WALIOITWA NI WENGI, ILA WATEULE NI WACHACHE.

WALIOITWA NI WENGI, ILA WATEULE NI WACHACHE.

Kama Ukijifunza Biblia kwa undani utagundua kuwa Bwana Yesu hakuwa na wanafunzi 12 tu! Bali alikuwa na wanafunzi wengine wengi sana Zaidi ya 70 biblia inasema hivyo katika (Luka 10:1-2)…Lakini baadaye alikuja kuteua wanafunzi 12 tu miongoni mwao wakutembea naye kila mahali alikokwenda ambao aliwaita Mitume. 

Sasa kama ukizidi kufuatilia kwa makini, utagundua kuwa Bwana Yesu alianza kwanza kuchagua wanafunzi wake wengi katika hatua ya Kwanza, ikiwemo wale 12, kwahiyo tuseme lilikuwepo jopo la watu kama 80 hivi waliochaguliwa na Bwana, na ni wazi kuwa wote Bwana aliowaita aliwaambia kuwa watakuwa na shughuli ya uvuvi wa watu…alipita huko na huko kuwaita kutoka katika ulimwengu, katika njia ile alikutana na mvuvi Petro akamwita, katika njia nyingine akakutana pengine na fundi wa nyumba akamwita, sehemu nyingine akakutana na Mathayo mtoza ushuru akamwita…wengine pengine walikuwa hawana shughuli yoyote wapo mtaani akawaita, likawa kundi moja la watu kama 80 hivi walioitwa….Na wote walioitwa walikuwa sawa machoni pa Bwana Yesu, hakuna aliyekuwa mkubwa zaidi ya mwingine, na wote aliwaambia waache vyote wamfuate, na walimtii..Sasa hiyo ilikuwa ni hatua ya kwanza ya wito..kundi kubwa la wanafunzi liliitwa…. (Kwa somo refu jinsi gani Bwana aliwachagua wanafunzi wake na jinsi anavyowachagua sasa unaweza kututumia ujumbe inbox tutakutumia hilo somo).

Hatua ya pili ilifuata kipindi kifupi baadaye, pengine baada ya miezi kadhaa, ambapo Bwana akaanza tena kuwatenga wanafunzi 12, miongoni mwa lile kundi kubwa la wanafunzi wake…kumbuka hawa 12, hawakuteuliwa moja kwa moja kutoka kwenye ulimwengu, hapana! bali kutoka katika lile kundi la wanafunzi wengine aliokuwa nao…Huo ndio ulikuwa mchujo wa pili, Ndio siku ile Bwana Yesu alipokwenda kukesha kwenye maombi na Mungu akamfunulia mitume 12 miongoni mwa lile kundi…

Luka 6:12 “ Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. 13 Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; AKACHAGUA KUMI NA WAWILI MIONGONI MWAO, ambao aliwaita Mitume; 14 Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, 

15 na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, 

16 na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. 

17 Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; 18 na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa”

Unaona?..Mitume 12 walichaguliwa miongoni mwa kundi la wanafunzi wengi…sasa hawa 12 hawakuchaguliwa kwasababu ya jitihada yao yoyote waliyokuwa nayo, au kwasababu ya utakatifu wao, au kwasababu walikuwa wanajuhudi kuliko wengine, au kwasababu mbele za Mungu wenyewe ndio walikuwa wanaonekana wanaunafuu…Hapana, walichaguliwa kwa Neema tu… Neno ‘neema’ linakaribiana sana kufanana na neno ‘bahati’….lakini sio bahati…Neema ni Zaidi ya bahati, bahati mara nyingine inamwangukia mtu ambaye amestahili, lakini Neema siku zote ni kwa mtu ambaye hajastahili…Hivyo hawa 12 waliochaguliwa katika mchujo wa Pili walipata NEEMA na sio BAHATI. Walikuwa hawastahili kuchaguliwa lakini walichaguliwa…Na hata hao wengine pia sio kwamba hawakuchaguliwa kwasababu walikuwa waovu au kwasababu walikuwa watakatifu sana, hapana! ni uchaguzi tu wa Mungu! Ndivyo ilivyompendeza awachague wale na hao wengine awaache, hatuwezi kuelezea kibinadamu, na wala hatuwezi kumwuliza Mungu kwanini kafanya hivyo! (soma Warumi 9:13-25).

Sasa katika hatua hii ya Pili ndipo linapotimia Neno hili “walioitwa ni wengi ila wateule ni wachache”…Hapo liliitwa kundi kubwa pengine la watu Zaidi ya 80, lakini walioteuliwa kwa Neema kuwa mitume ni 12 tu!.

Lakini bado mchujo unaendelea kwasababu hata miongoni mwa hao walioteuliwa 12, bado kuna uwezekano wa kupotea…Sio kwasababu tu! Umeitwa Mteule basi ndio tiketi ya kusema nimeokolewa…

Biblia inatuambia kuwa hata “wateule wanaweza kudanganyika”.

Mathayo 24:23 “Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. 

24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; WAPATE KUWAPOTEZA, KAMA YAMKINI, HATA WALIO WATEULE.

25 Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.

 26 Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki.

 27 Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu”.

Yuda alikuwa miongoni mwa wateule 12, lakini alidanganyika na kupotea!…na hapo biblia inatuonya kuwa katika siku za mwisho watatokea makristo wa Uongo, watatoa ishara na maajabu wapate kuwapoteza kama yamkini hata walio wateule…

Wakati huo tunaoishi ni sasa, wateule wanaozungumziwa hapo ni wale wote ambao Bwana ameshawaita watoke katika ulimwengu, na kuwateua miongoni mwa watu wake, na kuwapa neema ya kuzijua siri za ufalme wa mbinguni kama wewe unayesoma hapa…Kumbuka sio mambo yote Bwana Yesu alikuwa anawaambia makutano, ni machache sana ndio alikuwa anawaambia makutano, siri zake nyingi alikuwa anawafunulia wale mitume 12 tu aliowachagua…wengine wote alikuwa anawafundisha kwa mifano…

Mathayo 13:10 “Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? 

11 Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa”.

Unapopata Neema ya kusikia injili popote pale, tena unapata kuzijua siri za ufalme wa mbinguni ambazo wengine hawazioni wala kuzipata, na kuna kitu ndani kinakushuhudia kuwa ni kweli… fahamu kuwa wewe ni mteule, lakini katika hizi siku za mwisho wateule wengi watadanganyika kama tu vile Yuda alivyodanganyika na kuishia kumsaliti Bwana Yesu… Yuda alishawishika kabisa ndani ya moyo wake kumwamini Bwana Yesu katika hatua za kwanza za wito wake, alipata ufunuo kabisa kuwa Yesu ndiye masihi aliyetabiriwa, na hivyo akaingia gharama ya kuacha kila kitu na kumfuata Yesu, kwasababu hakuna mtu yeyote ambaye angemfuata Yesu bila kuacha kila kitu na kujikana nafsi yake, Yuda alifanya vyote hivyo, aliitikia wito inavyopaswa….lakini ilifika wakati akaanza kulizoelea Neno, akaanza kuingiwa na tamaa ya vitu vya ulimwengu, akaanza wizi kidogo kidogo, akaanza kuipenda dunia kidogo kidogo, Bwana hakumfukuza asiambatane naye, alimwacha mpaka mwisho, wala upako wake haukukatika aliendelea nao alitoa pepo na kuombea watu kama kawaida na kupokea uponyaji, lakini mwisho wake ulikuwa mbaya, alipasuka matumbo (Matendo 1:16-20).

Na hata leo, ulianza vyema kusikia injili na kuamua kumfuata Yesu kwa moyo, hapo ni Bwana alikuita kweli na akakuteua kuwa karibu naye Zaidi ya wengine, uliacha vyote na kumfuata…lakini imefika kipindi sasa umelizoelea Neno, umeoza ndani, unamwibia Bwana, umekuwa ni mwana wa ulimwengu huku, huku bado unatembea na Yesu, kumbuka Bwana hatakufukuza wala hatakutenga, ataendelea kutembea nawe kama alivyotembea na Yuda, wala hataonesha dalili ya kukudharau wala kukuvunjia heshima, na wala nguvu ya kufanya miujiza hatakupokonya, lakini mwisho wako utakuwa kama wa Yuda!…ili maandiko yatimie , Yuda alikuwa ni mteule lakini Bwana alisema ni kheri asingezaliwa mtu kama huyo kuliko mambo mabaya ambayo yatakwenda kumpata!…Hebu fikiria Mtu aliyeteuliwa na Mungu mwenyewe anaambiwa maneno hayo?.

Ndugu hizi ni siku za mwisho sana, Hayo ya akina Yuda yalitokea ili kutufundisha sisi watu wa siku hizi za mwisho, kuwa tufanye IMARA WITO wetu na UTEULE WETU. Kama maandiko yanavyotuambia..

2 Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi KUFANYA IMARA KUITWA KWENU NA UTEULE WENU; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.


Imarisha wito wako ewe Mteule. Ni wakati wa kumrudia Bwana pasipo mguu mmoja nje wala mguu mmoja ndani, kabla wakati wa kupasuka matumbo haujafika, kabla wakati wa kujutia kama Yuda haujafika, kabla wakati wa kula tonge la mwisho la Bwana, na shetani kukuingia haujafika, siku hiyo mlango utakuwa umefungwa, Yuda baada ya kulila lile tonge shetani alimwingia, ikawa ndio mwisho wake pale. Tengeneza wakati wako, linda wito wako na utendee kazi uteule wako.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

UMEITIKIA WITO INAVYOPASWA?

JE! UMECHAGULIWA KABLA YA KUWEKWA MISINGI YA ULIMWENGU?

JE! KARAMA NI UTHIBITISHO WA KUWA NA MUNGU?


Rudi Nyumbani


Maran atha!

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Dr.Frank
Dr.Frank
2 years ago

Hakika Bwana nimukuu anawatumieni kwa wakati ulio faa
Tumepokea wito wa jina la Bwana na kubarikiwa pamoja na ndugu na majirani
Bwana awape nguvu kazi yenu ikazidi kuwa wokovu kwa w
alio gizani bado,
Ahsante.

John Messa
John Messa
4 years ago

Bwana yesu asifiwe. Nimependa mafundisho yenu na ningependelea munitumie mengine kwenye email yangu. Nimebarikiwa sana na nimeona ni vizuri na mimi kufundisha haya mafunzo yenu. Yamenijenga sana kabisa.