHA NI ISHARA YA KUWA NA MAPEPO?

MAMBO YATAKAYOTOKEA ISRAELI SIKU ZA HIVI KARIBUNI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Danieli
Danieli
2 years ago

Amina