lakini katika sura hii tukisoma kuanzia mstari wa 1-3 tunaona shetani akikamatwa na kufungwa na kutupwa kuzimu, kwa muda wa miaka 1000, kumbuka huyu hakutupwa katika lile ziwa la moto kama wale wengine, huyu atafungwa kwa kitambo tu akingojea kuja kufunguliwa baadaye kwa kazi maalumu na kisha ndio aje kutupwa katika lile ziwa la moto aliyomo yule mnyama na nabii wa uongo.
Kuna vitu kadhaa vya kuzingatia hapo…
1) Malaika akishuka kutoka mbinguni. Huyu ni mmoja wa Malaika watakatifu, kumbuka kuna malaika walioasi ambao waliungana na shetani, na kuna waliobaki kuwa waaminifu kwa Mungu, na wametofautiana kimaumbile na uwezo, wapo malaika wa vita na wa sifa n.k na huyu ni mmoja wapo wa vita kwasababu tunaona ameshika mnyororo mkononi mwake..
2) mwenye ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake…Kumbuka Bwana Yesu Kristo baada ya kushinda mauti alizitwaa funguo zote za mauti na kuzimu, kwahiyo watu wote walio hai na waliokufa wapo chini yake yeye…anao uwezo wa kumshusha mtu kuzimu na kumpandisha, huo uwezo anao ndio maana siku za mwisho atawafufua watu wote ambapo wengine atawapa uzima wa milele wengine atawafufua kwa hukumu, hivyo kama anao huo uwezo ni lazima atakuwa na uwezo pia wa kumshusha mtu au kiumbe chochote kuzimu, na ndio hapa tunaona anampa huyu malaika funguo hizo ambazo ni amri ya kumkamata shetani na kumtupa kuzimu. Kuzimu iliyozungumziwa hapa ni SHIMO REFU LISILOKUWA NA MWISHO ( Bottomless Pit).
Huko hakuna raha sana, ni sehemu mbaya ya uchungu ambayo iliwekwa maalumu kwa malaika walioasi sio wanadamu…wanadamu walioasi sasa wanaokufa wanakwenda sehemu yao (kuzimu yao ambayo hiyo na yenyewe ina mateso lakini sio makali kama ya hawa malaika walioasi…(Mapepo na yenyewe yanayokuzimu yao ambapo yakifanya jambo lisilopasa yanakwenda kutupwa huko).
Ndio maana wakati Fulani Mapepo yalimsihi Bwana yasipelekwe shimoni, baada ya kumtesa Yule mtu wa Pwani ya wagerasi…yalijua Bwana tayari alichukizwa na jambo lile la kumtesa Yule mtu anazo amri za kufunga na kufungua..na yalijua endapo Bwana angetamka Neno tu la wao kwenda shimoni, habari yao imeisha….huko shimoni ni mahali ambapo wanafungwa na kuna mateso yasiyoyakawaida.
Luka 8: 30 “Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia.
31 Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni.
32 Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa”.
Na mpaka sasa kuna baadhi ya mapepo yamefungwa huko biblia inasema hivyo…kwa maelezo marefu kuhusu roho za mapepo zilizopo kifungoni bonyeza hapa >> ‘‘Vifungo vya Giza vya Milele”
Sasa shetani naye atakamatwa na kwenda kutupwa shimoni, mule mapepo yalipomwomba Bwana asiwapeleke. Atakaa kule kwa muda wa miaka 1000, akionja uchungu mkali kuliko wa wanadamu..Na hatakwenda peke yake bali na mapepo yote pamoja naye…duniani hakutabaki na roho yoyote chafu..watakaa kule kwa maumivu kwa miaka 1000..Kumbuka hilo sio ziwa la Moto…ziwa la Moto litakuja kuzinduliwa rasmi na yeye mwenyewe(shetani) baada ya hukumu ya kiti cheupe ambayo tutakuja kuiona huko mbeleni.
Ufunuo 20:3 “akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache”.
Baada ya kufungwa tunaona pia ukatiwa muhuri juu yake, Nia ya kutiwa muhuri ni “ili asiwadanganye tena mataifa hata itimie miaka elfu”…Muhuri kazi yake ni kuzuia kitu Fulani kisiendelee juu ya huyo mtu/kitu kwa kipindi Fulani cha muda…Hapa shetani baada ya kufungwa nguvu za upotevu zinaondolewa juu yake, anakuwa hana kitu tena..
Kadhalika na watu wa Mungu wana Muhuri wanaotiwa na Mungu ambao huo Mungu anawatia ili wasipotee au wasidanganywe tena mpaka siku ya ukombozi wao..Na huo Muhuri sio mwingine zaidi ya Roho Mtakatifu…
Waefeso 4:30 ” Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.”
Kundi la pili ni wale waliofufuliwa ambao waliuawa na mpinga-kristo katika ile dhiki kuu, kwa kukataa kusujudia sanamu yake na kupokea chapa katika vipaji vya nyuso zao, hapa watakuwa ni wayahudi na wakristo, hawa nao watafufuliwa na kupewa miili ya utukufu na kuingia katika ule utawala wa miaka 1000 pamoja na Kristo ,huo ndio ufufuo wa kwanza, lakini wafu wengine wote waliosalia ikiwemo watu wote walioipokea ile chapa ya mnyama pamoja na watu wote waovu, hawatafufuliwa mpaka ile miaka 1000 itakapoisha, biblia inasema Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Kumbuka hatutakaa mbinguni milele, bali biblia inasema makao yetu yatakuwa na Bwana hapa duniani milele.
Kuna hatari kubwa sana ya kukosa unyakuo, au kufa katika dhambi sasa, kutakuwa hakuna nafasi ya pili, inatisha sana!!
Sasa anaposema vitabu anamaanisha ni vingi, na hivi si vingine zaidi ya maisha ya kila mmoja wetu alivyoishi hapa duniani,na kile kitabu cha uzima kipo kimoja tu na si kingine zaidi ya NENO LA MUNGU(biblia), na kama unavyosoma hapo kama jina lako halikuonekana katika kile kitabu cha uzima ikiwa na maana kuwa kama MATENDO YAKO(ambayo ndio kitabu chako) hayaendani na kile KITABU CHA UZIMA(yaani biblia) sehemu yako itakuwa ni katika lile ZIWA LA MOTO. Kumbuka biblia inasema “sisi ni BARUA inayosomwa na watu wote” ikiwa na maana maisha yetu ni “KURASA ZINAZOANDIKWA” na kila siku tunafungua ukurasa mpya, siku utakapokufa kitabu chako kitakuwa kimeisha na kufungwa…kinasubiriwa kufunguliwa tena katika ile siku ya hukumu, sasa jiulize! je leo hii kitabu chako unakiandikaje? je maisha yako ya jana na ya leo yanaendana na kile kitabu (Neno la Mungu). Angalia muda unavyokimbia usije ukasema nitatubu siku nitakayokaribia kufa au nikiwa mzee, wakati huo pengine kitabu chako kitakuwa hakina maana tena au hakikidhi viwango vya kufanana na kile kitabu cha uzima, na hiyo ndio maana ya “KUKOSEKANA JINA LAKO KATIKA KILE KITABU CHA UZIMA”.
Na baada ya haya yote kuisha BWANA YESU atakuwa amekwisha waweka maadui zake wote chini na adui wa mwisho ni MAUTI, Kisha baada ya hapo UMILELE unafunguliwa usio kuwa na dhambi,wala vita,wala shida, wala waovu,wala maumivu,wala shetani wala mapepo. Ni MBINGU MPYA NA NCHI MPYA, tutaendelea kujifunza katika sura zilizosalia juu ya hayo.
Je! Leo hii bado unaendelea kuishi maisha ya kutokujali, unavaa vimini, unakuwa mzinzi,mlevi,mtu wa mizaha,msengenyaji, mpenda anasa, mtukanaji,n.k kumbuka biblia ilishaonya kuwa watu kama hao sehemu yao itakuwa katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti, hivyo ndugu maombi yangu ni utubu umgeukie Bwana Yesu angali bado unayo nafasi ya kukiandika kitabu chako vizuri.