MAVAZI YAPASAYO.

MAVAZI YAPASAYO.

Shalom, Mtu wa Mungu karibu tujifunze Neno la Mungu, Taa pekee ya kweli iongozayo miguu yetu.

Leo kwa ufupi tutajifunza ni kwanini Mwanamume hapaswi kuvaa mavazi yampasayo mwanamke, kadhalika na mwanamke hapaswi kuvaa mavazi yampasayo mwanamume.

Neno hilo linapatikana katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 22:5 “ Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo NI MACHUKIZO KWA BWANA, MUNGU WAKO.”

Jambo la msingi na muhimu ambalo watu wengi hatulifahamu kuhusu huu mstari ni kuwa Biblia haijasema hapo, mwanamume au mwanamke asivae mavazi yaliyotengenezwa mahususi kwa jinsia nyingine hapana bali imesema “YAMPASAYO”.

Neno yampasayo ni Neno linalohusiana na maumbile, yaani mavazi yanayopatana na maumbile ya mtu husika…

Kwamfano maumbile ya mwanamume ni ya misuli, na ukomavu kidogo, na yasiyo na mvuto hivyo mavazi yake yanapaswa yawe yanaendana na jinsi mwili wake ulivyotengenezwa, kadhalika na mwanamke mwili wake ni mlaini kidogo na umbo lake ni la kipekee tofauti na mwanamume hivyo na mavazi yake yanapaswa yaendane na jinsi mwili wake ulivyotengenezwa.

Kwahiyo mwanamume umbile lake linamlazimu avae suruali, wakati mwingine na nguo ngumu hayo ndio mavazi yanayoendana na mwili wake..Na kadhalika mwanamke hana sababu ya kuvaa suruali kwasababu umbile lake sio sawa na la mwanamume..yeye nguo zake ni magauni mazuri, marefu yaliyotengenezwa kwa ustadi mbali mbali ambayo yanamsitiri na sketi zenye heshima…hayo ni mavazi yanayompasa mwanamke

Sasa kwanini ni machukizo kuvaa nguo zisizoupasa mwili wako, leo tutajua ni kwanini ni machukizo..

Machukizo maana yake, ni kitu kinachochukiza, Mfano ukifanya kitu usichokitaka au usichokipenda maana yake hicho kitu kitakuchukiza, na kama tayari kimeshakuchukiza hapo ni rahisi kuchukua uamuzi wowote aidha kukasirika au kutengana na hicho kitu. Huo ni mfano tu!…Na tabia nyingine ya kitu kinachokuchukiza ni kwamba mtu mwingine anaweza asione kama kinakuchukiza, jambo linalokuchukiza wewe kwa watu wengine linaweza kuonekana kama ni jambo la kawaida.

Na ndivyo hivyo hivyo kwa Mungu wetu tunavyoonekana, tunafanya kitu kinachomchukiza tunapovaa mavazi yasiyopasa maumbile yetu. Unaweza ukaona hakuna shida kufanya hivyo lakini ni machukizo. Ni kitu kinachomuudhi sana Mungu ndani ya moyo wake.

Unakumbuka pale Edeni, Adamu na Hawa baada ya kuasi wakashona majani wakajitengenezea mavazi ya majani?…wao waliona wamejisitiri na kupendeza lakini mbele za Mungu wote wawili walikuwa wamevaa mavazi yasiyowapasa na hivyo Mungu hakupendezwa na yale mavazi akawatengenezea mavazi mengine ya ngozi.

Kwahiyo ni machukizo makubwa sana kuvaa mavazi yasiyoupasa mwili wako, jaribu kufikiri leo labda simba wamepewa akili kama mwanadamu..halafu unakwenda porini na kukuta simba kavaa ngozi ya fisi, au unamwona simba jike kaota zile nywele za shingoni kama za simba dume, na simba dume hana zile nywele..Unaona ni kitu kisicholeta picha nzuri ni kitu cha kuchukiza.

Na ndio hivyo hivyo tunavyoonekana mbele za Mungu..

Sasa hivi utakwenda kila mahali mpaka kanisani utakuta wanawake wamevaa suruali, na ukijaribu kuuliza atakwambia hizi ni suruali za kike kwahiyo hazina shida!! Dada yangu mpendwa…shetani asikupofushe macho, hakuna suruali za kike, suruali zote ni za kiume zilitengenezwa mahususi kufuatia maumbile ya wanaume soma kutoka 28:42-43 utathibitisha hilo…sio kwasababu na wewe dada una miguu miwili iliyogawanyika kama mwanamume ndio iwe sababu ya wewe kuvaa suruali, ndugu usidanganyike…hata simba jike ana kichwa kama cha simba dume lakini yale manyoya ya kichwa yamewekwa mahususi kwa ajili ya maumbile ya kichwa cha simba dume tu!!..Kwahiyo usijaribu kulinganisha vitu bila hekima ya macho ya rohoni..Hizi ni siku za mwisho, shetani anakuja kwa ujanja mwingi sana ambao usipokuwa makini unachukuliwa nao.

Hivi unajua kuwa siku hizi kuna SIDIRIA ZA KIUME PIA??…Kama ulikuwa hulijui hilo, hebu katafute kulijua, zipo sidiria za kiume na zinauzwa bei ghali sana, nyingine mpaka kufikia sh. Laki moja za kitanzani, na nyingine zaidi ya hapo, na zipo za mitindo tofauti tofauti.. unaweza ukazi-search kwenye google utaziona, na tena zina maua maua kama zile za wanawake, na zinavalika sana na kuuzika sana duniani, na zinaheshimika…Na watu wanazivaa kama fashion, nk.

Sasa hebu nikuulize wewe mwanamke, umekwenda kanisani na kukuta mchungaji kavaa hiyo sidiria ya kike halafu anakuhubiria na anakwambia hii haina shida! Ni sidiria ya kiume haina tatizo!! Je! Utamwamini?…si utasema dunia imeisha??…Kadhalika na wewe usidanganywe na kuambia ‘‘kuna suruali za kike’’.

Kama mchungaji wako havai sidiria za kiume madhabahuni asikudanganye na wewe uvae suruali za kike kanisani au nje ya kanisa, kama yeye haweki hereni, mabangili, hapaki wanja, lipstick wala havai sketi za kiume ambazo zipo na watu wanazivaa…basi asikudanganye na wewe uning’inize mambo hayo katika mwili wako…Biblia inasema mwanamke avae mavazi ya KUIJISITIRI, na sio ya Kuficha sehemu za siri (1Timotheo 2:9)..Suruali yoyote inafunua maumbile ya mwanamke, hivyo haiwezi kumsitiri, Kwanini avae?

Weka mbali vimini, weka mbali tattoo, weka mbali hereni, mawigi, suruali.. na kila aina ya fashion za ulimwengu huu..Biblia inasema aupendaye ulimwengu hata kumpenda Mungu hakupo ndani yake…

Jehanamu ipo!! Sio hadithi za kutunga..Ni kweli ipo! Ni kitu halisi na dhahiri kabisa..Na ni maelfu ya watu shetani anaofanikiwa kuwapeleka huko.

Ni matumaini yangu kuwa Bwana atakupa macho ya kuliona hilo, ili uiepuke ghadhabu yake..

Bwana azidi kukubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE.

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

JE! KUCHORA TATTOO NI DHAMBI?

MWANAMKE YEZEBELI

KUZIMU NI MAHALI PA NAMNA GANI, JE! HUKO WANAISHI WATU WAKIFA NA KWENDA KUPATA MATESO AU NI VINGINEVYO?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Zioens bankurunaze
Zioens bankurunaze
3 years ago

Huduma hii inanifanya nimjue mungu naye mtumikia,
Nashukuru mbarikiwe nanyi.

Zieons bankurunaze
Zieons bankurunaze
3 years ago

Naomba kuwa mwanafuzi wakristo

evasong
evasong
3 years ago

Asante sana msikate tamaa lakini hata hivo siku hizi kuna mavazi siyo ya kiume wala sio ya kike yapo tu kwa hajili ya kuwaharibu walimwengu .kuna suluali za kiume zinazo bana saaana na vijana wa sijuhizi wanazikimbilia sana .mungu atusamehe vijana naomba mbadilike ufalme.wa MUNGU unatekwa na wenye nguvu