NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

SWALI: Je Mungu anazaa?..Kama hazai kwanini sisi tunaitwa Watoto wa Mungu?..Je! Mungu ana mke?..na kama hana huoni kama ni kukufuru kusema kuwa sisi ni Watoto wa Mungu?


JIBU: Swali hili linaulizwa sana na watu wa Imani nyingine Lakini ni vizuri kufahamu kuwa Tukisoma Biblia kwa haraka haraka tu! au tukiitafsiri kwa fahamu zetu za kibinadamu pasipo sisi wenyewe kutenga muda kutafuta msaada wa Roho Mtakatifu kwamba atujalie Neema ya kuyaelewa maandiko tutaishia kukwama tunapoisoma biblia.

Kwasababu biblia inasema…2Wakorintho 3:6 “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha”.

Hapo inasema andiko huua, bali Roho huhuisha…maana yake ni kwamba tukiyatafsiri maandiko bila msaada wa Roho tutaishia kupotea tu au kuiona biblia ni kitabu cha uongo…. Hivyo maandiko pekee bila Roho yatatupoteza….

Sasa tukirudi kwenye swali letu linalouliza..ni kwa namna gani sisi ni watoto wa Mungu?…ili kuelewa sisi tuliomwamini Yesu Kristo ni wana wa Mungu kwa namna gani…hebu turudi kutafakari Maisha ya kawaida tunayoyaishi sisi wanadamu. Katika kuyatafakari hayo kwa makini tutaweza kuelewa ni kwanini sisi (Tuliomwamini Yesu Kristo tunaitwa wana wa Mungu).

Hebu tumtafakari mtu mmoja maarufu aliyeitwa Julius Nyerere…ambaye alifanya jambo fulani la kishujaa la kwenda kuliletea taifa letu uhuru wakati huo…na kulifanya Taifa la Tanganyika kuzaliwa rasmi mwaka 1961, Sasa Kwa hekima za kibinadamu tunaweza kusema yeye ndiye aliyelizaa Taifa hili,..kwasababu kama si yeye kwenda kutafuta uhuru, bado kusingekuwa na Taifa linaloitwa Tanganyika na baadaye likaja kuwa Tanzania, linalojitegemea lenyewe, lenye serikali yake, lenye katiba yake, na mipango yake… hivyo si vibaya kumwita yeye Baba wa Taifa hili.…maana yake ni Baba wa Nchi hii…

Na sisi Raia tuliozaliwa ndani ya nchi hii tunajulikana kama wana au watoto wa nchi hii, ndio maana tunaiwa WANA-NCHI..akiwa mmoja anaitwa Mwana wa nchi hii (kwa kifupi mwana-nchi)..wakiwa wengi wanaitwa wana-nchi.

Kwahiyo mpaka hapo tumeshaona kuna BABA WA NCHI ambaye ni Mmoja aliyeitwa Julius na pia tuna Wana wa nchi ambao ni wengi..Na tumeshajua ni kwanini sisi Raia tunaitwa wana-nchi na kwanini Julius Nyerere anaitwa Baba wa Nchi, au Baba wa Taifa.

Sasa katika ufahamu huo..Hebu tafakari mtu mmoja anakuja na kuhoji… “Nyerere si Baba wa Taifa hili/nchi hii… ni lini Nyerere alioa akaizaa hii nchi? Mke wa Nyerere ni nani ambaye alimuoa na kuzaa naye watoto mpaka kufikia yeye aitwe Baba wa Taifa?”….Na mtu huyo huyo anaendelea kuhoji..sisi sio watoto wa hili Taifa wala sio wana wa hili nchi?… Ni lini hii nchi ilioa likatuzaa sisi mpaka tujiite sisi ni watoto wa hii nchi?..Mke wa hii nchi ni nani?…Hivyo sisi sio wana-nchi!..Tukijiita sisi ni wana-nchi tunakufuru! Na ni dhambi,.. Kwasababu nchi haiwezi ikaoa wala kuolewa, wala haiwezi kuzaa..hivyo…nakataa nakataa..

Umeona ufahamu wa huyu mtu?..Yeye chochote tu kinachoitwa mwana au mtoto au Baba au chochote ambacho kimezaliwa kwake anakitafsiri kwamba ni lazima kiwe aidha kimeoa, au kimeolewa kimwili… Sasa kwa ufahamu kama huo mtu wa namna hiyo ni ngumu kuelewa chochote. Mpaka atakapokubali kutulia kwanza na kukubali kujifunza ndipo atakapoelewa..

Kadhalika sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo tunapoitwa wana wa Mungu au watoto wa Mungu…haimaanishi kuwa Mungu anazaa au ameoa, au ana mke na akatuzaa sisi..tukitafakari kwa namna hiyo bado ufahamu wetu utakuwa umefumbwa na hatutaweza kumwelewa Mungu kamwe…ingawa pengine tunaweza tukajiona tuna hekima.

U-wana wetu sisi ni wa namna ya Roho…sio wa namna ya mwili…Biblia inasema katika..

Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;

13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu”.

Tunapomwita Mungu wetu Baba ni kwasababu yeye ndiye chanzo cha uzima wetu na yeye ndiye aliyeutengeneza ufalme wa mbinguni…na kwa neema akatupa huo…Hivyo sisi ni wana wa huo ufalme!…kama vile tulivyo wana wa hii nchi..

Je umeelewa sasa?…Je! unataka leo kufanyika mwana wa Mungu?….Njia pekee ya kufanyika mwana wa Mungu ni kumwamini Yesu Kristo…Huwezi kufanyika mwana wa Mungu kama hujamwamini Mwana pekee wa Mungu Yesu Kristo.. “Wagalatia 3:26 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.

YESU ANAWAPENDA WATU WOTE:

Hivyo mwamini leo kwa kutubu na kumwambia kuanzia leo nakuhitaji Ee Yesu mwokozi wangu… nadhamiria kabisa kuacha dhambi na kwenda kubatizwa na kulishika Neno lako, karibu moyoni mwangu nifanye kiumbe kipya, nabeba msalaba wangu kuanzia leo na kukufuata wewe, nishike mkono na kuniongoza njia yangu yote mpaka nitakapoimaliza safari yangu hapa duniani. Naomba pia unifanye sababu ya kuwa wokovu kwa wengine.”….

1Petro 2:9 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu”

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia masomo kwa njia ya whatsapp ya kila siku basi, bofya hapa uweze kujiunga >>> WHATSAPP Au tuandikie kwa namba hizi +255789001312

Mada Nyinginezo:

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU WATOTO.

MJUE SANA YESU KRISTO.

WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

Tofauti ya deni na dhambi ni nini?

Furaha ni nini?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments