JINSI EDENI ILIVYOKUWA.

by Admin | 30 May 2019 08:46 pm05

Shalom, mwana wa Mungu karibu tujifunze maneno ya Uzima, yaliyo taa ya miguu yetu (Zaburi 119:105). Leo tutaona mwonekano wa Edeni ulivyokuwa hapo mwanzo na sasa ulivyo. Ukisoma kitabu cha Mwanzo, utaona baada ya Mungu kumaliza kuumba mbingu na nchi na vitu vyote tunaona alifanya tena kazi nyingine ndogo ya ziada, nayo ni kutengeneza BUSTANI. Bustani hii Mungu aliifanya mashariki mwa Eneo linaloitwa Edeni, aliitengeneza kuwa makao ya kiumbe chake maalumu kinachoitwa Mwanadamu. Mungu alikipa heshima ya kipekee mpaka kumtengenezea makao ndani ya makao, Bustani hii ilikuwa ni tofauti kabisa na maeneo mengine ya Dunia yaliyosalia.

Hivyo pale bustanini Mungu aliweka kila kitu ndani yake kinachomfaa na kumtosheleza mwanadamu.. Edeni tunaweza kusema ulikuwa ni kama mji mkuu wa Adamu, na ile Bustani ni Kasri lake. Wanyama wote na viumbe vyote viliweza kuishi nje ya Edeni lakini Adamu hakuishi nje na Bustani ile Mungu aliyompa.

Mwanzo 2:8 “Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.

9 Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

10 Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne.

11Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu;

12 na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham.

13 Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi.

14 Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati.

15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.

Zipo sababu kwanini Mungu hakumwambia Adamu akaishi mahali popote tu anapopapenda duniani. Sababu mojawapo ni kwamba huko kwingine Mungu hakuweka utukufu wake wa kiungu kama ilivyokuwa pale Bustanini Edeni, na ndio maana Mungu alipotaka kuzunguza na Adamu alizungumza naye pale bustanini tu. Na pia kumbuka mahali popote utukufu wa Mungu upo, mahali hapo kunakuwa na (UTAJI) WIGO fulani au ULINZI Fulani. Adui au chochote kisichohusika hakiwezi kupenyeza.

Ili kulielewa hili vizuri tunaweza kujifunza katika mambo yanayotuzunguka ya kila siku. Siku hizi kuna kilimo kijulikanacho kama “ kilimo cha Banda-kitalu” kwa lugha ya kigheni iliyozoeleka na wengi kinaitwa GREEN HOUSE farming. Kilimo hichi hakina tofuati na kile kingine isipokuwa tu, hichi mmea au mboga, au matunda, au maua huwa yanawekwa katika banda maalamu lililozibwa pande zote katika uzalishaji wake. Na wanafanya hivyo sio kwasababu wamependa tu iwe hivyo hapana, lakini kama wewe ni mkulima mzuri utajua kuwa kulima mazao yako katika green-house, kuna faida kubwa kuliko kulima huria, sababu kubwa kwanza ni kinazuia wadudu waharibifu wa mazao kuvamia shamba, pili kinazuia mionzi mikali ya jua kuharibu mimea, hivyo inasaidia kuhifadhi unyevunyevu na kutokutumia gharama nyingi za kupiga madawa, kwa ajili ya wadudu. Na matokeo yake ile mimea huwa inakuwa vizuri, yenye afya, na mwisho wa siku kuleta mazao mengi kuliko hata Yule ambaye yalilimwa mabondeni tu. Huyu anaweza akajiona analoshamba kubwa, lakini mimea ikiaanza kumea tu wadudu waharibifu wanakuja, na hivyo atajikuta anahangaika kupiga madawa, mimea inaliwa na kukosa mvuto na hata akifanikiwa kupeleka sokoni bidhaa yake hainunuliwi kwasababu inakuwa haina ubora unaostahili. Maua mengi ya thamani kama Maua Rose, yanalimwa ndani ya Green house, nje na hapo matokeo yatakuwa hafifu, na ndio maana unaona ubora wake na thamani yake ni kubwa.

Sasa chukua mfano huo huo urudishe pale Edeni, Mungu alimweka Adamu katika GREEN-HOUSE yake, ambayo ndio ile bustani, akamwekea wigo mkubwa wa utukufu wake, na ndio maana chakula na kila kitu kilikuwa kinajiotea tu chenyewe katika ubora wote ndani ya bustani ile, hiyo yote ni kwasababu hakukuwa na viumbe viharibifu vilivyoingia na kugeuza mambo. Lakini sasa baada ya wao kumpa nafasi NYOKA, nyoka akawadanganya walitoboe HEMA lao, na walipofanya vile tu, basi lile hema lote likapasuka, kukawa hakuna ulinzi tena wowote wa bustanini, wanyama hawaribifu wakaanza kuingia. Ndio tunaona pale Mungu anaanza sasa kuwaeleza matokeo yatakayofuatana nao kwa kosa walilolitenda..Adamu atakula kwa jasho, nchi itamzalia michongoma, na mwisho wa siku atakufa tu.

Sasa hayo yote yalikuwa katika mwili, ingekuwa ni heri tu kama yangeishia hapo, lakini fahamu lengo kubwa habari nzima inayoelezwa hapo lengo lake ni kuturudisha katika roho, ni kutuonyesha kwa lugha ya vitendo vya kimwili mambo yaliyofanyika rohoni eneo lile..Sasa katika huu upande mwingine wa roho, ni Shetani mwenyewe alimvaa nyoka ili kumshawishi mwanadamu avunje agano la ulinzi waliowekewa na Mungu katika roho. Kumbuka shetani alipoasi yeye pamoja na malaika zake alitupwa chini, hivyo alikuwa yupo huku chini katika giza, lakini alipoona Mungu kaitengeneza tena nchi upya na kila kitu amepewa mwanadamu, huku yeye hana chochote anasubiri hukumu yake ya mwisho. alitumia ujuzi kutafuta namna ya kuoondoa ulinzi wao ili aingie na kuuharibu uzao wa Mungu kama alivyofanya huko mbinguni..(Yohana 8:44 ….Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo;). kama vile tu wale wadudu wahaaribifu wa mazao.

Na alipofanikiwa kuwashawishi Adamu na Hawa ili wauvunje ulinzi wao kwa Mungu, ndipo akapata nafasi ya kuingia na kuanza kuuwa uzao wa Mungu kiroho. Sasa mambo kama dhambi na uasi vikaanza kuingia, maovu ya kila namna yakaanza kujaa ndani ya wanadamu, vitu ambavyo mwanadamu hakuwahi kuwa navyo, uuaji sio asili wa mwanadamu, uchawi sio asili ya mwanadamu n.k…Vifo vya kiroho vikawa vingi.

Mwanzo 3:22 “Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele;

23 kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.

24 Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka hukona huko, kuilinda njia ya mti wa uzima”.

Lakini ashukuriwe Mungu, Edeni ya rohoni haikufutwa kabisa, bali Mwanadamu alifukuzwa tu, hii ikiwa na maana kuna wakati Mungu aliuweka kuwa watu wake watapata njia ya kuirudia Edeni hiyo. Na leo hii tunafahamu kuwa njia ya kurudia huko ni BWANA YESU TU.

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”.

Shetani naye hajalala anaendelea kupiga vita ili kuzuia watu wasiirudie Edeni yao anafanya hivyo kwa nguvu ili azidi kuwatesa na kuwaua rohoni na mwisho wa siku waende kuzimu..Ndugu YESU alishalipa gharama kwa ajili yako, kwanini unaruhusu mwingine achezee roho yako kama mpira?. Ukiwa bado unaendelea kuteswa na dhambi hiyo ni umejitakia wewe mwenyewe, ikiwa bado unaendelea kuteswa na mapepo na nguvu za giza hiyo ni umejitakia wewe mwenyewe, ikiwa bado unaishi kwa mashaka na hofu kwamba ukifa leo hujui utakwenda wapi hiyo ni umejitakia mwenyewe.. Kwasababu Yesu alishatuita na kutuahidia raha, tumaini na uzima wa milele bure..yeye ndiye safina yetu sasa, yeye ndiye green house yetu halisi ukiwa ndani yake una uhakika wa ulinzi wa kutosha na roho yako itakuwa salama.

Ushauri wangu ni kuwa kama bado hujayakabidhi maisha yako kwa Bwana kwa kumaanisha kabisa, fanya hivyo leo haraka, kwani shetani hana urafiki na wewe anataka ufe leo katika hali hiyo hiyo na mwisho wa siku uende kuzimu. Ukiwa ndani ya YESU utakuwa na amani na tumaini,..Yeye mwenyewe ameahidi kukupa raha nafsini mwako. Hivyo piga hatua utubu dhambi zako hapo ulipo na yeye atakupokea, Kisha chukua hatua nyingine ya Imani ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamwishwa kwa jina la YESU KRISTO ikiwa bado hujafanya hivyo. Na Mungu atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu.

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:
EDENI YA SHETANI:
MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA.
UTAWALA WA MIAKA 1000.


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/05/30/jinsi-edeni-ilivyokuwa/